TLS ifanyie kazi alichosema Jaji Mkuu kuhusu mawakili

Muktasari:

  • Hafla hiyo ilihudhuriwa na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Hamis Juma, Mwanasheria Mkuu, George Masaju na viongozi wengine waandamizi wakiwamo wale wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).

Mawakili 296 juzi waliapishwa katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Hamis Juma, Mwanasheria Mkuu, George Masaju na viongozi wengine waandamizi wakiwamo wale wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).

Awali ya yote tunawapongeza mawakili walioapishwa. Tunaamini wanakwenda kuwatumikia Watanzania wa kada mbalimbali ambao wamekuwa wakidhulumiwa kwa kutojua sheria au kushindwa kujitetea kwa namna yoyote ile.

Lakini pia tunaamini watakwenda kusimamia haki ili rasilimaliza za umma zisifujwe kwa namna yoyote ile iwe kwa mikataba au wizi wa kalamu.

Hata hivyo, wakati tukithamini na kutambua unyeti wa taaluma ya uwakili, kilichosemwa na Jaji Mkuu wakati wa kuapishwa kwa mawakili hao kimetushtua na kutufanya tuwakumbushe mawakili kuthamini unyeti wa taaluma yao ni ile aliyosema kwamba wapo baadhi yao ambao hawathamini jukumu kubwa na zito walilonalo hivyo kutozingatia maadili.

Jaji Mkuu alisema jumla ya malalamiko 25 yamefikishwa katika Kamati ya Mawakili na kufanyiwa kazi na tayari mawakili wawili wamekutwa na hatia.

Kilichotushangaza zaidi ni aina ya malalamiko wanayohusishwa nayo mawakili hao ikiwamo rushwa, kuchukua fedha za wateja wanaposhinda mashauri yao, kutoa siri za wateja wao, kukosa umakini na kushindwa kuendesha kesi, kuchukua kesi ambayo mteja hajatoa ruhusa pamoja na kuandika mkataba zaidi ya mmoja.

Inapofikia hatua kwa wakili kuandika mkataba zaidi ya mmoja maana yake ni kwamba wakili huyo hasimami kama mtetezi, bali anashiriki kudhulumu na kusababisha matatizo zaidi, wakili wa aina hii na wengine wanaoghushi, wanaotoa siri za wateja na kukiuka maadili yao kwa ujumla, hawafai.

Kwa mantiki hiyo, ni jukumu la TLS kuhakikisha inayafanyia kazi yote yaliyosemwa na Jaji Mkuu kwa lengo la kulinda unyeti wa taaluma yao ambayo malalamiko ya aina hii yanatoa ishara mbaya kwamba inaelekea kuporomoka kimaadili.

Tunaamini kwamba TLS inayafahamu malalamiko haya na pengine inawajua mawakili au wanachama wake wanaokiuka maadili hivyo ni jukumu lake kusimama imara kuhakikisha inaondokana na watu wa aina hiyo kwani mbali na kuitia doa taaluma yao, lakini pia wanasababisha mateso kwa wananchi wasio na hatia.

Tunaamini ni jukumu la TLS kuhakikisha taaluma ya sheria ambayo tunaamini ni nyeti, inalindwa kwa nguvu zote lakini pia mwananchi wa kawaida anaepushwa na matatizo yanayotokana na aina ya mawakili wala rushwa na wenye tabia ya kughushi na hata kuchukua fedha za wateja wao wanaposhinda mashauri.

TLS isiruhusu taaluma ya uwakili ichezewe na watu wachache, isiruhusu ifike wakati mwananchi wa kawaida akapoteza imani na mawakili. Tunataka waendelee kuamini kwamba wakili ni mtu muhimu wa kumpa msaada wa kisheria hivyo hana sababu ya kujiuliza mara mbilimbili kama atapata msaada wa kwake au atatapeliwa.

Yumkini malalamiko yaliyotajwa na Jaji Mkuu ni machache huenda yapo ambayo hayajafikishwa kwenye Kamati ya Mawakili. Tunaamini kwamba TLS ina uwezo wa kukabiliana nayo.