MAONI: Changamoto hizi zisitumike kuvuruga Ligi Kuu Bara

Muktasari:

  • Katika mchezo huo Simba ilitwaa Ngao ya Jamii kwa ushindi wa mabao 2-1 ikiwa ni mara ya pili mfululizo. Msimu uliopita ilitwaa ubingwa kwa kuilaza Yanga kwa penalti 5-4 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ukizikutanisha timu bingwa ya msimu uliopita Simba na bingwa wa Kombe la FA, Mtibwa Sugar ya Morogoro ni ishara ya kuanza Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika mchezo huo Simba ilitwaa Ngao ya Jamii kwa ushindi wa mabao 2-1 ikiwa ni mara ya pili mfululizo. Msimu uliopita ilitwaa ubingwa kwa kuilaza Yanga kwa penalti 5-4 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kama inavyofahamika, Ligi Kuu msimu huu itakuwa na timu 20 badala ya 16 ambazo zimekuwa zikishiriki kwa muda mrefu.

Timu zilizopanda Ligi Kuu msimu huu ni Biashara Mara, African Lyon na KMC (Dar es Salaam), JKT Tanzania, Costal Union ya Tanga na Alliance ya Mwanza.

Tunazikaribisha timu hizi kwenye ligi hii licha ya kuwa Coastal Union na African Lyon ni wageni wenyeji kwani zilikuwepo kwenye ligi hiyo kabla ya kushuka katika vipindi tofauti.

Msimu huu wa Ligi Kuu ni tofauti na mingine kutokana na mambo kadhaa yaliyojitokeza.

Wingi wa timu unatarajiwa kuongeza ushindani kwani sasa zitalazimika kucheza mechi nyingi zaidi (38) tofauti na ilivyokuwa awali.

Mechi nyingi pia zitatengeneza ushindani ndani ya timu zenyewe kwa wachezaji kwani ili kupata nafasi, watakuwa hawana budi kujituma kikamilifu. lakini kwa timu zenyewe, zitakuwa na fursa ya kuwatumia wachezaji wengi ziliowasajili hasa ikizingatiwa kwamba kutokana na wingi wa mechi, baadhi wanapata majeraha na changamoto nyingine.

Wakati timu zikiongezeka hivyo gharama za uendeshaji kuongezeka pia, ligi hiyo inaanza huku ikikabiliwa na changamoto kubwa ya udhamini. Baadhi ya timu zitashindwa kufikia malengo ya maandalizi kutokana na uhaba wa fedha ambazo awali zimekuwa zikitolewa na wadhamini wakuu kwani nyingi hazina wadhamini binafsi.

Kutokana na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji huku ligi ikiwa haina mdhamini, maana yake ni kwamba zitakuwa na mzigo mkubwa ikilinganishwa na msimu uliopita. Zitalazimika kusafiri zaidi kutoka eneo moja kwenda lingine hivyo kuingia gharama nyingi zaidi za usafiri na posho.

Katika hilo, inawezekana baadhi ya timu zikawa na mtihani mkubwa kushiriki vyema na kwa viwango vya ushindani sawa.

Kwa mfano, Lipuli ya Iringa imesema ina wasiwasi kuwa mambo yanaweza kuwa magumu zaidi kwa kuwa timu hiyo haina mdhamini wa kuipa hata maji ya kunywa.

Kwa muktadha huu, tunatoa angalizo kwa wasimamizi wa ligi hiyo kuwa makini ili kuhakikisha kuwa nguvu ya fedha kwa baadhi ya timu ambazo ni chache haitumiki vibaya hivyo kuondoa ladha ya ushindani na mshindi kupatikana uwanjani.

Angalizo lingine kwa waandaaji ni kujitahidi kadri iwezekanavyo kuhakikisha kwamba ratiba haipanguliwi ovyo. Tunasema hivyo tukiwa tumeshaona dalili kwani imeshapanguliwa hata kabla haijaanza.

Aidha, tunawasihi waamuzi wachezeshe kwa haki bila ushawishi wa namna yoyote ile. Kiongozi wao awe sheria 17 ili kupata bingwa anayestahili.

Changamoto ni nyingi, lakini isiwe kigezo cha kuvuruga ligi, matarajio yetu ni kuiona ikifanikiwa.