Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ukosefu wa mitalaa ndicho chanzo cha uhaba wa ajira

Muktasari:

Wenzetu wa Kenya wameanza kujiandaa kwanza kwa kupanua taaluma ya lugha ya Kiswahili na kuielekeza katika stadi mbalimbali ili wahitimu waweze kujiajiri badala ya kuajiriwa.

SUALA la ajira linajadiliwa kwa masikitiko makubwa miongoni mwa wanasiasa, wananchi wa kawaida na wanataalamu wengi hapa nchini wakidai kuwa vijana wanaomaliza elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu hawapati ajira.

Kwa mtazamo  wa watu wengi, lawama  zinaelekezwa kwa viongozi wa Serikali kwa kukosa uzalendo. Lawama zinaweza kuwa ni kutokuwa na mitalaa inayolenga kuwaandaa wanafunzi kujitegemea baada ya masomo yao. Vilevile SerikaIi  kutokuchangamkia fursa za ajira zinazojitokeza ndani na nje ya nchi.

Siku za nyuma, mitalaa iliandaliwa kuwawezesha wahitimu wa Shule za Kati (Middle Schools) kujiajiri baada ya masomo yao ya darasa la nane. Katika shule za (Middle School) wanafunzi  walijifunza kilimo cha kisasa, useremela, ufugaji na ushonaji. Kwa wale walioshindwa kuendelea na masomo yao waliweza kujitegemea kwa kufanya kazi na kujipatia kipato.

Wazo la kuwawezesha wanafunzi waliohitimu masomo yao katika ngazi ya sekondari nao walipatiwa mafunzo ya kuwafanya wajitegemee kimaisha. Kulikuwa na mitalaa ya Kilimo, Biashara na Ufundi kwa shule za sekondari zilizoteuliwa na wizara ili kuwaandaa wanafunzi katika fani hizo. Wako walioendelea na masomo yao ya  juu na kujiunga na Vyuo vya Ufundi Stadi (Veta) na hata vyuo vya ufundi kama Vyuo vya Ufundi Arusha, Dar es Salaam na Mbeya.

Matunda yao tumeyashuhudia katika shughuli za ujenzi wa barabara, nyumba za kuishi, katika ujenzi wa   mabwawa ya kuhifadhia maji, shule na kilimo na uvuvi. Mafundi hawa stadi walichangia sana katika ujenzi wa nchi wakisaidiana na wahandisi.

Juhudi zote hizi zilizoelekezwa katika kuwapatia ajira vijana wetu zilisitishwa baada ya kiongozi wa kisiasa katika Wizara ya Elimu kuamua kufuta mihutasari ya masomo hayo katika shule za sekondari.

Matokeo yake ni kuwa maendeleo katika fani za ujenzi,biashara na kilimo  yanaonekana dhahiri hivi sasa.

Katika  kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya kisiasa hapa nchini, Watanzania tunatakiwa tubadilike kifikra, kimtazamo na kimwelekeo. Inasikitisha kuona kuwa Watanzania wengi hata wale waliosoma hadi  vyuo vikuu hawabadiliki kwa kujiendeleza zaidi.

Wanaendelea kutekeleza mipango yao ya kazi kulingana na nadharia walizosomeshwa miaka ya nyuma bila kujali kuwa kila siku kunatokea mabadiliko kwa mujibu wa mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Kwa kusoma katika vyombo vya habari tukitumia intaneti tunaona kuwa kila kukicha kuna uvumbuzi mpya ambao hatuna budi kujielimisha kwa kusoma majarida na machapisho.

Tusipofanya hivyo tutashindwa kwenda na wakati hasa katika kipindi hiki cha utandawazi ambapo soko la ajira la Afrika Mashariki litakuwa wazi na vijana wa Kitanzania watashindanishwa na wenzao wa Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Wenzetu wa Kenya wameanza kujiandaa kwanza kwa kupanua taaluma ya lugha ya Kiswahili na kuielekeza katika stadi mbalimbali ili wahitimu waweze kujiajiri badala ya kuajiriwa.
Nasi hatuna budi kuwaandaa vijana wetu ili wawe na ujuzi wa lugha hii siyo kinadharia tu bali kuwawezesha kupata ajira.

