Kuna mengi ya kujifunza Ethiopia

Muktasari:

Mambo hayo ni pamoja na usafiri wa anga, matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam, nishati ya umeme, kuimarisha utalii, kuondoa vikwazo vya kufanya kazi kwa raia wa nchi hizo mbili, viwanda, uchimbaji madini, kilimo, mawasiliano na michezo.

Wiki hii, Serikali ya Tanzania na Ethiopia zilitia saini mikataba mitatu ambayo inalenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika mambo 13.

Mambo hayo ni pamoja na usafiri wa anga, matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam, nishati ya umeme, kuimarisha utalii, kuondoa vikwazo vya kufanya kazi kwa raia wa nchi hizo mbili, viwanda, uchimbaji madini, kilimo, mawasiliano na michezo.

Nchi zote mbili zinatarajiwa kunufaika katika mambo hayo na hivyo kuzidi kupiga hatua kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Kama alivyosema Rais John Magufuli, Ethiopia imepiga hatua katika usafiri wa anga, ikiwa ni moja ya mashirika makongwe na makubwa barani Afrika na duniani, Ethiopian Airways na hivyo uzoefu wake utasaidia katika harakati za kufufua Shirika la Ndege la ATCL.

Pia, Ethiopia ina miradi mikubwa ya umeme ambayo itaifanya nchi hiyo iuze nje na hivyo Tanzania kunufaika. Pia, katika miaka ya karibuni, Ethiopia imezipiku nchi za Tanzania na Kenya kwa mapato yatokanayo na utalii, wakati nchi hiyo pia imefanya vizuri katika usafiri wa ndani baada ya kufungua treni ya umeme na pia reli inayokwenda hadi Djibout.

Kwa upande wa kilimo, Ethiopia inasifika kwa kuwa na mifugo mingi na kutumia vyema ngozi ya mifugo yake kwa ajili ya shughuli nyingine kama ushonaji mabegi, viatu na mavazi, wakati wanariadha wake ni mabingwa wa mbio ndefu duniani.

Pia, suala la viza, limekuwa tatizo la muda mrefu kwa wananchi wa Ethiopia na Tanzania licha ya nchi hizi mbili kuwa na uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu. Kuondokana na tatizo hilo, Rais Magufuli na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemarian Desagen wamekubaliana kutafuta njia za kuondoa tatizo hilo na Ethiopia imeamua kufungua ofisi ya ubalozi mjini Dodoma.

Makubaliano hayo yote yataisiaidia Tanzania kupiga hatua sehemu ambazo ilikuwa imekwama kama tulivyoeleza awali kuwa baadhi ya sekta kama za usafiri wa anga, utalii, mawasiliano na matumizi ya bandari bado hatujawa vizuri.

Ni vizuri watakaohusika katika kutekeleza makubaliano hayo wakafanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa ili malengo ya viongozi hao wawili yaweze kutumia.

Lakini, jambo ambalo tungependa waliangalie zaidi ni jinsi Ethiopia ilivyoweza kumudu kupiga hatua hizo katika shughuli za kiuchumi na kuziacha nchi kama Tanzania ambazo zina rasilimali zilezile zinazolingana na za Taifa hilo lililo katika pembe ya Afrika. Ni mwaka 2000 tu, Ethiopia ilikuwa nchi ya pili kwa umaskini duniani, lakini kasi yake ya kuendeleza uchumi itaifanya iwe nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Kati ya mwaka 2004 na 2014, Ethiopia ilipiga hatua za haraka kiuchumi kiasi cha Pato la Taifa kufikia asilimia 10.9.

Kilimo kilichangia kwa kiasi kikubwa kuibuka kwa Ethiopia, ikisaidiwa na kuibuka kwa sekta ya ujenzi na baadaye sekta ya huduma.

Yapo mambo mengi yanayoweza kuelezwa kuwa yalichangia kuimarika kwa uchumi wa Ethiopia. Cha muhimu ni kujifunza kutoka kwao kwamba walifanya. Tunaweza kuwa na miradi mikubwa ya ujenzi, lakini isiwe na matokeo chanya kama Ethiopia.

Maana yake, kuna kitu zaidi ambacho tunaweza kujifunza kutoka kwao ili miradi mikubwa ya ujenzi itakapoanza, tujue kuitumia kuleta matokeo chanya. Hali kadhalika katika kilimo, usafirishaji, bandari, ukusanyaji kodi, utalii na umeme.

Makubaliano haya yatupe fursa ya kujifunza mengi kwa wenzetu wa Ethiopia.