Muungano wetu unahitaji hekima, si hisia
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa Aprili 26, 1964, si tukio la kawaida katika historia ya Afrika. Ulizaliwa wakati bara likiwa katika kipindi cha misukosuko ya ukoloni, mapinduzi na migawanyiko ya kisiasa. Wakati mataifa mengi yakitafuta njia za kujitenga, viongozi wa Tanganyika na Zanzibar walifanya uamuzi wa kuunganisha dola mbili huru na kuunda taifa moja.
Uamuzi huo haukulenga manufaa ya kisiasa ya wakati huo, bali uliweka mbele maslahi ya vizazi vijavyo. Ndiyo maana zaidi ya miongo sita baadaye, Muungano wa Tanzania unabaki kuwa miongoni mwa miungano michache duniani iliyodumu bila kuvunjika. Umestahimili mabadiliko ya mfumo wa kisiasa kutoka chama kimoja hadi vyama vingi, mageuzi ya kiuchumi na changamoto mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Kwa waasisi wake, Muungano haukuwa makubaliano ya kisiasa pekee. Ulikuwa msingi wa kujenga usalama, umoja na maendeleo ya wananchi wa pande zote mbili. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisisitiza mara kadhaa kuwa kuvunja umoja wa watu kuna gharama kubwa kuliko tofauti zinazoweza kujitokeza. Vivyo hivyo, Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, aliamini kuwa nguvu ya Watanganyika na Wazanzibari ingeongezeka zaidi wakiwa taifa moja kuliko kila upande kusimama peke yake.
Kwa zaidi ya miaka 60, Muungano umeijengea Tanzania utambulisho wa kipekee. Wananchi wameishi, kufanya biashara, kusoma, kuwekeza na kujenga familia bila mipaka ya Tanganyika na Zanzibar. Juu ya yote, umeifanya Tanzania kuwa na sauti moja katika diplomasia ya kimataifa na umeimarisha uwezo wa taifa kulinda usalama wake na kushughulikia changamoto za kikanda na kimataifa.
Hata hivyo, mafanikio hayo hayaondoi ukweli kwamba Muungano umekuwa ukikabiliwa na changamoto zinazohitaji majibu ya busara. Hoja kuhusu mgawanyo wa madaraka, masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano, mgawanyo wa mapato, fursa za ajira na utendaji wa taasisi zimeendelea kujitokeza kwa nyakati tofauti. Aidha, zipo hisia na mitazamo inayohitaji kujadiliwa ili kuendelea kuimarisha mshikamano wa wananchi wa pande zote mbili.
Changamoto hizo hazipaswi kutafsiriwa kama ishara ya kushindwa kwa Muungano. Badala yake, zinaonyesha kuwa ni taasisi hai inayopaswa kuendelea kujitathmini na kufanya maboresho kadri mazingira yanavyobadilika. Hakuna taasisi inayoweza kudumu kwa miongo mingi bila kurekebisha mifumo yake. Katiba hurekebishwa, sheria huboreshwa na sera huhuishwa ili ziendane na mahitaji ya wakati. Hata hivyo, kuboresha si sawa na kubomoa.
Katika miaka ya karibuni, mjadala kuhusu Muungano umeongezeka. Wapo wanaopendekeza mabadiliko makubwa ya mfumo uliopo na wapo wanaotetea uendelee kama ulivyo. Huo ni mjadala unaostahili katika jamii ya kidemokrasia. Lakini demokrasia yenye afya hujengwa kwa hoja zinazolenga suluhu, si kauli zinazoweza kupandikiza chuki au kuwagawa wananchi.
Ni muhimu kutambua kuwa serikali hubadilika, vyama vya siasa hushinda na kushindwa, na viongozi huingia na kuondoka. Taifa ndilo hubaki. Vivyo hivyo, Muungano unapaswa kuendelea kutazamwa kwa mizani ya maslahi ya taifa badala ya maslahi ya muda mfupi ya kisiasa. Kauli yoyote kuhusu Muungano inapaswa kujengwa juu ya historia yake, Katiba na wajibu wa kulinda mshikamano wa Watanzania.
Wapo wanaoamini kuwa njia bora ni kukaa kimya ili kuepusha mjadala kuhusu Muungano. Mtazamo huo unaweza kupunguza joto la hoja kwa muda, lakini hauondoi maswali yaliyopo. Suluhu ya kudumu ni kuyajadili kwa uwazi, ukweli na heshima, huku maslahi ya taifa yakiwekwa mbele.
Tunahitaji viongozi wanaosikiliza, wananchi wanaovumiliana na wasomi wanaotafuta suluhu badala ya kuongeza mpasuko. Tunahitaji mijadala inayojenga uelewa na kuimarisha umoja, badala ya kushindana kwa maneno yanayoweza kudhoofisha tunu ambazo taifa limezijenga kwa zaidi ya nusu karne.
Historia inaonyesha kuwa mataifa yanayodumu si yale yasiyokuwa na changamoto, bali yale yanayokuwa tayari kufanya maboresho bila kuvunja misingi yake. Tanzania inaweza kuendelea kuwa mfano huo ikiwa kila changamoto ya Muungano itaonekana kama fursa ya kuuimarisha badala ya kuudhoofisha.
Hilo ndilo somo walilotuachia waasisi wa taifa. Walituachia nchi moja, bendera moja na matumaini kwamba vizazi vijavyo vitakuwa na hekima ya kulinda walichokijenga. Ni wajibu wa kila kiongozi, mwanasiasa na mwananchi kuhakikisha mijadala kuhusu Muungano inatanguliza maridhiano kuliko migawanyiko, hoja kuliko jazba na uzalendo kuliko maslahi binafsi.
Mwisho wa yote, Muungano si wa viongozi wa jana wala wa leo. Ni urithi wa Watanzania wote. Kila kizazi kina wajibu wa kuuboresha kwa busara, kuuenzi kwa uzalendo na kuulinda kwa maslahi ya vizazi vijavyo.
0617368599