Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nani anastahili kupewa maua na miba yake na Mstaafu?

‘Njaanuari’ hiyoo inakuja, na mwisho wa mwezi huo mstaafu wetu wa kima cha chini na wenzake wanategemea kupata nyongeza ya pensheni yao ya shilingi elfu hamsini ili hatimaye watie mfukoni laki na elfu hamsini iliyotangazwa Novemba katikati na ikaelezwa wastaafu hao wataanza kuipata mwisho wa ‘Njaanuari’, miezi miwili na nusu baadaye. Haijaelezwa kwa nini.

Mstaafu wetu analazimika kusubiri mpaka mwisho wa Njaanuari ili apate pensheni yake ya laki moja na nusu iliyoongezwa, huku akiomba Mungu kusitokee dharura yoyote nchini inayoweza kufanya nyongeza yake ya elfu hamsini kwa wastaafu wote wa kima cha chini ichape lapa. Hii ni Bongo. Tunaijua wenyewe. Lolote linawezekana.

Kunaweza kukatokea dharura yoyote itakayobidi nyongeza ya mstaafu ichukuliwe, ili ikazibe dharura hiyo kabla haijaingia mifukoni mwao. Hatuombei, lakini inawezekana. Kama wastaafu wa kima cha chini wameweza kukaa miaka 20 bila nyongeza ya pensheni na watu wakaona ni sawa tu, wakati hatupo kwenye miezi 18 ya kufunga mikanda kama ilivyokuwa wakati ulee baada ya vita vya Kagera, kila kitu kinawezekana!

Ndio hapo mstaafu wetu amejikuta akitafakari ili kufahamu hasa ni nani amepewa jukumu la kumuongezea pensheni yake, potelea mbali baada ya miaka 20, au kumuwekea kikokotoo ili sasa asichukue hela yake yote aliyokatwa kwenye mshahara wake, ili akafie mbele mwenyewe. Ni nani anawezesha haya? Ni Siri-kali au kibubu chake? Ni vema kujua hili ili maua yaende panapostahili, hali kadhalika miba!

Tukumbuke kwamba ua la waridi ni zuri sana, lakini unapotaka kulichuma ni lazima uwe muangalifu, ili miba yake isije ikafanya vitu vyake kwenye vidole vyako! Mstaafu wetu amekuwa kwenye ajira kwa miaka 40, na kwa miezi yote 4,800 ya miaka 40 hiyo amekatwa kodi ambayo anapenda kudhani kuwa kama angeitunza mwenyewe angekuwa mbali na asingekuwa na haja ya kukaa miaka 20 ili kuongezwa shilingi elfu hamsini na mtu! Miaka 20 kwa alfu hamsini?

Toka enzi za ‘marhum’ NPF, mstaafu aliamini anayeweza kutoa nyongeza ya pensheni yake alikuwa ni siri-kali, maana NPF ilikuwa kama ni tawi tu la siri-kali. Ndio maana hata yule Baba wa Taifa nyongeza ya mshahara wa wafanyakazi aliitolea kwenye mkutano wake wa Mei mosi, sikukuu ya wafanyakazi. Tukajizoesha na kujiaminisha kwamba siri-kali ndio ilihusika kwenye kuongeza mishahara na pensheni za wafanyakazi na wastaafu.

Katikati hapo katika kile tulichoamini kuwa ni maendeleo, nchi ikaanzisha rundo la vyama vya wafanyakazi, kila kimoja kikitunza pesa za wafanyakazi wa sekta yake. Pakatokea kiasi fulani cha ‘pata shika nguo kuchanika’ wakati wafanyakazi walipokuwa wanahamishwa kushoto, kulia na katikati, wengine ikiwachukua miezi kadhaa kujua walikuwa wametupiwa kwenye kibubu gani!

Kutokana na rundo hilo la vyama vya wafanyakazi, mstaafu wetu akapata matumaini kuwa hata mambo ya kuongeza mshahara ama kuongeza pensheni ya wastaafu yatakuwa ni mambo ya huku huku chini kwa vibubu vya wafanyakazi, maana ndio vinavyoshika hela zetu na kuzifanyia biashara, ingawa faida ya biashara hizo inafanywa kuwa haimhusu mstaafu! Hela yetu wenyewe inafanyiwa biashara, lakini faida yake haituhusu!

Vibubu vinapokea hela ya wafanyakazi iliyokatwa kwenye mishahara yao na kuwatunzia, biashara wanazofanya kupitia hela zao bila kuwauliza wenyewe, ndio inaviwezesha vibubu kufanya mambo mema mengi tu kumsaidia mstaafu kukabiliana na hali ngumu ya maisha, kama kuwagharimia wafanyakazi kina mama wanapokuwa wajawazito, kugharimia mazishi ya mstaafu anaporudi mavumbini alikotoka, na bima ya afya kwa wafanyakazi na watoto wao, ingawaje hili bado halijakaa vyema!

Hili linamfanya mstaafu afikiri vibubu vinavyotunza hela ya wafanyakazi na wastaafu ndio vingeweza kukaa na kupiga hesabu kujua mstaafu anastahili nyongeza ya pensheni kila baada ya miaka mingapi, sio miaka 20. Na kutokana na akiba yake wanayofanyia biashara, mstaafu wetu ana hakika kwamba vibubu vingekuwa havina haja ya kuwapa wastaafu miezi mingine miwili na nusu ya ziada kusubiri nyongeza hiyo, maana kila kitu wanacho na tangazo la nyongeza lingetoka na mwisho wa mwezi huohuo nyongeza ikiwa mfukoni!

Siri-kali haishughuliki na akiba za wafanyakazi. Inasimamia tu shughuli hiyo, na kusubiri kodi yake. Ndio maana ilianzisha hivi vibubu maalumu kwa ajili ya hilo. Mstaafu wetu anaamini hata hili la nyongeza ya pensheni ya wastaafu lingepaswa kuwa jukumu la vibubu husika, maana ndio vyenye hela ya mstaafu. Ndio itaweza kuwahakikishia wastaafu haya ya kupokea ‘laki si pesa’ kwa miaka 20 ndipo wapate nyongeza ya pensheni yao shilingi elfu hamsini yanabaki kuwa ‘hadithi ya Allan Kotameni!!

Wastaafu wanaipa siri-kali maua yake kwa hatimaye kuwapa nyongeza ya pensheni yao pamoja na kwamba bado ipo kwenye makaratasi tu na sio mifukoni mwao. Na ndiyo maana hata kwenye Krismasi kuna wastaafu wametoka kapa, hela haijaingizwa! Siri-kali ikumbuke tu kuwa mchuma ua la waridi anapaswa kutahadhari na miba yake! Mstaafu wetu anawatakia heri ya Mwaka mpya 2025 wasomaji wote wa Mwananchi.