Si Mbeya pekee, abiria wengi nchini washamba

Hivi karibuni niliandika katika gazeti hili kueleza abiria katika Mkoa wa Mbeya wanavyokataa tiketi kwenye mabasi ya kwenda wilayani na hata daladala kutokana na nilichokiita ‘ujanja wa kijinga’.

Nilifafanua kwamba ujanja wa kijinga kwa tafsiri nyepesi ni tabia ya mtu kuona mtazamo wake unafaa zaidi kuliko hata sheria za nchi ambazo zinamlinda yeye.

Ni tabia ya mtu kutaka kujiona kama ni mwelewa zaidi ya wengine na hivyo kutotaka hata kufuata taratibu au sheria zilizowekwa ama zilizopo.

Mara baada ya gazeti kusambazwa mitaani, wasomaji kutoka mikoa mbalimbali ikiwamo ya Tanga, Kilimanjaro, Singida na Ruvuma walipiga simu huku wengine wakituma ujumbe wakipongeza na kushauri polisi wa usalama barabarani na Sumatra kufanya operesheni maalumu kila mwezi kuwakamata abiria wasio na tiketi kwenye mabasi hayo.

Miongoni mwa walioandika ujumbe ni Mwalimu S. P Mushi wa Kilimanjaro, Abdallah Said Salim wa Tanga na Jumanne Khamis wa Sengerema ambao walisema wamejionea abiria wengi wasiotaka tiketi kutokana na ujanja wa kijinga.

Mushi alisema ujanja wa kijinga umejikita pia katika magari yanayosafiri kati ya Machame na Moshi mjini na kutaka vyombo vya dola vianze kuwakamata abiria wasiodai tiketi badala ya makondakta.

Naye Gwamaka Mwakatobe ambaye alijitambulisha kuwa ni mchambuzi wa masuala ya siasa, alipiga simu akipongeza na kushauri elimu izidi kutolewa kwa abiria ili wadai tiketi kila wanaposafiri.

Alisema abiria wenye tiketi wanaweza kunufaika na fidia za bima wanapoumia kwenye ajali na pia tiketi zinasaidia kutambuliwa kirahisi kwa majeruhi au wanaokufa inapotokea ajali .

Kwa ujumla, wasomaji wengi walisisitiza kwamba ujanja wa kijinga wa abiria wa kukataa tiketi uko sehemu mbalimbali nchini, huku wakisisitiza kwamba wasafiri wengi wanaingia kwenye mabasi na kusafiri bila kujua umuhimu wa tiketi.

Itakumbukwa kwambanilicholenga ni kueleza wazi umuhimu wa tiketi kwa abiria anayesafiri kwa mabasi ya aina zote, kwamba ni pamoja na kumsaidia abiria kupata fidia ya bima anapopata ajali na pia inamsadia kupata mizigo inayosahaulika ndani ya basi.

Inaelezwa pia kwamba kisheria kila abiria anatakiwa kupata tiketi ya basi alilopanda, lakini cha ajabu wasafiri wengi mjini Mbeya na wilaya zake wanadharau tiketi wakionyesha dhihaka kwa wanaozidai.

Ulitolewa mfano wa kituko cha abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Tukuyu wilayani Rungwe kwenda jijini Mbeya ambao walimshambulia kwa dhihaka abiria mwenzao aliyedai tiketi kwa kondakta wa basi kabla ya kutoa nauli ya Sh3,000.

Lakini watu waliosoma uchambuzi huo na kupiga simu walidokeza kero nyingine za abiria wanajojifanya wajanja kwamba wapo wanaopenda kujazana kwenye magari kama magunia, huku wakisaidia watu wajazane na kukubali kuchuchumaa au kubanana kama chane za ndizi.

“Abiria wengine wanajifanya makondakta kwa kuwapanga wenzao ndani ya mabasi huku wakikejeli kwa kutoa kauli chafu zikiwamo za , kama unataka kusafiri kwa raha nunua gari lako,” alisema Jailos Mwakilima kwa njia ya simu akiwa Iringa.

Bila shaka wakati umefika abiria lazima wajitambue na kudai haki kwa usalama wao katika safari.

Lazima wakubali kupokea tiketi. Abiria wasikubali kujazwa kwenye mabasi kupita kiasi na pia wasikubali kujazwa watu sita kwenye bajaji moja kama inavyofanyika katika Jiji la Mbeya.

Mchambuzi anapatikana kwa simu namba 0767-338897