Mwaifwani: Nani anapanga bei za vyakula safarini?
Muktasari:
- Bei za vyakula kwenye migahawa hii hazina tofauti na bendera, zinapepea uelekeo ziutakao. Nimewaza hili kwa sababu abiria hawana chaguo la sehemu ya kununua chakula zaidi ya pale dereva wa basi husika atakaposimama.
Nilipokuwa mtoto nilifurahia kusafiri, leo nimekuwa mtu mzima, maisha yananilazimisha kusafiri. Niwapo safarini nayaona mengi, mojawapo ni bei za vyakula kwenye vituo ambavyo abiria wa mabasi ya mikoani tunalazimika kula.
Bei za vyakula kwenye migahawa hii hazina tofauti na bendera, zinapepea uelekeo ziutakao. Nimewaza hili kwa sababu abiria hawana chaguo la sehemu ya kununua chakula zaidi ya pale dereva wa basi husika atakaposimama.
Tuanze kwa kujiuliza: je, ni nani anachagua vituo vya chakula vya mabasi ya mikoani na huwa anazingatia vigezo gani? Nani anadhibiti bei za vyakula kwenye vituo hivi? Msingi wa maswali haya ni kuwa wauzaji wa vyakula kwenye vituo hivi wameachwa wapange bei za vyakula vyao kwa namna watakavyoona inafaa. Bahati mbaya sana, bei hiyo si rafiki wala ya soko.
Ni wazi kuwa iwapo mabasi ya mikoani yatapitiliza, vituo hivi vitalala na vyakula vyao kwa sababu wakazi wa maeneo jirani hawawezi kulipa gharama za vyakula ambazo vituo hivi vinawatoza abiria. Hii ni wazi kwa sababu hakuna bei ya soko na huduma haiendani na gharama.
Nani atalipa Sh8, 000 kwa vipande vya chipsi kavu unavyoweza kuvihesabu kwa macho na kipande kimoja cha nyama ya kuku iliyopoa? Hakuna, isipokuwa abiria ambao dereva wa basi walilopanda ameamua kuwaleta hapo, watake watanunua, wasitake watanunua. Hawana chaguo.
Hata kwenye vinywaji, vituo hivi vinatoza zaidi ya bei elekezi, nani anajali? Wauzaji wanaviuza kwa bei watakazoamka nazo siku hiyo kwa sababu wana uhakika abiria watalipa tu. Wakati abiria anahesabia hela mfukoni huku akijiuliza ni lini bei ya soda ilipanda, dereva wa basi anapiga honi nyingi kuashiria muda wa kula umeisha, kawia uachwe na basi, utaomba 'lift' kwenye lori.
Hali hii imekuwepo siku zote. Inaendelea kuwa jinsi ilivyo kwa sababu kila mmoja anadhani hili jambo halimhusu, jambo ambalo si sawa kwa sababu nchi yetu inayo mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa nchi kavu iitwayo Latra. Nani haijui Latra? Kila siku uchwao inatangaza viwango vipya vya nauli. Je, Latra haijui kuwa wanaosafiri ni watu na watahitaji kula wawapo safarini?
Katika mazingira ya safari, ambayo msafiri hana chaguo jingine zaidi ya pale basi liliposimama, msafiri tayari ana nafasi ndogo ya ushawishi wa bei na maafikiano ya kibiashara kabla ya kununua. Mazingira ya safari yanamfanya mtoa huduma ya chakula kuwa na nafasi ya juu ya kuamua bei ya chakula chake, hata kama bei hiyo ni uonevu kwa msafiri na faida isiyo ya haki kwa muuzaji.
Pengine kuna kundi la watu wanufaikao na hizi faida zisizo za haki wazipatazo wauza vyakula kwenye vituo hivi, lakini hoja ya msingi ni kuwa sisi raia wa nchi hii, kwa mujibu wa Katiba yetu, tuliacha majukumu yetu kwa Serikali ili Serikali isimamie tusinyonywe.
Serikali, kupitia Latra, haipaswi kufumba macho kama vile hakuna kinachoendelea angali ni dhahiri kuwa wasafiri tunanyonywa.
Umewahi kusafiri ikafika muda wa kula ukawaona wasafiri wenzio wasio na fedha za kutosha jinsi wanavyotia huruma kwa kushindwa kumudu gharama za vyakula kwenye vituo hivi? Ni jambo la kusikitisha sana. Kwa huruma, unaweza kumsaidia mtu leo ama kesho lakini hutatatua tatizo la siku zote.
Tatizo la msingi ni kuwa wafanyabiashara ya chakula kwenye vituo hivi wameachwa wapange bei kwa namna wanavyotaka na bei hizo zinaumiza Watanzania wengi wenye vipato vidogo. Hivyo basi, namna pekee ya kuwasaidia Watanzania hawa ni kuwaondoa kutoka kwenye makucha ya unyonyaji.
Labda tujiulize tena: je, kwa nini migahawa ambayo abiria wanalazimishwa kula isiuze vyakula kwa bei ya soko ilhali wateja wanaletewa hadi mlangoni? Kama wenye mabasi wanapewa bei elekezi za nauli, kwa nini wenye migahawa wasipewe bei elekezi za vyakula? Lengo la kutaka udhibiti kwenye biashara ya chakula kwa abiria si kuifanya Serikali mwamuzi wa biashara baina ya watu, hapana, lengo ni kulinda haki ya abiria kupata chakula wawapo safarini. Sio tu kupata chakula, bali kupata chakula kwa utaratibu unaoepuka unyonyaji kati ya mtu na mtu.
Waswahili wanasema 'tembo hazidiwi na mkonga wake' na mimi nina imani Latra hawazidiwi na watoa huduma ya chakula kwa abiria. Kwa kusema hivyo, natoa rai kwa Latra kuingilia kati suala hili kwa vitendo thabiti, hasa msimu huu wa mwisho wa mwaka ambao Watanzania wengi wanasafiri kurudi makwao.
Clay Mwaifwani ni mwananchi wa kawaida, anapatikana kwa simu: 0758850023 au baruapepe [email protected]