Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Suluhu ya muda wa maongezi ulionunuliwa kimakosa

Matumizi ya huduma za mawasiliano kupitia simu za mkononi wakati mwingine huja na changamoto zake. Miongoni mwa hizo ni pale mteja anaponunua muda wa maongezi kimakosa, Jambo hili naamini bado linaweza kuongezewa mbinu bora za utatuzi.

Kununua muda wa maongezi kimakosa ni pale ambapo mtu ananunua kiasi cha muda wa maongezi (airtime) zaidi ya kile anachohitaji. Hii haihusiani na kununua kifurushi, au kufanya miamala ya pesa za mkononi kwa makosa, ambapo mtu anaweza kumtumia pesa mtu mwingine kimakosa.

Kwa mfano, inaweza kujitokeza pale ambapo mteja amekusudia kununua muda wa maongezi wa Sh5,000, lakini ghafla, la haula!, anashituka kugundua kuwa amenunua muda wa maongezi wa Sh50,000 badala yake.

Kwa uzoefu wangu, changamoto hii inaweza kuwakumba zaidi wateja wanaopendelea kununua muda wa maongezi kwa kuhamisha pesa aidha kutoka kwenye akaunti ya pesa mkononi, au kupitia benki mtandaoni kutoka akaunti ya benki. Ni ngumu kutokea kwa wanaonunua muda wa maongezi kwa mfumo wa vocha.

Kwa mfano, mteja anaweza kujikuta, badala ya kutuma pesa kama muamala (transaction) kwenye namba yake ya simu, amejitumia pesa hizo kama muda wa maongezi (airtime). Inaweza kuwa ni kukosa umakini, kujisahau, au pia, uelewa mdogo wa matumizi ya teknolojia, na mengineyo.

Kadhia hii inaibua changamoto mbalimbali, kwa namna tofauti;

Kwanza, muda wa maongezi hauwezi kutumika kwa matumizi mengine zaidi ya yale yaliyoanishwa na watoa huduma za simu. Kwa mfano, kwa kampuni za simu hapa nchini, ukiwa na kiasi cha muda wa maongezi, unaweza kununua vifurushi; dakika, bando za intaneti, au vifurushi vya kutuma ujumbe (SMS).

Ikiwa kimakosa mteja amenunua muda wa maongezi wa Sh50,000, hana njia ya kutumia muda huo zaidi ya hizo. Au mbadala wake, kwa jitihada binafsi, utafute mtu mwingine mwenye uhitaji wa “salio” umuuzie.

Pili, changamoto inaweza kuwa kubwa zaidi pale ambapo kiasi cha muda wa maongezi kilichonunuliwa kimakosa kinapokuwa kikubwa. Chukulia mfano, mteja amenunua “salio” la Sh1milioni, ni kweli zote atanunua data, au kifurushi cha dakika? au atafute wateja wa kuwauzia ili arudishe ela yake?. Si kazi rahisi!.

Kuna namna kadhaa kampuni zinaweza kufanya kutatua kadhia hiyo;

Kampuni ziweke huduma ya kurudisha au kubatilisha kiasi cha muda wa maongezi kilichonunuliwa kimakosa, hasa ikiwa ombi hilo litafanyika ndani ya muda mfupi, kwa mfano ndani ya saa 24 hadi 48.

Kiasi cha pesa kinaweza kurudishwa kwenye njia iliyotumika kulipia . Huduma hii inaweza kuwekwa kama chaguo kwenye menyu au kupitia njia nyingine ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wateja.

Njia hiyo itasaidia kwa namna mbili: kwanza, wale ambao hawataki kutumia kiasi cha ziada cha muda wa maongezi walichonunua kimakosa watakuwa na uwezo wa kurudisha fedha zao kirahisi. Pili, itaepusha mteja aliyekosea kugeuka kuwa muuza “vifurushi” ili kurudisha ela yake.

Vilevile, kampuni ziweke huduma inayoruhusu matumizi mengine mbadala ya muda wa maongezi. Kwa mfano, kwa sasa kwenye menyu, unaweza kutumia kiasi cha pesa kilichomo kwenye salio kuu kununua data, dakika, SMS, n.k.

Iongezeke chaguo jingine linaloruhusu kutumia salio kuu kulipia bili, manunuzi mtandaoni, na kadhalika. Hii itasaidia kuwapa wateja uhuru zaidi wa kutumia muda wao wa maongezi walionunua kimakosa. Endapo akiamua kutoomba kurudishiwa ela.

Kampuni ya Safaricom nchini Kenya inatoa huduma hiyo kupitia menyu inayowezesha mteja kurudisha muda wa maongezi alionunua kimakosa na kubadili kuwa pesa kwenye akaunti yake ya M-Pesa.

Hali kadhalika, kampuni ya MTN nchini Ghana inatoa huduma inayomwezesha mteja kuwauzia kampuni hiyo muda wa maongezi alionunua kimakosa, na fedha hizo kurudi kwenye akaunti yake ya pesa mkononi.

Mamlaka za usimamizi wa mawasiliano nchini zinaweza kufuatilia changamoto hii na nyinginezo kwa kina katika utoaji wa huduma za mawasiliano. Kufanya hivyo kutasaidia kuboresha huduma, kupata suluhu ya changamoto, na kulinda haki za watumiaji huduma za simu.