Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Magari haya ya kifahari serikalini yanaifilisi nchi

Kati ya vitu vinavyoumiza kichwa changu ni pale linapokuja suala la matumizi ya Serikali.

Nashangaa mno, Serikali masikini inayokwama kwenye mambo mengi ya kimaendeleo, inaposhitadi kutenga mabilioni ya fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ya kifahari kwa maofisa wake.

Sio kama napingana moja kwa moja na matumizi ya magari hayo hasa kwa baadhi ya maofisa, mantiki ya andiko langu imejikita katika aina ya magari yanayonunuliwa, watendaji wanaopaswa kuwa na magari hayo na wapi wanayatumia.

Hii ina maana kwamba, wapo baadhi ya maofisa kutokana na shughuli zao wanapaswa kuwa na aina fulani ya magari, ingawa siungi mkono yale ya kifahari yanayoiingiza nchi kwenye gharama.

Hivi kuna sababu gani ya kila mwaka Serikali kununua magari ya thamani kubwa kuanzia Serikali Kuu hadi serikali za mitaa kwa maana ya halmashauri zote nchini?

Nimewahi kusikia Sh500 bilioni zimetengwa kwa ajili ya magari ya kifahari kwa matumizi ya maofisa, hivi tuko makini kweli kama Taifa ambalo kimsingi halijajitosheleza katika mambo mengi tu ya kimsingi?

Leo Taifa zaidi ya nusu karne ya kuwa huru na kuanza kujitegemea, hatujaweza kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa kila Mtanzania; hatujaweza kufikisha huduma za msingi za afya kila kijiji; mtandao wa barabara bora bado kizungumkuti. Halafu tunatenga mabilioni kununua magari ya kifahari.

Kuna gari thamani yake ni sawa na mradi mmoja wa maji au afya kwa ngazi ya kijiji au hata kata, lakini sisi Watanzania pesa hiyo tunaitupa kwenye mashangingi ya wateule wetu!

Kuna wakurugenzi wa halmashauri na mameya wa miji ambao safari zao kwa kiasi kikubwa ni mjini, sioni kama kuna ulazima kwao kutumia magari ya kifahari kama vile VX na V8. Haya ni matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi.

Nafahamu wapo wanaosema umuhimu wa magari hayo kwa maofisa wa Serikali ni urahisi wa kuwafikisha kwenye maeneo magumu ambayo wananchi wanahitaji huduma. Hata hivyo, wenye mitazamo hiyo, wanapaswa kufahamu kuwa, kwa kadri gari linavyouzwa kwa gharama kubwa, ndivyo gharama za kulihudumia huwa juu.

Kwa maneno mengine, ninapoonyesha upinzani dhidi ya aina hii ya magari, ninalenga kuona Serikali ikipunguza gharama zisizo za msingi na fedha hizo zielekezwe kwenye miradi ya huduma kwa wananchi.

Mafuta, vipuri na matengenezo ni baadhi ya maeneo yanayogharimu fedha nyingi tunapotumia aina hii ya magaria ambayo hivi leo kila mtendaji anataka awe nalo.

Hivi huwezi kuwa bosi ukabaki na hadhi ya ubosi serikalini kwa kutumia magari ya bei chini ya Sh100 milioni?

Tunachopaswa kujua ni kwamba fedha hizi tunazozitapanya kwenye magari haya ya kifahari, zingeweza kununua magari ya kuchimbia visima virefu, matrekta, kuchimba malambo ya maji kwenye maeneo kame.

Zingeweza kutumika kwenye miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji na maeneo mengine ambayo kwanza yangeongeza uzalishaji na kutoa ajira kwa wananchi.

Kwa maoni yangu, badala ya kufikiria kutumia maburungutu ya fedha kununua magari ya kifahari, tungewaza mbinu za kuwapunguzia Watanzania mzigo wa gharama za maisha.

Kinachoshangaza zaidi ni pale tunapoona hata wale wanaotengeneza magari hayo, maofisa wa Serikali zao wamechagua magari mbadala ambayo aghalabu hupatikana kwa gharama ndogo.

Mbali na kushangaa, naumia ninapoona mara nyingi magari haya yakiharibika kitu kidogo tu, yanaishia kuachwa karakana, kisha inaombwa fedha nyingine ya kununua jipya.

Ukifuatilia kwa makini, utabaini idadi kubwa ya magari haya yanapopata ubovu kidogo yanaishia kuachwa karakana kisha baadaye yanauzwa chini ya asilimia 10 ya gharama yake halisi.

Natamani kuona mawaziri na wabunge wanafikiria maisha ya watu wa chini, badala kwenda kijijini na gari la Sh300 milioni, bora uende na fedha zitakazobadilisha maisha yao.

Nakumbuka iliwahi kuelezwa kwamba viongozi wa Serikali wakopeshwe magari hayo, naliunga mkono hili kwa sababu watayatunza na itapunguza gharama ya uagizaji kila mwaka.

Pia, upo uwezekano wa kuingia ushirikiano na watengenezaji wa magari kuwaomba watutengenezee magari ya bei nafuu, lakini yenye uwezo wa kutumika katika njia zote.

Kwa mwenendo huu wa magari ya Sh300 milioni, maana yake viongozi watano wanagharinu Sh1.5 bilioni. Fikiria Tanzania tuna viongozi wangapi wanaotaka kutumia magari hayo? Tunapaswa kujirekebisha, utaratibu huu unatugharimu.