NIKWAMBIE MAMA: “Kausha damu” ikaushwe, ujasiriamali uhuishwe

Maendeleo yana changamoto zake. Kila penye maendeleo yanayoelekea mafanikio ya jambo kunatanguliwa na ukakasi wa kutosha. Wakati wa kutafuta faraja tunapitia mambo mengi ya kutisha na kudhoofisha azma, inafikia hatua ya watu kuyalaani mapito ya mafanikio hayo. Na ni kawaida yetu wanadamu kukata tamaa katika changamoto hizi zinazotangulia mafanikio. Lakini waandishi na wanazuoni wanatufariji kuwa “kiza kingi ni ishara ya mapambazuko”.

Hakuna awezaye kushindana na athari za maendeleo. Wakati mwingine ni lazima maendeleo yasindikizwe na vyombo vya usalama viongoze mtiti wa kuwashurutisha wananchi kuyapokea. Utaona katika ujenzi wa miradi ya maendeleo inabidi kutokee upotevu wa makazi na mashamba ya watu wanayoyategemea kwenye maisha yao ya kila siku. Lakini hakuna jinsi, watu hao hao ndio wanaoyataka maendeleo.

Hivi sasa kama tunavyojua, ulimwengu mzima umehamia kwenye teknolojia. Yale makabrasha yaliyokuwa yakibebwa kwapani sasa yamehamia kwenye mitandao kama njia rahisi ya kutafuta ajira na fursa. Rekodi za wagonjwa, miamala ya kibenki, masjala za kiofisi, maktaba za vitabu, mauzo na manunuzi, habari, elimu na mambo kede kede, sasa hayana budi kufanyika kimtandao.

Pamoja na faida nyingi za teknolojia, hali ya maisha inazidi kuwa ngumu siku hadi siku. Duniani kote kumekuwa na ukatili kutoka kwa watoa huduma muhimu kwenda kwa wahitaji wa huduma hizo. Ni wazi kuwa wenye funguo za teknolojia wanafanya kama waliokosana na watumiaji wa huduma hii muhimu kwa jinsi wanavyowatoza gharama kubwa. Lakini kwa kuwa tunataka maendeleo, hatuna budi kufanya ya mtaka cha uvunguni.

Kwa kuwa hapo ndipo maendeleo yalipotufikisha, tumejikuta hatuna budi kutafuta mbinu za ziada kujikwamua kiuchumi. Zamani tulizoea kuwaona wafanyakazi wa Serikalini wakitegemea ajira zao mpaka ulipofika wakati wa kustaafu, lakini sasa ni lazima wajiongeze katika kilimo, biashara na shughuli nyingine ilimradi waweze kukidhi mahitaji muhimu kama matibabu, kusomesha watoto na kulipa kodi za makazi.

Ndoto za kusubiri kustaafu na kujenga nyumba zao kwa fedha za kiinua mgongo zikafutwa. Wengi tumewashuhudia wazee wetu wakisaga lami kuyafuatilia mafao yao bila kuyapata, hadi walipoiaga dunia. Waajiriwa wakaona kumbe njia bora ni kupambana wangalimo kwenye ajira. Kiinua mgongo kimekuwa sawa na hadithi ya kipofu anayemsaka paka mweusi katika kiza kinene, kumbe paka mwenyewe hayupo!

Hivyo wafanyakazi wengi waliamua kujaribu ujasiriamali. Lakini haikuwa rahisi kwa mwajiriwa anayelipa kodi na kusomesha watoto kudunduliza kipato chake hadi kujijengea nyumba. Pia si kitu rahisi kupata msingi wa biashara kwenye mshahara ambao tayari una majukumu kama yote. Mshahara unaoliwa kabla haujapokewa. Hivyo njia pekee ya kufanikiwa ikaonekana kuwa ni mikopo.

Taasisi zote za kifedha nchini zinatangaza mikopo hasa kwa wafanyakazi. Matangazo yanajipambanua kuwa ndiyo njia ya mkato kuelekea kwenye mafanikio. Lakini baada ya kuuingia mkopo ndipo mkopaji anakutana na msalaba wa riba na madeni. Badala ya kufanya kazi, mtu anajikuta akikimbizana na marejesho kila kukicha bila mwisho. Wakapoteza nyumba na mali zao walizoweka rehani kwenye taasisi hizo.

Huku uswahilini hali ni mbaya zaidi. Wajasiriamali na wamachinga walipokaribia kupoteza dhamana zao (kufilisiwa) ndipo wanapojikuta wakipandikiza mkopo juu ya mkopo ili kurejesha mkondo wa marejesho. Lakini riba za mikopo hiyo zinayaua kabisa matarajio yao na kujikuta wakiingia kwenye sifa za kutokopesheka. Bila kutarajia wanajikuta wakibisha hodi kwa “kausha damu”.

Kausha damu ni mfumo usio rasmi uliotengenezwa na watu wachache walio na uwezo wa kifedha. Wanaokopesha kwa masharti nafuu zaidi ya taasisi za fedha, lakini wanapanga marejesho na riba kwa kadiri watakavyo. Wanayageuza mateso ya masikini kuwa fursa, na wanaitumia fursa hiyo kwa kuwakamua kila senti wanayoifanyia kazi. Wapo makausha wanaovuna zaidi ya asilimia mia kutokana na fedha wanayokopesha.

Katika nchi yenye tatizo kubwa la ajira, ujasiriamali ndio ufumbuzi pekee kwa wananchi. Katika kila kona hapa duniani tunaona bidhaa za China zinavyokamata soko. Wenzetu walifanikiwa kuisimamia sekta hii hadi kwenye ushindani wa kimataifa. Bidhaa za wajasiriamali wao zinashindana na bidhaa za viwandani, hivyo kufanya mauzo makubwa hasa katika ukanda wetu. Haya ni matokeo ya uwezeshaji katika elimu ya ujasiriamali na mikopo salama kutoka kwenye mamlaka zao.

Mjasiriamali wa Kitanzania naye asitambuliwe kuwa mlipa kodi tu. Bali awezeshwe kuwa balozi wa kutangaza bidhaa zetu ulimwenguni. Kwa njia hii atainua uhai wa viwanda vyetu, atapunguza tatizo la ajira na kuongeza pato la Taifa kwa ukubwa. Asichukuliwe kuwa chombo cha kuwatajirisha kausha damu, ila awezeshwe kusimama mwenyewe katika biashara kwa manufaa ya Taifa.

Njia pekee ya kumnusuru kukaushwa damu yake ni kumpa elimu bora ya ujasiriamali na mikopo yenye masharti nafuu yenye riba inayobebeka. Taasisi za fedha kama Benki na makampuni ya simu ziwekewe viwango elekezi vya riba, na Vikoba iongezewe nguvu na kuthibitishwa kuanza na wamachinga wanaojitafuta. Lengo liwe maendeleo kwa wote kwa sababu hata nyumba zikivunjwa kupisha ujenzi wa barabara, tunaonufaika ni sote.