Kila mtu atimize wajibu kudhibiti ubakaji

Kila mtu atimize wajibu kudhibiti ubakaji

Muktasari:

  • Takwimu za Jeshi la Polisi nchini zimeonyesha kupanda kwa kasi ya matukio ya ubakaji kutoka 5,803 yaliyoripotiwa mwaka 2015 hadi 7,263 mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 25.95.

Takwimu za Jeshi la Polisi nchini zimeonyesha kupanda kwa kasi ya matukio ya ubakaji kutoka 5,803 yaliyoripotiwa mwaka 2015 hadi 7,263 mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 25.95.

Ripoti ya polisi inaendana na nyingine iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya mwaka 2020 ikionyesha kuwa kwa mwaka huo zaidi ya matukio 7,388 yaliripotiwa, sawa na wastani wa matukio 615 kwa mwezi.

Ubakaji ni miongoni mwa vitendo vya ukatili ambavyo vinawaweka wanawake na watoto wa kike kwenye hali ya hatari.

Vitendo hivi vinahusisha ndoa za utotoni, ukeketaji wa watoto wa kike, ubakaji na unyanyasaji wa watoto kijinsia ambavyo mara nyingi huwaachia waathirika madhara ya muda mrefu ya kimwili na kiakili.

Miongoni mwa sababu zinazoelezwa kuchochea kuongezeka kwa matukio hayo ni utandawazi, mmomonyoko wa maadili, ukosefu wa elimu ya dini na matumizi ya vileo kama pombe na dawa za kulevya.

Kuna kesi zimewahi kuripotiwa kwamba baba amekamatwa kwa kumbaka binti yake wa kumzaa au binti wa kumlea, hii ina maanisha kuna ukosefu mkubwa wa maadili.

Cha kushangaza ni kwamba kwa mujibu wa ripoti ya LHRC ya mwaka 2015, asilimia 90 ya wahusika wa ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto ni wanafamilia na ndugu wa karibu kwa watoto. Pia, kwamba wahusika wengine ni marafiki, walimu, majirani na wakati mwingine viongozi.

Vilevile, kuna wakati hata baadhi ya viongozi wa dini wasio waadilifu na wanasiasa nao wamekuwa wakitajwa kuhusika na vitendo hivyo.

Hali hii inasababisha ugumu katika kuwachukulia hatua watuhumiwa, kwani mara nyingi masuala haya humalizwa kifamilia.

Ni ukweli kwamba hali hii pia inarudisha nyuma upatikanaji wa haki kwa waathirika na kufifisha juhudi za Serikali, wanaharakati na taasisi mbalimbali za kutetea haki na kupinga vitendo hivyo.

Rai yetu kwa Watanzania katika kukabiliana na tatizo hili, kila mmoja ana wajibu wa kuheshimu na kulinda utu na haki za watoto na wanawake.

Haitakuwa sahihi kuendelea kupiga kelele wakati wahusika wako miongoni mwetu na wengine tunawajua, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuchukua hatua sasa, kujenga maadili mema kuanzia ngazi ya familia.

Ni kinyume na utamaduni wa Kitanzania suala la malezi ya watoto kuwaachia wasichana wa kazi pekee au kuwaachia walimu.

Watanzania tutaweza kupambana na tatizo hili, ikiwa kila mmoja atachukua hatua kujenga maadili mema kwa familia yake na kuacha tabia ya kulindana na kuanza kuwafichua wahusika wa vitendo hivyo bila kuoneana aibu.

Tunaamini kwamba wahusika watakapoanza kuchukuliwa hatua za kisheria na ushirikiano wa familia ukiwa mkubwa, kasi ya kuongezeka vitendo hivi itaanza kupungua.

Pia, ni muhimu kudhibitiwa kwa vitendo vya ulevi wa kupindukia, ni imani yetu kwamba hivi navyo huchangia katika kuchochea vitendo vya ubakaji.

Sheria zinazodhibiti ulevi usio na utaratibu maalumu zitumike kuwabana watengenezaji wa pombe za kienyeji na wauzaji kwenye vilabu.

Tunaamini kwamba ikiwa kila mmoja atatimiza wajibu wake kumlinda mwenzake na kuchukua hatua bila kuoneana aibu, vitendo hivi vitapungua.

Pia, ni imani yetu vyombo vya dola navyo vitatekeleza wajibu wake wa kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria wale wote watakaobainika kujihusisha na ubakaji.