Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TAAMULI HURU: Nida iwe zaidi ya kitambulisho

Muonekano wa kitambulisho cha Nida. Picha na Mtandao



Kitambulisho cha Taifa kinazidi kuwa nyenzo muhimu katika maisha ya kila siku ya Mtanzania. Leo hii, karibu kila huduma muhimu ya Serikali na sekta binafsi inaanza na utambuzi wa mtu kupitia Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN), maarufu kama Jamii Namba. Hii ni hatua kubwa katika kujenga mfumo wa kisasa wa utambuzi wa wananchi na utoaji wa huduma.

Katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi aliipongeza Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kuboresha kwa kiwango kikubwa huduma zake.

Kwa sasa, mwombaji anaweza kupata Namba ya Utambulisho wa Taifa ndani ya siku moja, huku kitambulisho kikitolewa ndani ya takribani wiki moja. Kasi hii ni mafanikio yanayostahili pongezi.

Waziri Katambi alisisitiza kuwa Jamii Namba imekuwa msingi wa kupata huduma nyingi muhimu, kuanzia usajili wa huduma mbalimbali za Serikali, huduma za benki, afya, usafiri na shughuli nyingine za kiuchumi.

Aidha, alisema mfumo huu unaimarisha usalama wa taifa kwa kuwezesha kutambua kwa usahihi hadhi ya kila mtu, iwe ni raia, mwekezaji, mkimbizi au mgeni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, alisema mwitikio wa wananchi katika banda la NIDA kwenye maonesho ya Sabasaba umeonyesha uelewa unaoongezeka kuhusu umuhimu wa kitambulisho cha taifa.

 Kwa kuwa mifumo mingi ya Serikali sasa imeunganishwa na Jamii Namba, hivyo mtu mwenye kitambulisho cha NIDA hupata urahisi zaidi wa kuomba huduma mbalimbali bila kujaza taarifa zilezile mara kwa mara, kwa kuwa mfumo hutambua taarifa zake moja kwa moja.

Hakuna ubishi kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi ya utambulisho wa kidijitali. Hata hivyo, naamini wakati umefika wa kwenda hatua nyingine zaidi.

Katika nchi nyingi zilizoendelea, namba za utambulisho wa taifa, hazitumiki tu kuthibitisha utambulisho wa mtu, bali pia hujenga historia ya uaminifu inayomwezesha kupata huduma mbalimbali za kifedha kwa urahisi.

Ndiyo maana wananchi wao hutumia credit cards kwa kiwango kikubwa kuliko debit cards.

Tanzania inaweza kujifunza kutoka katika mifumo hiyo. Ni maoni yangu kuwa Serikali iangalie uwezekano wa kufanya marekebisho ya sheria, kanuni na taratibu ili kitambulisho cha taifa kiweze kutumika kama dhamana katika mazingira yanayoruhusiwa kisheria, hususan kwa makosa madogo yanayodhaminika kwenye vituo vya polisi na hata mahakamani.

Mtu mwenye kitambulisho halali cha taifa na ambaye taarifa zake zote zinapatikana kwenye mfumo wa Serikali, anaweza kuwa rahisi kufuatiliwa kuliko kutegemea wadhamini wa kawaida katika baadhi ya mazingira yanayoruhusiwa na sheria.

Vilevile, sekta ya benki inaweza kuanza kutengeneza mazingira yatakayowezesha matumizi mapana ya credit cards kwa kuzingatia historia ya mapato, uwezo wa kulipa na taarifa za utambulisho zinazotokana na Jamii Namba.

Hii itasaidia kuongeza upatikanaji wa mikopo midogo, kukuza matumizi ya huduma za kifedha na kuchochea shughuli za kiuchumi bila kuathiri usalama wa mfumo wa fedha.

Bila shaka, jambo hili halitahitaji kutegemea kitambulisho cha taifa pekee.

Litahitaji tathmini ya uwezo wa mkopaji, historia yake ya kifedha na mifumo madhubuti ya usimamizi wa mikopo. Hata hivyo, Jamii Namba inaweza kuwa msingi muhimu wa kujenga mfumo huo.

Hatua iliyofikiwa na NIDA inaonyesha kuwa Tanzania imejenga miundombinu imara ya utambuzi wa wananchi.

Mafanikio hayo yanaonekana pia kupitia ongezeko la wananchi wanaojitokeza kupata huduma katika banda la NIDA kwenye Maonesho ya Sabasaba, pamoja na mchango wa taasisi hiyo kwa Serikali kupitia gawio ililotoa.

Sasa ni wakati wa kujiuliza swali moja muhimu: Je, kitambulisho cha taifa kibaki kuwa nyenzo ya utambuzi pekee, au kiwe pia msingi wa kujenga mfumo wa kisasa wa dhamana, mikopo na huduma za kifedha kama ilivyo katika mataifa mengi yaliyoendelea?

Maoni yangu ni kwamba, kwa kuzingatia maboresho ya sheria, kanuni na mifumo ya usimamizi, Tanzania inaweza kufikia hatua hiyo.

Tukifanya hivyo, Jamii Namba haitakuwa tu kitambulisho cha utambulisho wa raia, bali itakuwa nyenzo ya kuongeza fursa za kiuchumi, kuimarisha uwajibikaji na kurahisisha maisha ya Watanzania.