Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sheria ya lumbesa iangaliwe upya

Muktasari:

  • Sheria hiyo ya vipimo sura ya 320 inasaidia kukomesha vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na wafanyabiashara na taasisi mbalimbali dhidi ya wakulima au wazalishaji wa bidhaa.

Mwaka 2016 Serikali ilipitisha sheria ya kupiga marufuku upakiaji wa mazao na bidhaa kupita ujazo au uzito maarufu lumbesa katika magunia hususan kwa bidhaa kama dagaa, viazi na vitunguu.

Sheria hiyo ya vipimo sura ya 320 inasaidia kukomesha vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na wafanyabiashara na taasisi mbalimbali dhidi ya wakulima au wazalishaji wa bidhaa.

Idara ya Sera, Mipango na Utawala ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), iliwahi kufanya utafiti na kubaini matumizi ya vipimo kwenye mazao ya kilimo ambapo kila mwaka asilimia 30 ya mapato hupotea kutokana na matumizi ya lumbesa.

Utafiti huo pia ulibainisha kuwa kati ya kilo 120 hadi 130 huwekwa kwenye gunia la kilo 100 na hivyo kumnyonya mkulima na kuisababishia hasara Serikali.

Kwa mujibu wa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage upakiaji huo wa mazao kupita kiasi unawasababishia hasara wakulima na kuwataka kutumia vipimo halisi wanaponunua na kuuza bidhaa.

Pamoja na sheria hiyo inayotoa adhabu kali, kumekuwepo na hoja kinzani kutoka kwa wafanyabiashara ambao wanasema ujazo wa magunia wanayobebea mizigo hasa mazao ya kilimo haufikii kilo 100 kama tangazo la Serikali lilivyotolewa.

Kwa mfano, gunia la mahindi la kilo 100 haliwezi kubeba kilo 100 za viazi.

Mwenyekiti wa Soko Kuu jijini Mwanza, Hamad Nchora anasema magunia yanayotumika kununulia viazi mviringo kutoka kwa wakulima ukilijaza unapata kilo 80 badala ya 100 na mtu akiongeza kilo 20 zinazopungua juu ya gunia anakuwa amevunja sheria.

Nchora anasema kutokana na changamoto hizo, baadhi ya wafanyabiashara wameshindwa kuingiza bidhaa sokoni.

Kutokana na upungufu huo viazi vilivyokuwa vinauzwa Sh700 kwa kilo, vimepanda hadi Sh1,400 na bei ya chipsi kavu imepanda kutoka Sh1,500 kwa sahani hadi Sh2,000.

Katika utekelezaji huo wa sheria, ni dhahiri kuwa wanaoumia ni wengi kuliko wanaonufaika.

Pamoja na kuwapo sheria hiyo, ni ukweli usiopingika kuwa kila mmoja anavutia upande wake maana wapo wakulima wanaotaka kuuza kwa ujazo huo na tena wanauzia mashambani lakini pia wapo ambao wanaisikiliza Serikali, lengo likiwa ni kuhakikisha wanapata masilahi kwenye shughuli wanazozifanya.

Hata hivyo, upo umuhimu wa wakulima kujiamini kwani mazao wanayolima yanalo soko popote nchini, hivyo kudanganywa kwa kuweka lumbesa ni kujinyima haki ya msingi katika kukabiliana na wimbi la umaskini.

Niishauri Serikali kuwa, ni vyema ikaja na njia mbadala ya kumaliza changamoto hiyo kwa kuviagiza viwanda vinavyotengeneza mifuko kutengeneza inayoweza kubeba bidhaa, mathalan viazi vyenye uzito wa kilo 100 bila kushonea kilemba juu ambacho ndicho kinaitwa lumbesa.

Suala hili pia lisimamiwe na Wakala wa Vipimo nchini (Wima) ili kuhakikisha mkulima na mfanyabiashara wananufaika. Jambo hili litawasaidia wakulima na wafanyabiashara hususan tunapoelekea kwenye uchumi wa viwanda ambapo ili lengo litimie ni lazima Serikali iwekeze kwenye sekta ya kilimo na kuwasaidia wakulima.

Mbali na kuwanufaisha wakulima, pia halmashauri zitakuwa zinasanya mapato stahiki huku afya za wabebaji zikilindwa kwa kubeba uzito unaoeleweka.

Pamoja na changamoto zote hizo ni vyema Serikali ikazingatia upya utekelezaji wa sheria ya lumbesa ili kuondoa tofauti zilizopo kati ya wakulima na wafanyabiashara kila upande uweze kunufaika.

Ngollo John ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Mwanza