Kupaa kwa bei ya mchele iwe fursa

Mpunga ni kati ya nafaka muhimu zinazotegemewa na watu wengi nchini, lakini kuanzia mwishoni mwa mwaka jana bei yake imekuwa ikipanda kwa kasi kubwa kiasi cha baadhi ya wananchi kushindwa kumudu kula wali kama walivyozoea.

Katika masoko ya jijini Dodoma kilo moja ya mchele mzuri iliyokuwa ikiuzwa Sh2,300 miaka miwili iliyopita sasa hivi inapatikana kwa kati ya Sh3,500 hadi Sh4,000, hali inayowafanya wengi kushindwa kuumudu, tofauti na miaka ya nyuma.

Mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa mahitaji kutokana na kufunguliwa kwa soko la mazao nje ya nchi kunatajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kupaisha bei ya chakula hiki pendwa kwa watoto wengi wa mjini.

Katika kukabiliana na kupanda kwa bei ya vyakula nchini, mwezi uliopita Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji alitoa vibali vya kuingiza tani 90,000 za mchele kutoka nje.

Dk Kijaji alisema mchele huo ambao haujulikani unaagizwa kutoka nchi gani, ulitarajiwa kuingia nchini kuanzia mwishoni mwa Februari ili kupunguza bei sokoni.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni miaka karibia 10 tangu Serikali ilipositisha uingizaji wa mchele kutoka nje ya nchi kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa mpunga nchini kuzidi mahitaji yaliyopo.

Mpaka Aprili 2014, Serikali ilitangaza zuio la mchele kutoka nje ya nchi kutokana na ongezeko la asilimia 14 katika uzalishaji wa mpunga nchini hivyo kuzidi mahitaji yaliyokuwapo kipindi hicho, hali ambayo bado inaendelea mpaka sasa.

Mavuno ya mpunga yalikuwa yameongezeka kwa miaka sita mfululizo kutoka tani 1,699,825 mwaka 2009/10 hadi tani 1,936,909 mwaka 2014/15 sawa na ongezeko la asilimia 14.

Kupanda kwa bei ya mchele katika siku za hivi karibuni ni dalili za wazi kuwa mahitaji ya zao hilo yameongezeka nchini hivyo tunapaswa kuwa na mikakati madhubuti.

Baada ya kuzuia vibali vya kuagiza bidhaa hii nje ya nchi na kufungua soko la mazao nje ya nchi, tulipaswa kujikita kuongeza uzalishaji. Chakula kimekuwa biashara kubwa hivi sasa, hivyo tukiwa na ziada ya kutosha ni fursa ya kuliingizia Taifa fedha za kigeni.

Hatua hii ingewezesha wakulima kupata kiasi kikubwa cha mazao na hivyo kuongeza kipato, sambamba na wananchi kutoumia kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo.

Kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa hiyo ni fursa kwa Tanzania iwapo itaangaliwa kwa mtazamo chanya wa kuongeza uzalishaji wa mazao yenye mahitaji makubwa nchini pamoja na majirani zetu kama inavyojionyesha kwenye mchele.

Fursa inaweza kuonekana yenye tija iwapo Taifa litajikita kuongeza uzalishaji kwa kiwango cha kujitosheleza kwa mahitaji ya ndani na kuuza nje ya nchi.

Hivyo, uamuzi wa kuruhusu vibali vya kuagiza mchele kutoka nje ya nchi ni mzuri, lakini bila shaka Tanzania itajikita katika kuongeza bajeti ya kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji.

Pasipo kuweka mikakati ya kuwawezesha wakulima kutumia teknolojia za kisasa na kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa sehemu kubwa ya nchi, itakuwa ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Fursa zitakuja na kuondoka bila kuwanufaisha Watanzania.

Taifa litakuwa na uhakika kwenye uzalishaji wa zao hili iwapo kutakuwa na mipango shirikishi itakayosaidia kuondokana na kujirudia kwa changamoto ya kuelemewa na mahitaji ya bidhaa tofauti.

Ili kuwa na uzalishaji mkubwa, ni muhimu Serikali ishirikiane na sekta binafsi kuweka mipango inayotekelezeka na wananchi waelezwe wajibu wao ili kila mmoja ajue anatakiwa kufanya nini.

Inawezekana kuweka jitihada katika uzalishaji wa mpunga kama ilivyofanyika kwenye sukari kwa kujielekeza katika kuepuka uagizaji kutoka nje ya nchi, mkakati ambao unakwenda vizuri kwa mujibu wa takwimu za Serikali.

Tunatarajia katika Bunge la bajeti ya mwaka 2023/24, kuona mpango thabiti wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula nchini mbali ya yale ya biashara ambayo tumezoea kusikia yakizungumziwa mara kwa mara.

Tanzania inacho kila inachokihitaji ili kuilisha dunia na vita vinavyoendelea nchini Ukraine ambavyo vimeathiri kwa kiasi kikubwa usambazaji wa chakula duniani, ni fursa inayohitaji mikakati ya haraka kufanikisha mpango huo.

Kilimo cha kimkakati cha mazao ya biashara ni fursa inayoweza kuubadili uchumi wa Tanzania ndani ya muda mfupi iwapo kutakuwa na usimamizi makini wa utekelezaji mipango itakayowekwa.