MAKENGEZA: Tabaka la vibaka na mapambio ya wapambaji

Tabaka la vibaka na mapambio ya wapambaji

Muktasari:

  • Eeenzi za … ni watu wazima tu sasa ambao wanakumbuka eeenzi hizo za uhai wake na ni wazima zaidi wanaokumbuka eeeenzi za uongozi wake na ni wahenga tu wanaokumbuka eeenzi za matamko mengine. Na kila mtu anamkumbuka kwa namna tofauti.

Eeenzi za … ni watu wazima tu sasa ambao wanakumbuka eeenzi hizo za uhai wake na ni wazima zaidi wanaokumbuka eeeenzi za uongozi wake na ni wahenga tu wanaokumbuka eeenzi za matamko mengine. Na kila mtu anamkumbuka kwa namna tofauti.

Miye? Kama mhenga ninakumbuka mengi sana. Yameniangaza na kuniongoza maishani mwangu hata wengine wanapojaribu kunichonga niwe chongo wa kuchungulia kwingine. Basi leo napenda kukumbuka suala moja tu maana tungefuata mfano wake katika hilo, nadhani tusingepata matatizo ambayo tumeyapitia.

Wajua neno ‘ndugu’ lilipoanza kutumika? Wengine wakadai oooh anatuletea ukomunisti, oooh ni tafsiri ya komredi n.k. Lakini mimi nilielewa tofauti. Wakati ule, wapambe walikuwa wameshanza kumwita mtukufu, mtu wa Mungu, na sifa nyingi nyinginezo.

Walitegemea kumpaisha juu kichwa kipotee kwenye mawingu asiweze kuona matendo yao huko chini. Walitegemea kumvimbisha kichwa ashindwe kupitia mlango wa Ikulu na kutoka nje kuwaona na ulafi wao.

Naam, kwenye hilo wakakubaliana kabisa kupandana mmoja juu ya mwingine ili wamwinue zaidi na zaidi. Si ndiyo … juu … juu … juu zaidi. Na wao pia, walipenda kujipandisha wenyewe, si watu, si waishiwa tena kama sisi, bali ni waheshimiwa, kana kwamba wote hawastahili heshima, na katika kustahili heshima wapewe fahari zote za heshima pia.

Kumbe hawakujua. Ghafla mwenyewe akapunga kifimbo chake na kutamka kwamba hakuna mwishiwa na mheshimiwa, utakatifu ni kutaka vitu tu. Tuheshimiane kama ndugu. Sote tuitwe ndugu.

Dah! Waheshimiwa wakaanguka. Wakalaani kimoyomoyo. Lakini wakajikokota na kujipangusapangusa ili kuondoa vumbi na kuanza tena.

Ndugu mtukufu, sisi ndugu waheshimiwa …

Safari hii, fimbo ikawadondokea kichwani.

Ndugu ni ndugu. Hakuna cha mheshimiwa wala cha mwishiwa.

Dah! Watu wakabwagwa chini tena. Wale wawakilishi wa wananchi, ndugu, wenye kisomo, ndugu, mabalozi, wahandisi, mawaziri, sote ndugu. Iliwauma lakini wafanye nini. Siri yao ilifichuka. Ikabidi waitane ndugu huku wanapata vidonda vya tumbo kwa kulazimika kumezea.

Lakini hawakukata tamaa. Baada ya kushinda vita dhidi ya Idi Amni, wakaona nafasi nyingine ya kujimwayamwaya tena.

“Tumepata ushindi kwa sababu za busara za Amiri Jeshi Mkuu.”

Wakaanza kumsakama na kumsukuma hadi mawinguni tena afunikwe kwenye mawingu lakini hawakufua dafu. Fimbo ikacheza, fimbo ikacharaza.

“Kwani mimi nilienda vitani? Tuwasifie wapiganaji wetu. Hao ndio mashujaa wetu.”

Akazunguka nchi nzima kuwaandaa wananchi kuwapokea mashujaa. Na tuliwapokea kweli, tukawashangilia walioweka rehani maisha yao kwa faida ya nchi yetu. Lakini sijui fimbo yake ilikuwa imeanza kufifia kidogokidogo.

