Shule za mwendokasi zipigwe marufuku

Haika Kimaro

Muktasari:

  • Changamoto hiyo inaathiri utoaji wa elimu kwa kiasi fulani ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia watoto morali ya kusoma hasa pale wanapokutana na vikwazo mbalimbali kama kupigwa na jua, kunyeshewa mvua au kudondokewa na wadudu pindi wanaposomea chini ya miti.

Wakati serikali ikijinadi na elimu bila malipo kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne, bado baadhi ya shule zinakabiliwa na changamoto mbalimbali kama uhaba wa madarasa, madawati na hata walimu, hali inayosababishwa na kusajili shule ambazo hazijakidhi vigezo.

Changamoto hiyo inaathiri utoaji wa elimu kwa kiasi fulani ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia watoto morali ya kusoma hasa pale wanapokutana na vikwazo mbalimbali kama kupigwa na jua, kunyeshewa mvua au kudondokewa na wadudu pindi wanaposomea chini ya miti.

Uhaba wa madarasa pia umesababisha baadhi ya shule darasa moja kukaliwa na wanafunzi zaidi na 100 na kusababisha walimu kukosa fursa ya kumfikia kila mwanafunzi na kumpa msaada wa kitaaluma.

Lakini kwa wale wanaosomea chini ya miti hufadhaishwa na watu wanaopita jirani na maeneo ya shule kutokana na mwonekano au haiba ya mtu huyo kwani hakuna kizuizi kinachomzuia mwanafunzi kumtazama.

Mateso hayo yote ninaweza kusema yamesababishwa na kusajiliwa kwa shule ambazo hazijakidhi vigezo vya Wizara ya Elimu kwa upande wa sekondari lakini pia zile shule za shule za msingi ambazo vibali vyake vinatolewa na Ofisi ya Rais, Tamisemi.

Nao uhaba wa walimu umekuwa changamoto kiasi kwamba hivi karibuni serikali ililazimika kuwahamisha walimu wa masomo ya sanaa kutoka katika shule za serikali na kuwapeleka shule za msingi ili kukabiliana na upungufu huo.

Lakini changamoto kubwa zaidi ni vyoo na maji kwa wanafunzi, hasa kwa watoto wa kike pale wanapokuwa katika hedhi na hivyo kusababisha wengine kukosa masomo.

Suala la maji hasa katika baadhi ya shule za msingi limekuwa halipewi kipaumbele kabisa na linapopewa kipaumbele kila mmoja anawaza maji hayo ni kwa ajili ya kunywa, kupikia uji na chakula, kumwagilia maua au kunyunyizia vumbi darasani.

Imefikia wakati unakutana na kibanda kilichojengwa kwa miti na kuezekwa nyasi na kuwekwa kipande cha ubao kinaitwa shule, halafu mbaya zaidi unakutana na kibao cha shule kimejengwa kwa tofali na kupakwa rangi za kupendeza.

Lakini si hayo tu kweli zipo shule zilizoanzishwa kisiasa kwa lengo la kuwasaidia wanasiasa fulani kupata kile wanachokihitaji, wakidai wameanzisha shule ili kuwaokoa watoto kusafiri umbali mrefu kusaka elimu.

Suala la kumwokoa mtoto kutembea umbali mrefu ni nzuri lakini suala la kumjengea mazingira mazuri na rafiki bora zaidi.

Kutokana na tabia hiyo, wapo watu ambao bado wanashikilia dhana ya kizamani kwa kisingizio kwamba wazee wetu walisomea chini ya miti na walifanya vizuri na kusahau ya kwamba kila siku dunia inabadilika na teknolojia inazidi kukua na watu kujikita zaidi katika teknolojia mpya.

Haina maana kwamba kuondokana na mifumo ya kizamani kutabadili utamaduni wetu, hapana bali kama tukitoa elimu iliyo bora vizazi vilivyopo na vijavyo vitaweza kunufaika na kulinufaisha Taifa na wao kuwa katika ushindani duniani.

Hivyo basi kama Taifa, hatuna budi kuhakikisha tunabadili mfumo wa utendaji kazi katika sekta ya elimu na watu kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuwaingiza watoto wetu katika hatari nyinginezo ikiwa ni pamoja na kupata bora elimu.

Pia, ni vyema kuhakikisha shule zote za sekondari hazisajiliwi kama hazina hosteli za wanafunzi ili kuwaepusha ni vikwazo vya kutembea umbali mrefu na kukutana na vishawishi wawapo katika safari ya kusaka elimu.

Utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo unapaswa kwenda sambamba na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Walimu wapate nyenzo na mazingira bora yatakayowaongezea ari ya kufundisha na kuongeza ufaulu badala ya kujikita kwenye kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kwenye shule za umma.

Ili hili lifanikiwe ni vyema sasa wadau wa elimu pamoja na wazazi wajitolee kuchangia gharama za elimu kwa kujenga miundombinu ya madarasa, vyoo, nyumba za walimu na maabara bila kusahau viwanja vya michezo badala kujibweteka wakidhania serikali itagharamia kila kitu.

Suala lingine muhimu ni uongozi wa shule kwa kushirikiana na kamati ya wazazi kuweka mazingira mazuri kufikia makubaliano ya hiari kwa pande zote itakayowahakikishia watoto kupata chakula cha mchana wakiwa shuleni, walau uji, na hii itaongeza ufaulu. Tuzitazame shule ambazo wazazi wanagharamia huduma ya chakula cha mchana kwa watoto wao wameweza kufanya vizuri.