Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kakama inavyoipa nguvu Burundi kukuza, kuimarisha Kiswahili EAC

Muktasari:

  • Kamisheni ya Kiswahili Jumuiya ya Afrika Mashariki inashirikiana na mabaraza ya Kiswahili katika nchi wanachama nane kuhakikisha lugha hiyo inaimarika kimatumizi na kuwezesha maendeleo endelevu.

Burundi imeendelea kuonyesha kivitendo kuwa inaipa lugha ya Kiswahili nafasi muhimu katika kuimarisha mawasiliano, biashara, elimu na ushirikiano ndani ya Jumuiya Afrika Mashariki.

Mwelekeo huo umejidhihirisha kupitia kuwa mwenyeji wa Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kiswahili pamoja na maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika Bujumbura, yakiratibiwa na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (Kakama) chini ya Katibu Mtendaji, Dk Caroline Asiimwe kuanzia Julai 5 hadi 6, 2026 na kufuatiwa na maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani Julai 7.

Tukio hilo liliwakutanisha viongozi wa serikali, wataalamu wa lugha, wanataaluma, watafiti na wadau wa teknolojia kujadili nafasi ya Kiswahili katika maendeleo ya ukanda.

Kukubali kuwa mwenyeji wa kongamano hilo kulikuwa zaidi ya kuandaa mkutano wa kitaaluma. Ilikuwa ni ishara kwamba Burundi inakiona Kiswahili kama nguzo muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda. Kama mwanachama wa EAC, Burundi inatambua kuwa mawasiliano yenye ufanisi kati ya wananchi wa nchi wanachama yanahitaji lugha ya pamoja inayoweza kueleweka kwa urahisi.

Kiswahili ndicho kinachotimiza jukumu hilo kwa kuwa ni lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na mojawapo ya lugha zinazotumiwa na mamilioni ya watu.

Katika kongamano hilo, washiriki walijadili namna Kiswahili kinavyoweza kutumika katika elimu, biashara, utawala na teknolojia za kisasa, hususan akiliunde.

Mjadala huo unaonyesha kuwa Burundi haitazami Kiswahili kama lugha ya mawasiliano ya kawaida pekee, bali kama nyenzo ya maendeleo inayoweza kuongeza ushindani wa wananchi wake katika uchumi wa kikanda na wa dunia.

Kadiri matumizi ya teknolojia yanavyoongezeka, ndivyo umuhimu wa kuwa na maudhui ya Kiswahili kwenye mifumo ya kidijitali unavyozidi kuonekana.

Burundi pia imekuwa ikiongeza juhudi za kukuza ufundishaji na matumizi ya Kiswahili katika taasisi mbalimbali za elimu. Hatua hiyo inalenga kuwaandaa vijana na wataalamu kuwasiliana kwa urahisi na wenzao kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini. Kwa kufanya hivyo, wananchi wa Burundi wanapata fursa kubwa zaidi.

Kwa upande wa biashara, umuhimu wa Kiswahili unaonekana wazi kutokana na nafasi ya Burundi katika biashara za mipakani. Wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao na nchi jirani hutegemea Kiswahili katika mazungumzo ya kila siku, hivyo kukifanya kuwa chombo muhimu cha kujenga uhusiano wa kiuchumi. Hali hiyo imechangia kuongezeka kwa hamasa ya kujifunza na kutumia lugha hiyo katika sekta mbalimbali.

Aidha, kongamano la Bujumbura limeonyesha kuwa Burundi inaunga mkono juhudi za Kakama za kuifanya Kiswahili kiendane na mabadiliko ya teknolojia na maendeleo ya dunia.

 Washiriki walisisitiza umuhimu wa kuendeleza tafiti, kuongeza maudhui ya Kiswahili katika mifumo ya kidijitali na kuimarisha ushirikiano wa kikanda ili lugha hiyo iweze kutumika kikamilifu katika nyanja za sayansi, teknolojia na ubunifu.

Hatua ya Burundi kuwa mwenyeji wa kongamano hilo ni uthibitisho wa dhamira yake ya kuifanya Kiswahili kuwa nyenzo ya kuunganisha wananchi wa Afrika Mashariki.

Kupitia ushiriki wake katika shughuli za Kakama na juhudi za kupanua matumizi ya lugha hiyo, Burundi inaonyesha kuwa mustakabali wa ushirikiano wa kikanda unategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa lugha moja inayorahisisha mawasiliano, na Kiswahili kinaendelea kuthibitisha kuwa ndicho chaguo muhimu zaidi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Gadi Solomon, ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili. +2557127912