MAONI YA MHARIRI : Matukio ya wizi wa watoto yakomeshwe
Muktasari:
- Tukio hilo la kusikitisha lilitokea eneo la Mbezi Mwisho Wilaya ya Ubungo na baada ya saa 48 mtoto huyo alipatikana eneo la Kivule Wilaya ya Ilala.
Jumapili iliyopita jijini Dar es Salaam kumetokea tukio la kuibwa mtoto mwenye umri wa miaka mitatu, Beauty Yohana Isango alipokwenda kanisani akiwa na mama yake mzazi.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea eneo la Mbezi Mwisho Wilaya ya Ubungo na baada ya saa 48 mtoto huyo alipatikana eneo la Kivule Wilaya ya Ilala.
Mazingira ya kupotea mtoto na namna alivyopatikana ikiwamo maelezo ya mtuhumiwa kuna haja Jeshi la Polisi likawa na kitengo maalumu kwa ajili ya kushughulikia matukio ya wizi wa watoto.
Tunasema hivyo kwa sababu Mei 2014 gazeti hili liliwahi kuandika habari ya kiuchunguzi kuhusu tatizo la wizi wa watoto ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee ilibainika zaidi ya watoto 61 waliibwa katika kipindi cha mwaka 2012 na 2013.
Pia, taarifa ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilitoa taarifa kwamba mwaka 2012 kulikuwa na kesi za wizi wa watoto 20, hadi mwaka unamalizika watoto saba pekee ndio walipatikana.
Taarifa hiyo iliendelea kubainisha kuwa mwaka 2013 mkoani Dar es Salaam kulikuwa na kesi 31 za wizi wa watoto na hadi Desemba mwaka huo ni watoto 21 ndio walipatikana, kwa maana hiyo watoto 10 hawakujulikana waliko.
Mwananchi lilikwenda mbali kwa kupata takwimu za upoteaji wa watoto kwa mikoa mingine ambapo mkoani Dodoma kati ya Januari 2013 hadi Aprili 2014 kulikuwa na matukio ya kupotea watoto 24 na Mkoa wa Tanga kati ya mwaka 2012 na Aprili 2014 jumla ya matukio ya kupotea watoto yalikuwa 63.
Watoto wanahitaji ulinzi wa kila mtu lakini Jeshi la Polisi lina umuhimu wa pekee katika kushughulikia matukio ya wizi wa watoto, haya si masuala ya kushughulikia kwa uzito mwepesi.
Ni muhimu kwa Jeshi la Polisi kuanzisha kitengo cha kupambana na matukio ya wizi wa watoto, tunaamini hilo linawezekana na litapunguza kwa kiasi kikubwa uhalifu huu.
Kisa cha mtoto kuibwa Mbezi Mwisho na baadaye kupigwa simu kwamba ameonekana Kivule, inaonyesha umuhimu wa kuhusishwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika kukabiliana na uhalifu huu.
Lakini, hili litawezekana kama Jeshi la Polisi litaamua kuwa na kitengo maalumu cha kupambana na uhalifu wa wizi wa watoto, iwe hospitali, nyumbani, shule na kwenye nyumba za ibada.
Ule usemi wa Mama Salma Kikwete (mke wa Rais wa Awamu ya Nne) wa kuwatetea watoto wa kike kwamba ‘mtoto wa mwenzio ni mtoto wako’ unapaswa kuwa mtambuka na kuhusisha matukio ya wizi wa watoto wote.
Wanaharakati, Jeshi la Polisi na wananchi wote tunapaswa kusema imetosha, tusiwavumilie wanaotaka kuifikisha nchi kwenye hofu ya wizi wa watoto.
Haiwezekani watu watafute visingizio vya kuiba watoto kwa kuhusisha imani za kishirikina au migogoro kwa wazazi. Watanzania tukatae uzushi huu na Jeshi la Polisi lisaidie kuwatia mbaroni wanaotumia visingizio hivyo kuiba watoto.
Tunaamini tukio la mtoto Beauty litakuwa la mwisho kwa maana Jeshi la Polisi litakuja na mikakati mipya ya kupambana na uhalifu huo.