TAHARIRI: Mauaji haya hayakubaliki, tuyapinge

Inatosha kuelezea mauaji ya Ally Mohamed Kibao kama njama za siri za makundi ya watu waovu na hatari. Tunapata nguvu kubwa ya kuelezea hivyo hasa pale tunapoitazama nadharia kuhusu njama maarufu Kiingereza: ‘Conspiracy theory’ Nadharia hii haitoshi tu kuelezea mauaji ya mjumbe huyo wa Sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pekee lakini inafaa hata kuelezea matukio yote ya utekaji, utesaji na mauaji yanayoendelea kulikumba Taifa letu.
Ukifuatilia simulizi ya namna mzee Kibao alivyotekwa Ijumaa ya Septemba 6,2024 saa 12:00 jioni baada ya kushushwa kwenye basi na kwenda kuuawa kikatili, haitofautiani sana na simulizi za watu waliotekwa na kupotezwa kwa muda mrefu sasa.
Simulizi za watu wengi ambao walitekwa na wengine kupotezwa, zinaeleza namna watekaji walivyojitambulisha kama askari wa Jeshi la Polisi, huku wakiwa na silaha. Japo hili halitoshi kulibebesha mzigo jeshi hilo kwamba, wanaotajwa ni askari wake.
Mbali na kuwa na silaha hizo lakini matukio mengine ya utekaji, wahusika wamekuwa wakitumia magari ambayo ni ghali. Ujasiri wa watu hao wasiojulikana, waliomteka mzee Kibao kwa kumshusha kutoka kwenye basi, haitofautiani sana na simulizi za namna wale watu 83 waliopo kwenye orodha ya Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).
Leo hii kuna familia hapa nchini zinalia kwa zaidi ya mwaka na wengine hata miaka saba sasa hawajui ndugu zao waliotekwa wako hai au wamekufa, wametekwa na akina nani na kwa sababu gani na wala hawajui upelelezi umefikia wapi.
Ibara ya 14 ya Katiba imetoa haki ya kuishi ikitambua kuwa uhai wa mwanadamu haununuliwi dukani na ukipotea umepotea, hivyo mtu yeyote anayeweza kuteka mwingine na kwenda kumuua ni mtu muovu na anastahili hatua kali za kisheria.
Ukiacha Katiba yetu, kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu RE 2022, kinasema wazi mtu yeyote ambaye, kwa dhamira ya uovu, anasababisha kifo cha mtu mwingine kwa kitendo kisicho halali ana hatia na anastahili adhabu ya kifo.
Nchi yoyote inayoongozwa kwa utawala wa sheria kama ilivyo Tanzania, kiuhalisia inapaswa pasiwepo mtu au taasisi ambayo iko juu ya sheria, na kwa Tanzania ni mahakama pekee inayoweza kusema huyu auawe, aachiwe au aende jela.
Mwezi Julai 2024, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camlius Wambura alisema polisi hawahusiki na utekaji wa watu au kupotea kwa watu kunakofanywa na watu wasiojulikana kwani kazi yao ni kulinda raia na mali zao.
Tunaikubali kabisa kauli hii, lakini nani hasa wanahusika na utekaji huu na jeshi lina mpango gani kutokomeza mauaji haya yasiyokubalika hapa nchini?
Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuagiza vyombo vya uchunguzi kumpelekea haraka taarifa ya tukio la mauaji ya Kibao na mengine ya aina hii.
Kauli hii inatia faraja kwa kuwa Rais Samia ni muumini wa haki sawa na asiyependa dhuluma kwa wananchi wake, lakini tunashauri kama itampendeza aunde tume ya kijaji ili kwenda kuchimbua mzizi na mikakati ya kukomesha matukio haya.
Kwa hali ilivyofikia, matukio haya yanatia doa amani ya nchi yetu hivyo, tunadhani uchunguzi huru utakuwa suluhisho.