Serikali irahisishe upatikanaji vitambulisho kwa wanafunzi
Serikali imetangaza kuanzia sasa waombaji wa mikopo katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) watalazimika kuwa na namba (NIN) au kitambulisho cha Taifa.
Tunaamini kutumia njia hiyo kama kigezo rasmi cha kupata mkopo wa elimu ya juu ni hatua inayolenga kuboresha uwazi, uwajibikaji na utoaji wa huduma kwa wanafunzi wanaohitaji ufadhili wa masomo yao.
Licha ya hatua hiyo nzuri, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) inapaswa kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho hivyo kwa wanafunzi ili kuwawezesha kupata mikopo yao kwa wakati na isigeuke kuwa kikwazo.
Miongoni mwa hatua muhimu za kuchukua ni pamoja na kuondoa misururu, urasimu na mlolongo mrefu hadi kukipata kitambulisho.
Ili kurahisisha utoaji wa vitambulisho kwa wanafunzi, Serikali inatakiwa kuongeza ushirikiano wa karibu kati ya vyuo vya elimu ya juu na Nida.
Taasisi za elimu zinapaswa kutoa orodha ya wanafunzi walengwa wa mikopo mapema ili kuwawezesha kufuatilia mapema vitambulisho na Nida wenyewe ikibidi iwafikie wanafunzi walipo au wafungue ofisi zake ndogo ndani ya kampasi au karibu ili kutoa huduma ya haraka na ya kitaalamu.
Ushirikiano kama huo ukitekelezwa utasaidia kuondoa misururu ya foleni ofisi za Nida, jambo linaloweza kumwathiri mwanafunzi kufuatilia kila mara kitambulisho.
Aidha, mamlaka ya vitambulisho ipanue wigo wake wa mfumo wa e-Nida kuwaruhusu wanafunzi kujisajili mtandaoni kwa urahisi, mfano kuwa na e-Nida Wanafunzi na kupakia hati zao za kuthibitisha kama vile cheti cha kuzaliwa, barua ya usajili wa shule na ushahidi wa makazi. Mfumo huu ukiimarishwa utarahisisha mchakato na kupunguza muda wa kusubiri.
Pia kwa sababu wanafunzi ni wengi, wakiwekewa jukwaa lao pekee itarahisishwa kushughulikiwa jambo hilo kwa haraka kulingana na umuhimu wa vitambulisho hivyo kwao.
Pia, badala ya kumtaka mwombaji afike mahali alipofanya maombi, mamlaka hiyo iboreshe mfumo wake wa kuwafikishia taarifa waombaji kupima hali ya ombi moja kwa moja, hivyo mwanafunzi anapewa taarifa kupitia baruapepe au SMS kuhusu maendeleo ya maombi yao.
Kutokana na hitaji hilo la lazima, ni wakati mwafaka sasa kuhakikisha bajeti katika eneo hilo inaongezwa ili kusiwepo visingizio kwa wahusika kwamba malighafi zinazotumika kutengeneza vitambulisho hivyo hakuna, hivyo zinasubiriwa.
Aidha ni muhimu mamlaka husika kutoa mafunzo kwa watendaji wa ofisi zao kuhusu mahitaji maalumu ya wanafunzi ili waweze kubaini vitambulisho feki kama ilivyoibuliwa na gazeti hili wiki iliyopita, pamoja na kutoa miongozo ya hatua kwa hatua kwa wanafunzi kupitia mitandao ya kijamii na tovuti.
Elimu hiyo iende sambamba na kudhibiti matumizi holela ya vitambulisho hivyo kwenye taasisi nyingine za mikopo, ambapo zipo baadhi humtaka mhusika kuacha kitambulisho chake kama dhamana ya kupata mkopo.
Serikali iandae vikao vya mara kwa mara vya wadau, yaani vyuo na wanafunzi ili kubaini mapungufu katika upatikanaji wa vitambulisho
Shughuli hiyo, ili ifanyike kwa ufanisi, ni muhimu kuwepo na ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kitambulisho kisije kugeuka kuwa kikwazo kwa wanafunzi katika kupata mikopo.
Tunatahadharisha hilo kwa sababu, wapo wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu na wanahitaji mikopo lakini mazingira ambayo wanatokea ni vijijini na wakati mwingine wanakosa viambatanisho muhimu vinavyotakiwa, hasa nyaraka za wazazi wao.
Hilo likitekelezwa kwa ufanisi, itakuwa ni hatua muhimu kwa wanafunzi wengi kupata mkopo.