Mwaka 1988 Tanzania ilitakiwa kuwaandaa wataalamu wa Kitanzania wenye ujuzi wa Kifaransa na Kiswahili ili wapelekwe  Ufaransa kwa kipindi cha mwaka mmoja kusomea kozi ya ukalimali na baadaye kuajiriwa na Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU). Walipatikana Watanzania wanne waliopelekwa Ufaransa. Hatua hii ilitokana na uamuzi wa kikao cha Mawaziri wa Utamaduni wa OAU kilichofanyika Mauritius.

Iliamuliwa kuwa lugha ya Kiswahili iwe ni miongoni mwa lugha rasmi ya kazi katika vikao vya OAU. Lugha nyingine zilizoteuliwa ni Kifaransa, Kiingereza, Kireno na Kiarabu. Kiswahili kilipendekezwa na kuteuliwa kwa sababu ni lugha inayovuka mipaka ya makabila na nchi tofauti na Kiigbo, Kihausa, Kiwolof na Kiyoruba ambazo ni za makabila maalumu.

Pia Kiswahili kinazungumzwa na watu wengi katika Bara la Afrika na kwingineko duniani.
Baada ya wataalamu hawa kumaliza kozi yao walirejea nchini tayari kukabiliana na majukumu yao mapya. Waliripoti katika Wizara  ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kuambiwa kuwa warudi katika sehemu zao za kazi na baadaye wangeelekezwa hatua za kufuata. Kwa bahati mbaya walisubiri kwa kitambo kirefu bila kupata ajira mpya.    

Jambo hili liliwafanya wajitafutie ajira nje ya nchi katika mashirika ya kimataifa.
Katika miaka ya 1996 ilitokea fursa nyingine kwa Watanzania kwenda kufundisha Kiswahili katika nchi za Maziwa Makuu. Nchi zilizoleta maombi zilikuwa ni Jamhuri  ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda na Burundi.  

Nchi za DRC na Rwanda  ziliomba walimu wa kufundisha Kiswahili katika shule za sekondari ambapo Burundi walitaka walimu wa kufundisha Kiswahili katika shule za msingi. Katika maombi hayo yaliyoletwa Tanzania kupitia katika Wizara ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa yalielekezwa kwa  Wizara ya Elimu, Habari na Michezo (wakati huo) ili yashughulikiwe ipasavyo.
Maombi haya yaliishia kapuni. Hii ni aibu pia ni ukatili usio kifani kwa kuwanyima Watanzania kupata fursa za ajira bila sababu za kimsingi.

Wananchi hawajafahamishwa  ni hatua zipi zimeanza  kuchukuliwa katika kufuatilia maombi haya.  Tumefahamishwa kuwa maombi haya yalitolewa kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa mkutano wa Wakuu za Nchi za Afrika nchini Gabon.
Inawezekana hatukuwa tumejiandaa kwa maombi haya. Kwa ufahamisho ni kwamba yafuatayo yangeandaliwa kukabiliana na hali hii.

Kwanza ni kuwapata walimu ambao wanafahamu lugha mbili yaani Kifaransa na Kiswahili. Lugha ya Kifaransa ni muhimu kwa sababu wananchi wa Gabon wanazungumza Kifaransa kama lugha yao rasmi. Tunao walimu wa taaluma hizi mbili pamoja na kwamba hawatoshi katika shule zetu za sekondari.

Pili, kutokana na upungufu wa walimu wa Kifaransa katika shule za sekondari hapa nchini,  kungekuweko na mikakati mahususi ya kuwaandaa walimu wapya wa masomo hayo.

Tunao wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na wamesomea somo la Kifaransa na wangeweza kuchaguliwa kujiunga na mafunzo ya ualimu. Wanafunzi hawa wapatikane na kuandaliwa ili wazibe mapengo yaliyotokana na walimu watakaopelekwa Gabon. Wananchi tufahamishwe ni nini kinaendelea.
0754  861664   0716  694240