Angalau wenye kusifia waliweza kurudisha kusifiwa. Waheshimiwa wakatangaza rasmi kutengana na waishiwa (isipokuwa wakati wa kutafuta kura. Hapo wanapiga magoti, ili watupige makofi baadaye).

Unaweza kuona haya ni mambo madogo, jina si jina tu, lakini matokeo yake tunayaona. Ukishakuwa mheshimiwa unadai kila kitu cha kiheshimiwa, magari ya kiheshimiwa, posho ya kiheshimiwa, marupurupu ya kiheshimiwa, mafao ya kiheshimiwa na sasa hata nyumba za kiheshimiwa. Madai hayaishi.

Kudadakei, hata matusi ya kiheshimiwa maana mheshimiwa akikutukana kudadadeki uvundo hufunikwa na marashi ya uheshimiwa.

Wakajaribu nyingine kidogo … eti zidumu fikra sahihi za mwenyekiti lakini hapa tulicheka na kuanza kujaribu kupembua zipi sahihi zipi si sahihi. Na wakati huo, fimbo ikacheza tofauti pia. Watu walikuwa wameanza kuchoka wakamwita mwenyewe Musa, maana Musa aliwatoa Waisraeli utumwani lakini hakuwafikisha kwenye nchi ya ahadi.

Wapambe waheshimiwa wakakasirika, bila shaka wangeanza kukamata na kutia ndani, lakini mwenyewe aliwakata kilimilimi chao na hamu ya kutumia mabavu ya kipumbavu kwenye hotuba yake.

“Nasikia waniita Musa …”

Akacheka, stori ikaisha.

Mwisho, alipotangaza kustaafu, walianza tena. Kwa kauli yake mwenyewe:

“Kila nilipotaka kung’atuka madarakani walikuwa wakiniambia “Mwalimu, endelea tu, hii nchi ni changa na umeitoa mbali, nchi hii haitaendelea bila wewe. Nami niliendelea hadi pale nilipokuja kugundua kumbe nchi changa waliyokuwa wanaiongelea ni familia zao na hazitaendelea bila mimi kuwepo madarakani.”

Kwa kuwa alikataa kupandishwa mawinguni, aliwaona na ufedhuli wa mioyo yao na kukataa.

Kwa nini naandika yote hayo. Si kwa Mwalimu tu. Mdhalimu hawezi kudumu peke yake. Anafanikiwa kuendelea kushika madaraka kwa sababu daima wapo wapambe wa kumwimbia mapambio, tabaka la vibaka linalofaidika kuwepo kwake. Basi kiongozi anakuta kichwa kiko mawingu, hasikii wala haoni kilio cha walio chini huku wapambe wanawakanyaga walio chini ili waweze kumwinua zaidi mdhalimu na kujiinua pia kwa jina lake. Naam. Tusisahau kwamba ndumilakuwili wana vichwa viwili, kimoja cha kuimbia mapambio na kingine cha kufakamia chakula chochote kinachopatikana, halali na haramu, pamoja na kuwagonga wote wanaothubutu kujaribu kupenyeza ukweli katikati ya mapambio.

Lakini wamesahau kitu kimoja. Nyoka ni nyoka tu na iko siku watu wataacha kuogopa kugongwagongwa na nyoka na kuungana kuwatoa. Hawatatishwa tena na vichwa vyake viwili. Au ikitokea kwamba yule ambaye walipenda kukaa kwenye kivuli chake baada ya kumpandisha juu anatoweka na wanabaki wakipepesa macho kwenye jua kali.

Hapo watajaribu kupambia huyu mwingine, labda kwa kutumia vichwa vyote viwili, lakini nyoka ni nyoka na hawawezi tena kudanganya kwamba ni kobe au panya buku. Hawafunikwi na kivuli tena. Katika undumilikuwili wao wameharibu sifa zao, na waishiwa daima hawatasahau.

Hata wakibadilika namna gani na kujivisha ngozi za kumeremeta, ili wakumbukwe kwa uzuri, wameshanyea kambi na mnuko haufunikwi na marashi ya uheshimiwa. Washukuru kama hawakamatwi kutokana na vitendo vyao viovu vya kivulini.

Imeandikwa na Richard Mabala