Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwalimu, wazawa watupe muendelezo

Msimu wa Ligi Kuu 2024/2025 umeanza vizuri kwa mshambuliaji wa Fountain Gate, Selemani Mwalimu kutokana na kasi ya kufumania nyavu ambayo amekuwa akiionyesha.

Mchezaji huyo katika mechi sita alizoichezea timu yake hadi sasa, tayari ameshaifungia mabao manne ambayo yanamfanya aongoze chati ya kufumania nyavu hadi sasa.

Makali hayo ya kufumania nyavu ambayo Mwalimu ameanza kuyaonyesha, yanafanya wengi wakumbuke kile alichokifanya msimu uliopita katika Ligi Kuu ya Zanzibar ambapo alimaliza akiwa mfungaji bora kwa kuifungia timu yake ya KVZ idadi ya mabao 20 katika michezo 27 ambayo alicheza.

Kana kwamba haitoshi, Mwalimu pia katika msimu huo uliopita alimaliza akiwa amepiga pasi saba za mwisho kwenye ligi hiyo ya Zanzibar.

Namba alizoanza nazo ndani ya kikosi cha Fountain Gate zinathibitisha kuwa haikukosea kumsajili kwani angalau amekuwa akihusika na bao moja katika kila mchezo, jambo ambalo ni zuri na linalotakiwa kufanywa na mchezaji wa nafasi ya ushambuliaji.

Mwanzo huo mzuri wa kufumania nyavu haujawa kwa Mwalimu pekee bali pia kuna wachezaji wengine wazawa ambao katika chati ya wanaowania tuzo ya ufungaji bora msimu huu wanaonekana kuwa na namba nzuri.

Pale Fountain Gate mbali na Mwalimu, yupo Edgar William aliyefumania nyavu mara tatu na anaonekana kuunda safu tishio ya ushambuliaji na mwenzake.

Wazawa wengine ambao wameonekana kuanza kwa kuchanga vyema karata zao kwa kufunga mabao ni Valentino Mashaka, Clement Mzize, Crispin Ngushi, Nassor Saadun, Salum Kihimbwqa, Paul Peter na David Ulomi.

Hili ni jambo lenye faida sana kwa nchi yetu kwa vile wazawa hao wanaonyesha uwezo wa kufumania nyavu katika kipindi ambacho Taifa lilianza kuwa na uhaba wa washambuliaji wazawa kwa ajili ya kuitumikia timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

Kama wachezaji hao watakuwa na muendelezo mzuri wa hicho wanachokifanya maana yake benchi la ufundi la Taifa Stars litakuwa na wigo mpana katika uteuzi wa kikosi cha timu hiyo siku za usoni tofauti na sasa ambapo haina machaguo mengi kwa wachezaji wa nafasi za ushambuliaji.

Jambo lingine la kuvutia ni kwamba wachezaji hao wote wana umri mdogo hivyo wana nafasi ya kutumikia timu yetu ya taifa kwa muda mrefu na hata kusogea mbali zaidi kwa kufuata malisho ya kijani katika ligi kubwa za ndani na nje ya Afrika.

Ukiondoa hao washambuliaji, kuna makipa pia ambao mechi za mwanzo wameonyesha viwango bora ambavyo vimechangia kwa kiasi kikubwa kuweka salama milango ya timu zao kwa kutoruhusu mabao katika baadhi ya mechi za ligi.

Majina ya mfano katika nafasi ya kipa ambayo yameanza vizuri msimu ni Musa Mbisa wa Tanzania Prisons, Yona Amos wa Pamba, Fikirini Bakari wa Fountain Gate Denis Richard wa JKT Tanzania na Zubery Foba wa Azam FC.

Fikirini Bakari kwa mfano pale ndani ya Fountain Gate amefanikiwa kulishawishi benchi la ufundi kutompa nafasi kipa wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria, John Noble na badala yake kumuamini yeye katika kikosi cha kwanza.

Wachezaji hao wazawa walioanza vizuri wengi ni wale wanaocheza katika nafasi ambazo kwa muda mrefu nchi yetu imekuwa na uhaba na mahitaji ya wachezaji wa kuzicheza.

Kwa wanachokifanya sasa wanastahili kupongezwa lakini jambo la msingi ambalo wanatakiwa kulifanya ni kuhakikisha kunakuwa na muendelezo wake badala ya kuishia njiani na baadaye wakatoa fursa kwa wachezaji wa kigeni kutawala.

Ni jambo lililo wazi kwamba vipaji vya soka havijawahi kuwa changamoto hapa nchini na mara kwa mara wachezaji wetu wamekuwa na mwanzo mzuri kwenye ligi au mashindano mengine mbalimbali ambayo wamekuwa wakishiriki lakini ambacho kimekuwa kikiwaangusha mara kwa mara ni kukosekana kwa muendelezo wa kufanya vizuri kwa muda mrefu.

Kile ambacho wanakitoa kimekuwa kama homa za vipindi kwamba kuna wakati wanaibuka na kufanya vizuri na wakati mwingine makali yao huwa hayaonekani jambo ambalo huchangia thamani zao kuwa chini.

Iko mifano mingi ya wachezaji wazawa ambao kwa nyakati tofauti, mwanzoni mwa msimu walionyesha kuwa wangemaliza kwa mafanikio makubwa lakini mambo yakawa kinyume hapo baadaye.

Mfano mzuri ni mshambuliaji wa Dodoma Jiji ambaye aliwahi kuzichezea pia Yanga na Namungo FC, Reliants Lusajo ambaye katika msimu wa 2021/2023 alianza vyema kwa kuifungia Namungo FC mabao sita katika mechi 10 za mwanzo na licha ya wengi kuamini kwamba angemaliza akiwa kinara wa kufumania nyavu au hata kupachika idadi kubwa ya mabao, mambo hayakwenda kama yalivyotegemewa kwani aliishia kufunga mabao 10 tu kwa msimu huo.

Wachezaji wetu wazawa ambao wameanza msimu kibabe, wanapaswa kufahamu kwamba kwa sasa wao bado ni wa daraja la kawaida na fursa ya kutambulika kama bora ipo ila ni hadi kile wanachokifanya wataendelea nacho hadi mwishoni mwa msimu na baada ya hapo wakifanye katika msimu unaofuata au zaidi.

Wapo wachezaji wachache ambao kwa nyakati tofauti walifanikiwa kuwa na muendelezo wa ubora wao na ndio maana vitabu vya historia vinawataja kama bora miongoni mwa waliowahi kuitumikia ligi yetu.

Kuna mfano wa wachezaji kama Mohammed Hussein 'Mmachinga', John Bocco, Abeid Mziba, Abdallah Kibadeni, Sunday Manara na Juma Mgunda ambao hawakuishia kutamba katika mechi za mwanzo za msimu au kwa msimu mmoja tu.