Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpango wa chakula shuleni ufanyiwe kazi

Gazeti la jana lilikuwa na taarifa kuhusu agizo la Serikali kwa wakuu wa mikoa na wilaya, kuhakikisha wanafunzi wote wa shule za kutwa za umma na binafsi wanapata chakula bila kujali madarasa yao.

Agizo hilo linapaswa kuzingatiwa na kufanyiwa kazi, kwani linaashiria hatua muhimu katika kutambua mchango wa lishe bora kwa maendeleo ya kielimu na afya ya watoto wetu.

Hata hivyo, utekelezaji wa agizo hili unahitaji uangalizi wa kina na ushirikiano madhubuti kati ya Serikali, wazazi, na wadau wengine wa maendeleo.

Wadau wa elimu wameshauri Serikali kuanza kutenga fedha kama ruzuku kwa shule zote nchini, ili kufanikisha azma ya kuhakikisha kila mwanafunzi wa shule za kutwa anapata chakula cha mchana. Pendekezo hili ni zuri, kwani utoaji wa chakula shuleni utakuwa kichocheo kikubwa cha kuongeza ari ya kusoma na pia kupunguza utoro miongoni mwa wanafunzi.

Inafahamika kuwa watoto wanashindwa kuzingatia masomo wakiwa na njaa, jambo ambalo linaathiri ufaulu wao pamoja na maendeleo ya kitaaluma kwa ujumla.

Kutoa chakula kwa wanafunzi wa shule za kutwa si tu kutaboresha afya zao, bali pia kutasaidia katika kukuza usawa wa fursa za kielimu kwa watoto kutoka familia zote, bila kujali kipato cha wazazi wao.

Kutoa chakula shuleni si suala la anasa, bali ni hitaji la msingi, hivyo wakati baadhi ya shule za bweni zinapata ruzuku kwa ajili ya chakula, shule za kutwa nazo zifikiriwe katika jambo hilo, ili wanafunzi katika shule hizo nao wanufaike.

Utoaji wa chakula kwa wanafunzi uzingatie mlo kamili ili kuboresha afya zao kama inavyoshauriwa na wataalamu wetu wa lishe, badala ya kupatiwa vyakula vya kujaza tu matumbo.

Pia wazabuni wa kupeleka chakula shuleni, wahimizwe na kufuatiliwa kwa kuhakikisha wanapeleka vyakula vyenye virutubisho ambavyo vitakuwa na tija kwa wanafunzi. Jambo hilo linapaswa kwenda sambamba na malipo yao kulipwa kwa wakati, ili huduma hiyo iwe endelevu shuleni.

Hivyo, ili kufanikisha mpango huu, ni muhimu Serikali kushirikiana kwa karibu na wazazi na jamii kwa ujumla.

Tunaamini ikiwekwa mipango madhubuti ya usimamizi na ufuatiliaji, jambo hili litakuwa jepesi kufanyika na hata fedha zinazotengwa zitatumika ipasavyo na zinawanufaisha watoto.

Pia jamii inatakiwa kuelewa kuwa jukumu la kutoa chakula shuleni si la Serikali pekee, hivyo wazazi wanapaswa kushiriki katika kuchangia mpango huo kwa njia mbalimbali.

Changamoto kubwa katika utekelezaji wa mpango huu inajitokeza pale ambapo jamii inatafsiri vibaya sera ya elimu bila malipo, ikiamini kuwa Serikali inapaswa kugharamia kila kitu, ikiwemo chakula.

Hali hii inaweza kudhoofisha jitihada za kuboresha lishe shuleni na hatimaye kuathiri maendeleo ya wanafunzi. Ni muhimu kwa Serikali na wadau wengine kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kushirikiana katika masuala ya elimu, hususan katika suala la utoaji wa chakula shuleni.

Tunapongeza jambo hili kwa kuwa ni hatua muhimu katika kuelekea kuboresha elimu na afya ya watoto wetu, lakini mafanikio ya mpango huu yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wazazi, na wadau wengine.