MAONI: Biashara ya sukari inahitaji sera na mfumo imara

Siasa za sukari zimerejea tena majukwaani. Jana tumeripoti taarifa ya baadhi ya wazalishaji wa sukari nchini wakisema pamoja na kuwa na vibali vya kuagiza sukari nje, hawajabweteka na bado wana uwezo wa kuzalisha sukari ya kutosha.

Wazalishaji hao walitoa tamko hilo kufuatia kauli ya Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga aliyewashukia akisema wamekuwa wakibweteka kuzalisha kwa wingi bidhaa hiyo muhimu kwa kuwa wana vibali vya kuiagiza kutoka nje.

Akizungumza na wadau wa sekta binafsi na wa kilimo majuzi, Hasunga alisema Serikali imeamua kusitisha vibali hivyo na badala yake itatumia kampuni nyingine, lengo likiwa ni kuwataka wazalishaji hao wa ndani kuongeza nguvu katika uzalishaji.

Ni kweli kama tutashitadi kuagiza sukari kutoka nje, tutakuwa tunapunguza uzalishaji wa ndani na hivyo kufifisha ndoto za kuwa nchi yenye uchumi imara wa viwanda. Hapa tunalazimika kuungana na waziri kwa mtazamo huo.

Katu vibali vya kuagiza sukari visiwe ndio mbadala wa shughuli za viwanda vyetu na kama alivyosema Hasunga, lazima viwanda vifanye kila juhudi za kukuza uzalishaji ikiwamo kulima miwa ya kutosha kwa ajili ya malighafi.

Hata hivyo, inawezekana kile anachokiita waziri Hasunga kuwa ni kubweteka kwa wazalishaji wa ndani kinatokana na Serikali yenyewe kwa kuwa ndio iliyotoa tamko ya kuwaruhusu waendelee kuagiza sukari.

Mwaka 2017, Serikali iliwapa baraka wazalishaji wa ndani kuagiza sukari kutoka nje, huku wakiendelea na jitihada za kuimarisha uzalishaji wa ndani.

Tunaamini matamko kama haya ndiyo kiini cha mgogoro wa sukari ambao mara kwa mara umekuwa ukiibuka. Vita hii ya maneno kati ya waziri na wazalishaji inaashiria kuwapo kwa tatizo ambalo tulifikiri lilishafanyiwa kazi na Serikali tangu kipindi kile cha mgogoro mkubwa wa sukari.

Tunaamini bado hakuna mfumo imara wa kusimamia uzalishaji na biashara ya sukari kwa jumla, ndio maana suala lake limekuwa likiibuka karibu kila mwaka kwa sura tofauti. Kilichopo ni matamko ya majukwaani ambayo kwa hakika hayatomaliza matatizo yanayoikabili biashara ya sukari nchini.Hata huo uzalishaji wa kutosheleza anaoutaka Waziri Hasunga, hauwezi kuwapo kwa kutamka tu mkutanoni.

Tunahitaji kuwa na sera maalumu na mfumo imara wa kusimamia na kuendeleza sekta ndogo ya sukari. Vitu hivi ndivyo vitakavyotusaidia ikiwa kweli tuna dhamira ya kuimarisha uzalishaji wa ndani.

Ni sera hiyohiyo ambayo pia itaainisha haja na utaratibu mzima wa kuagiza sukari kutoka nje.

Kwa mfano, tungependa kuona uagizaji wa sukari kutoka nje ukifanywa kwa malengo na kwa kipindi mahususi, ili kuepuka uingizaji holela na pia kuvibana viwanda vinavyozembea kuzalisha sukari kwa kutegemea kuagiza kutoka nje.

Wito wetu ni kuona Serikali ya Awamu ya Tano ikiweka mazingira mazuri ya kisera na kimfumo kuhakikisha tunajitosheleza katika uzalishaji wa bidhaa hii nyeti. Tena ikibidi tuzidishe uzalishaji kwa ajili ya kuuza nchi za nje.