Mwaka 2017 uwe wa mtazamo mpya kwa walimu

Hussein Madeni

Muktasari:

  • Mwaka umeanza na walimu wengi sasa wapo shuleni wakiendelea kuwajibika. Katika kufanikisha majukumu yao ya ualimu ya kila siku, moja ya maandalizi yao ni kusoma nyaraka iitwayo kwa Kiingereza ‘Standing Orders for the Public Service 2009.

Mfumo wowote wa elimu unategemea uongozi bora pamoja na walimu mahiri ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Mwaka umeanza na walimu wengi sasa wapo shuleni wakiendelea kuwajibika. Katika kufanikisha majukumu yao ya ualimu ya kila siku, moja ya maandalizi yao ni kusoma nyaraka iitwayo kwa Kiingereza ‘Standing Orders for the Public Service 2009.

Nyaraka hii imesheheni mambo yote yanayomuhusu mwalimu kuanzia siku anayoanza kazi mpaka anastaafu.

Miongoni mwa mambo ambayo ningependa kuwakumbusha walimu yaliyomo katika nyaraka hii ni kutilia maanani muda wa kuripoti na kuondoka kazini.

Jambo hili limekuwa likipuuzwa na halizingatiwi kuanzia kwa maofisa elimu, waratibu elimu kata, wakuu wa shule mpaka walimu wenyewe.

Baadhi ya walimu wamekuwa wakiripoti kazini muda wanaotaka na wanaondoka muda wowote pasipo kuwa hofu ya aina yoyote. Tabia hii imekuwa imefikia hatua ya kujenga usugu kwa walimu.

Cha kustajabisha ni kuwa, hata wakipewa onyo la mdomo na wakuu wao hudharau. Hii ni kwa sababu mamlaka hazizingatii sheria na kanuni zilizopo

Jambo la pili na ambalo ni muhimu kwa walimu tunapoanza mwaka mpya ni maandalizi ya kusoma vitabu vya kiada na ziada kulingana na darasa unalotegemea kufundisha huku ukizingatia mada mahususi. Hili halifanyiki kwa ukamilifu.

Nasema haya kwa kuwa ni nadra kukuta mwalimu akiwa mwanachama wa maktaba au ana tabia ya kusoma vitabu, tafiti, majarida au magazeti mbalimbali.

Kazi ya ualimu inahitaji mwalimu kujiandaa kuhusu somo na mada anazohitajika kufundisha. Kusoma kunaimarisha umahiri wa kufundisha.

Usomaji vitabu hauna budi kwenda sambamba na maandalizi ya azimio la kazi (Scheme of work). Maandalizi haya yanatakiwa kufanyika kwa ukamilifu. Utakuta mpaka muhula unaisha mwalimu hajaandaa azimio la kazi.

Siku hizi tabia za walimu wengi hazisadifu miiko ya ualimu. Ukipata bahati ya kukaa ofisini na walimu utagundua kuwa walimu wanatukanana, wanasengenyana na kufitiniana tena wakati mwingine mbele ya wanafunzi.

Licha ya kuwa kuna waraka wa mavazi kwa watumishi wa umma, changamoto ya kuvaa mavazi yasiyofaa imekuwa kubwa kwa walimu wengi. Hili halihitaji utafiti wa kina. Tembelea shule zisizozidi tano eneo lolote ulipo, naamini hutokusa kukutana na walimu waliovaa mavazi yasiyoendana na maadili yao. Huu ni mwaka wa kuabadilika.

Mbali ya kusoma nyaraka hiyo niliyoitaja awali na kuifanya kama rejea ya kila siku, niwasihi walimu kuzingatia yafuatayo kwa mwaka 2017.

Mosi, tafuteni vitabu vya sheria na kanuni za ajira ili kufahamu masuala mbalimbali ya kiutumishi. Kanuni hizi pamoja na mambo mengine zinaweza kuwaepusha na matukio kama yale ya walimu wa Mbeya ya matumizi makubwa ya nguvu katika kudhibiti nidhamu kwa wanafunzi

Pili, washashawishini wanafunzi kusoma vitabu ili hatimaye nanyi mpate kazi ya kuwa waandishi wa vitabu hivyo, jambo linaloweza kuwaongezea kipato.

Kumbukeni, umahiri, nidhamu na wito wenu ni muhimu katika kufanikisha malengo ya elimu nchini yanatimia. Walimu ni nguzo muhimu ya elimu, ufanyeni mwaka huu kuwa wa mabadiliko ya kimtazamo, tabia na taaluma.

Hussein Madeni ni mdau wa elimu, anapatikana kwa simu; 0622 571 189.