Mstaafu anapopaswa kuondoka bila shukurani baada ya kutenda wema

Ni maneno ya busara yaliyotoka kwa wazee wetu wa kale kwamba ‘tenda wema uende zako usingoje shukurani’.
Mstaafu wetu anaishia kusikitika tu sana kwamba pamoja na maneno haya kuwa na ukweli wake, lakini yanamuumiza zaidi yeye na wastaafu wenzake anapoona nchi yao hii waliyoitendea wema na kuijenga kwa jasho na damu yao ikikosa shukurani na kuwataka wachape lapa kwenda zao, ikiwezekana Burundi!
Inaumiza sana kama siyo kusikitisha kwamba mstaafu huyu mwalimu, daktari, mkunga, fundi bomba, mwanajeshi aliyepata kilema cha maisha huko Kagera akilipigania Taifa lake na huko Msumbiji hata Zimbabwe akiyapigania mataifa ya Afrika ili yapate uhuru wake, leo wanaishia kupata pensheni ya shilingi laki moja tu kwa mwezi kama shukurani yao kwa kulijenga Taifa hili.
Tukumbuke tu kuwa hii ni hela waliyochanga wenyewe kwa kukatwa kwenye mishahara yao na waajiri wao kuwaongeza chochote ili waweke akiba yao ya uzeeni.
Hakuna hela ya Siri-kali wala ya chama cha wafanyakazi wala hela kutoka kibubu cha akiba ya wafanyakazi.
Inamshangaza sana mstaafu kwamba kibubu chake kimekuwa kama kampuni ya ujenzi, huku kikiwa kijiwe cha ajira!
Wengi wao waliokuwa wakipokea mshahara wa kima cha chini, kama siyo kima cha chizi, walijikuta wakipokea pensheni ya shilingi alfu hamsini na wengine chini ya hizo, kwa mwezi.
Ndipo yule muungwana mwema wa Msoga bila ahadi ya kuwa ana ‘jambo lake na wastaafu’, akaamka tu asubuhi moja ya miaka 20 iliyopita na kupandisha pensheni kwa shilingi alfu hamsini nzima na pensheni kuwa shilingi laki moja na senti senti! asante zake.
Laiti na wengine wangefanya hivyo, mstaafu sasa angekuwa anapokea hata laki tano kwa mwezi.
Lakini hilo lilikuwa miaka 20 iliyopita na maisha hayajaanza kuwabana na kuwakaba wabongo na hata vijana wetu hawajaibatiza shilingi laki moja yetu ya madafu kuwa ‘Laki si Pesa’.
Wastaafu na pensheni yetu ya ‘Laki si Pesa’ tukaanza kukiona cha moto. Yule mwana muungwana wa Chalinze akawa ameishastaafu na waliofuata wote hawakukumbuka kuwa nchi hii kuna walioitendea wema na wanastahili shukurani kama alivyofanya yule muungwana wa Msoga.
Hakuna anayekumbuka wema aliotenda mstaafu wa kuijenga nchi hii. Wote wanaomba kimoyo-moyo mstaafu anayewakarahisha, achape lapa aende zake.
Majasiri zaidi wamemdhihaki mstaafu achape lapa aende Burundi! Waheshimiwa sasa wanaupiga mwingi na wanahomola kisawasawa, lakini hakuna anayemkumbuka mstaafu.
Wamkumbuke wachekwe? Si ametenda wema, achape yebo sasa na asingoje shukurani.
Nchi sasa imejaa waheshimiwa wema na ‘wanaoupiga mwingi’ pande zote, lakini siyo kwa wastaafu. Hata wanajeshi wetu waliopata vilema vya maisha wakilipigania Taifa hili wanaishia kuambiwa waandikishe majina yao na watapata chochote… kwa maneno tu, huku mstaafu akiendelea kupotelea polepole Kinondoni.
Waheshimiwa wanaosifiwa kwa kuwa wema na wanaoupiga mwingi sasa wanaupiga mwingi kwelikweli, lakini siyo kwa wastaafu waliojenga nchi hii na kuwawezesha kuupiga mwingi.
Wameupiga mwingi kwa wawakilishi wanaosemekana kuwa wanawawakilisha wananchi, wakiwemo wastaafu, na kufanya wapokee mshahara wa shilingi… mama wee! milioni 14… kwa mwezi wakati mstaafu aliyeijenga nchi hii kwa jasho na damu yake anapokea shilingi… mama wee! ...shilingi laki moja tu ya pensheni kwa mwezi!
Hivi mstaafu aliyeipa nchi hii uhuru wake, kuijenga kwa damu na jasho lake na hata kuipigania ilipobidi ili kuilinda ana haki kweli ya kupokea shilingi ‘Laki si Pesa’ kama pensheni yake kwa mwezi, lakini hawa watoto wake ambao walisoma bure kwenye shule alizojenga yeye na akiwalipia wasome bure kwa Paye (Pay As You Earn) yake, ndio sasa wamekuwa na haki ya kupokea shilingi… Mungu wangu! milioni 14 kwa mwezi na wanaona ni sawa tu?
Haya, waheshimiwa wameupiga mwingi tena na kuwezesha hata wenza wa waheshimiwa wastaafu kulipwa asilimia njema tu ya pensheni anayopata mheshimiwa mumewe ama mkewe ambayo ni mamilioni yaliyotakata, lakini wenza wa wastaafu wa nchi hii ambao walipambana sambamba na wenza wao ili nchi ipate uhuru wake, wanaishia kugombania na waume ama wake zao hicho hichoki ‘laki si pesa’ chao.
Kinachosikitisha zaidi ni kuwa hoja ya kuwawekea pensheni ya mamilioni kwa mwezi wenza wa waheshimiwa imepitishwa, lakini nyongeza ya wastaafu imeendelea makitaimu hapohapo kwa miaka 20 sasa, huku kapensheni ka wenza wao kakiwa ni ‘ajabu la tisa’ la dunia lisilokuwepo.
Tenda wema uchape yebo na usingoje shukurani. Sawa, lakini wastaafu wanasema hawatachapa lapa maana hii ni nchi yao, wachape lapa waende wapi. Waheshimiwa wauangalie ujumbe huu kwa umakini na kuufanyia kazi na hatimaye kuupiga mwingi kwa wastaafu, hata Kinondoni itawasubiri wapate walichotolea jasho lao kwanza.
Nchi iwe ya wananchi wote wanaostahili kula kipande cha keki ya Taifa walichopika wastaafu. Nchi isiishie kuwa kijikampuni cha Watanzania wachache wanaohomola kama vile hakuna kesho bila kumkumbuka mstaafu aliyeijenga nchi hii mpaka wao wakawa waheshimiwa. Mwenye masikio na asikie.