NIKWAMBIE MAMA: Mlinzi na mvunja sheria ni mwanasheria mwenyewe
Wakati tunauanza mwaka 2024, naomba nirejee jambo la mwaka jana. Ulianzisha jambo ninaloamini likifanyiwa kazi mwaka huu litakuwa ni ukombozi kwa kila Mtanzania.
Ilikuwa ni Tume uliyoiunda na kuipa majukumu ya kupitia na kurekebisha Haki Jinai na utekelezaji wa sheria kwenye vyombo vya kusimamia sheria. Tume hiyo iliundwa Januari 2023 na kuanza kazi Februari mwaka huo, hatimaye ikaja na mapendekezo yake muhimu.
Mapendekezo ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai yaliwaona viongozi wa vyama na Serikali, wanausalama, wanasheria na wengine ambao wangepaswa kuisimamia haki kuwa ndio wanaopindisha sheria na kuwaambukiza wengine udhaifu huo. Kama mawaziri na viongozi wa nchi wanavunja sheria kwa makusudi, walio chini yao watafanya nini?
Tume hiyo uliyoiunda chini ya Mwenyekiti, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman ilikuwa na maana kubwa hata kabla haijakabidhi mapendekezo yake. Nilidhani viongozi wetu wangekuwa na woga wa kurekebisha mienendo yao kabla hawajanyooshewa vidole. Lakini kilichoendelea ni jeuri, kiburi, dharau na kutojali wananchi watasikia nini, wala wewe mwenyewe utaamua nini juu yao.
Tume hiyo ilibaini uwepo wa udhaifu mkubwa kwenye mnyororo mzima wa Haki Jinai. Kulikuwa na shida kwenye kubaini na kuzuia uhalifu, kukamata na kupeleka watuhumiwa vituo vya polisi, uchunguzi wa upelelezi wa makosa ya jinai, uandikishaji mashtaka, usikilizaji wa mashauri ya jinai Mahakamani, waliotiwa hatiani kutumikia kifungo gerezani au kupewa adhabu mbadala na maisha ya wafungwa kumaliza vifungo vyao na kurejea uraiani.
Vilevile, Tume ilibaini Taifa halina mkakati mahususi wa kuzuia na kubaini uhalifu, jambo linalochangia vyombo vya utekelezaji sheria kujikita zaidi kwenye ukamataji holela badala ya kubaini na kuzuia uhalifu. Isitoshe, iligundua mnyororo mzito kwenye ngazi za uongozi ambako wakubwa hukiuka sheria kwa makusudi na kujichukulia sheria mikononi dhidi ya wananchi wa kawaida.
Kwa kawaida kiongozi huheshimiwa kwa misimamo na kauli zake zilizonyooka. Lakini uthabiti wake unaweza kuporomoka iwapo atawagawa wananchi kwenye pande tofauti. Kuhusu matumizi mabaya ya madaraka, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanalalamikiwa kutumia vibaya nyadhifa zao kwa kutoa amri ya kuwakamata na kuwaweka wananchi mahabusu. Tume ilipendekeza mamlaka haya yafutwe. Vyombo vilivyo na mamlaka ya kukamata vinapaswa kutumia mamlaka hayo kwa ajili ya kuzuia na kupambana na uhalifu.
Hata hivyo, wakati mwingine vyombo vya sheria vimekuwa vikitumika vibaya na hivyo kusababisha bughudha na kero kwa wananchi (kukamata watu bila sababu maalumu).
Kutokana na kuwekwa mahabusu bila sababu za msingi, baadhi ya watu walifungua na kushinda mashauri dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mfano ni Mchungaji Mtikila.
Tume ilibainisha desturi ya baadhi ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kutumia Sheria ya Tawala za Mkoa, wakuu wa wilaya na mikoa kuongozana na wajumbe wa kamati za usalama hata katika ziara ambazo hazistahili uwepo wa kamati hizo. Iliona pia wakuu wa mikoa na wilaya kujitambulisha kama wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama ni kinyume na sheria.
Wakuu wa mikoa na wilaya wakiwa wanatekeleza mamlaka ya ukamataji, walitakiwa kufuata vifungu sahihi kuepusha taharuki na uvunjifu wa amani. Tume ikapendekeza kiongozi yeyote atakayekiuka maagizo hayo awajibishwe, pia viongozi hawa wajitambulishe kama wenyeviti wa kamati za usalama wakiwa wanaongoza vikao vya baraza la usalama.
Mamlaka ya kumkamata na kumuweka mtuhumiwa kizuizini waliyonayo wakurugenzi wa halmashauri na maofisa watendaji wa kata yaondolewe, yaachwe mikononi mwa Jeshi la Polisi. Baadhi ya viongozi wa juu wa kisiasa wamekuwa wakitoa matamko na amri kwa vyombo vya dola kukamata na kuweka ndani wananchi wakati mamlaka hayo hawana. Viongozi hao waelekezwe kuzingatia sheria.
Mapendekezo ya Tume ni mengi, lakini yenye tija, na yanafaa yasimamiwe ili kupunguza uonevu. Tunaposema tunaongozwa katika utawala wa haki na sheria, hatuwataki viongozi wanaokuja na sheria zao za kujilinda na kuwaonea wananchi. Bali tunawataka viongozi wanaoziheshimu sheria na kuzisimamia. Vinginevyo nchi yetu itawavutia wavunjaji wa sheria, hivyo badala ya kuwa Paradiso ya Amani itakuwa Jehanamu ya Balaa.
Baadhi ya watu hawajui kwamba viongozi wa Serikali wanapaswa kufuata sheria hata pale watumiapo barabara. Hii inatokana na mazoea ya kuona gari la kiongozi linavunja sheria ya usalama barabarani, halafu na askari hana jeuri ya kumfanya chochote. Lakini endapo raia wa kawaida atajaribu kuvunja sheria atachukuliwa hatua muda huohuo.
Kwa sababu ya mbwembwe hizo, sio magari ya viongozi wa Serikali pekee wanaofanya jeuri barabarani. Madereva wengi wa magari ya Serikali wanaambukizwa jeuri ya kuvunja sheria wanapotumia barabara.
Bahati mbaya askari wa usalama barabarani wanawaangalia tu kwa woga wa kutojua magari hayo yamewabeba akina nani. Wanawaogopa wakubwa wao kwani hao ndio wanaotembea na hatima za ajira zao.
Viongozi wanapaswa kutambua kuwa hakuna mmojawao aliye juu ya sheria.