Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuna shida usimamizi wa viwanja      

Katika misimu ya hivi karibuni ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kumekuwa na tatizo linalojirudia mara kwa mara, kufungiwa kwa viwanja vya soka kwa kushindwa kukidhi vigezo vilivyowekwa na Bodi ya Ligi. Kinachoshangaza zaidi ni kwamba viwanja hivyo hivyo hufunguliwa tena baada ya muda mfupi, bila mabadiliko ya msingi yanayoonekana.

Hali hiyo baadaye imekuwa ikisababisha malalamiko mengi, na kupoteza ule ubora wa ligi yetu ambao umekuwa ukionekana kila siku.

Kwanza, ni muhimu kutambua kuwa ubora wa viwanja ni msingi wa maendeleo ya soka. Uwanja bora si tu unalinda usalama wa wachezaji, bali pia huongeza mvuto wa ligi kwa mashabiki, wadhamini na hata vituo vya matangazo. Hivyo basi, kufungiwa kwa viwanja kunapaswa kuwa hatua ya mwisho, siyo sehemu ya mchakato wa kawaida unaojirudia bila tija.

Suluhisho la kwanza ni uwekezaji wa dhati katika miundombinu ya viwanja. Klabu nyingi zinategemea viwanja vya umma ambavyo havitunzwi ipasavyo. Serikali na wadau binafsi wanapaswa kuwekeza kwa pamoja katika ukarabati na ujenzi wa viwanja vya kisasa, mfano viwanja vingi vinavyotumika kwenye ligi siyo mali ya klabu husika, kuna ambavyo ni vya Serikali kama ulivyo ule wa Mkapa na vingine ni mali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ni vyema wakaweka mkakati imara wa kuhakikisha viwanja hivyo vinakuwa bora na kutumika kwa kipindi chote, cha mvua na hata jua kali.

Pili, ni lazima kuwe na ukaguzi wa mara kwa mara unaozingatia viwango vilivyowekwa, lakini ukaguzi huo uwe na lengo la kuboresha badala ya kuadhibu. Badala ya kusubiri mpaka msimu uanze ndipo viwanja vikaguliwe na kufungiwa, Bodi ya Ligi inapaswa kuwa na ratiba ya ukaguzi wa awali kabla ya msimu kuanza na kutoa mapendekezo. Hii itawapa wahusika muda wa kurekebisha kasoro bila kuathiri ratiba ya ligi.

Tatu, uwajibikaji uwekwe wazi, mara nyingi, hakuna uwazi kuhusu nani hasa anawajibika pale uwanja unaposhindwa kukidhi vigezo. Je, ni klabu, halmashauri, meneja au wamiliki? Ni muhimu kuweka mfumo unaoeleza wazi majukumu ya kila mdau. Aidha, adhabu au hatua zichukuliwe kwa wahusika wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao, badala ya kuishia kufungia uwanja pekee na kuipa gharama kubwa klabu ambayo ilikuwa ikiutumia, kwa kuwa wakati mwingine wanakuwa wameshalipa kiasi kikubwa cha fedha.

Nne, elimu na mafunzo kwa wasimamizi wa viwanja ni jambo la msingi. Baadhi ya changamoto zinazojitokeza zinatokana na ukosefu wa utaalamu wa kutosha katika matengenezo ya viwanja. Kuanzishwa kwa programu za mafunzo kwa wasimamizi wa viwanja kutasaidia kuhakikisha kuwa viwango vinazingatiwa kila wakati, siyo tu wakati wa ukaguzi.

Tano, matumizi ya teknolojia yanaweza kuwa sehemu ya suluhisho. Mfumo wa kidijitali wa kufuatilia hali ya viwanja unaweza kusaidia kutoa taarifa za mapema kuhusu matatizo yanayoweza kujitokeza, kama vile ubovu wa nyasi, mifumo ya maji au taa. Hii itarahisisha kuchukua hatua za haraka kabla hali haijawa mbaya zaidi.

Mwisho, ni muhimu kuwa na msimamo thabiti kutoka kwa mamlaka husika. Ikiwa uwanja umefungiwa kwa kushindwa kukidhi vigezo, basi ufunguzi wake uwe ni baada ya kuthibitishwa kwa maboresho ya kudumu, siyo ya muda mfupi.