Tost iwe neema kwa wenye malalamiko ya kodi
Desemba 11, mwaka huu, Serikali ilitangaza kuanzishwa kwa Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na taarifa za Kodi Tanzania (TOST).
Kuanzishwa kwake, kama ilivyoelezwa na Mkurugenzi wake, Robert Manyama kumelenga kurahisisha utatuzi wa migogoro baina ya Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) na walipakodi.
Itakumbuka kabla ya uwepo wa taasisi hiyo, utaratibu uliokuwepo kwa ajili ya uratibu wa malalamiko ya kodi ni kupitia Bodi ya Mahakama ya Rufaa ya Kodi (TRAB) na Baraza la Rufani za Kodi (TRAT).
Ili kuwasilisha malalamiko kupitia majukwaa ya TRAB na TRAT, mlalamikaji alipaswa kuwa na uwakilishi wa mwanasheria atakayesimama badala yake.
Lakini, haikuwa bure kuwasilisha lalamiko, ulipaswa kugharimika, si tu ada ya wakili, bali hata ya kufungua jalada la malalamiko.
Si hivyo tu, utendaji wa TRAB na TRAT ulifanyika kwa sura ya kimahakama, hivyo migogoro ilimalizwa kwa utaratibu huo na si kwa njia ya usuluhishi.
Utaratibu mwingine uliokuwepo kabla ya TOST ni kukata rufaa kwa Kamishna wa TRA kwa ajili ya mazungumzo, iwapo umefanyiwa makadirio ya kodi unayoona hayalingani na uhalisia wa mauzo yako.
Huu ndiyo utaratibu uliokuwa unalalamikiwa zaidi na wafanyabiashara, wengine wakitilia shaka maamuzi yatakayotokewa kwa kuwa unakokwenda kulalamika ndiko mzizi wa lalamiko lako ulipo.
Kwa tafsiri rahisi, mashaka ya walipakodi yalitokana na hoja kwamba inawezekanaje Kamishna wa TRA ndiye awe msikilizaji wa malalamiko yanayoihusu TRA na mlipakodi badala ya kutafutwa chombo huru.
Kwa hiyo, hakukuwa na imani juu ya maamuzi yatakayotolewa, kwa sababu anayesikiliza lalamiko ndiye anayelalamikiwa, angewezaje kujinyima haki.
Malalamiko mengine dhidi ya utaratibu huo, ni gharama kabla ya kuanza kusikilizwa hayo malalamiko.
Kulingana na utaratibu huo, ili lalamiko lianze kusikilizwa kwa Kamishna wa TRA, mlalamikaji unapaswa uwe umelipa theluthi moja ya kodi uliyokadiriwa.
Malalamiko katika eneo hili, yaliibuliwa kwa hoja kwamba, inawezekanaje uanze kulipa faini katika kesi uliyoikatia rufaa.
Maana yake hata ukishinda rufaa hakutakuwa na tija kwa kuwa tayari umeshatekeleza hukumu.
Kwa sababu hizo, ndiyo maana Serikali imekuja na jukwaa huru litakaloshughulikia malalamiko ya kikodi kwa njia huru.
Tofauti ya TOST na majukwaa mengine yaliyopo ni kwamba, mlalamikaji hatapaswa kuwa na mwanasheria kwa ajili ya kumwakilisha katika uwasilishaji na msikilizaji wa lalamiko.
Hata hivyo, taasisi hiyo inashughulikia malalamiko hayo bila gharama yoyote kwa mlalamikaji.
Kadhalika, usuluhishi wake unafanyika nje ya utaratibu wa kimahakama, hivyo ni suluhu ya majadiliano baina ya mlalamikaji na mlalamikiwa.
Kwa msingi huo, taasisi hiyo itatoa jawabu la malalamiko lukuki ya walipakodi dhidi ya mamlaka zinazosimamia sheria za kodi nchini.
Hili ni jukwaa sahihi kwa walipakodi kuwasilisha malalamiko yao, hata hivyo kuna haja ule uhuru linalotajwa kuwa nao, uwepo ili litekeleze wajibu huo kukidhi haja za walipakodi.
Kwa mtazamo wangu, TOST haipaswi kuwa mshirika wa Serikali bali ijikite katika uhuru ili iwe na tija tarajiwa.
Nafahamu ipo chini ya Wizara ya Fedha, lakini kwa kuwa imeanzishwa na kupewa jukumu la kusuluhisha migogoro ya kikodi, isikwepe misingi ya kuanzishwa kwake.
Kwa kuwa ndiyo inayoonekana tumaini la walipakodi, utendaji wake ujikite katika haki, uhuru na weledi badala ya aibu na woga.
Nakiri uwepo wake, utakuwa na tija lakini napata mashaka kwenye maeneo kadhaa ambayo taasisi hiyo inapaswa kuandaa majibu yake mapema.
Kwa kuwa utendaji wake hautakuwa wa kimahakama, maana yake utekelezwaji wa maamuzi yake utabaki kuwa hiari ya anayetakiwa kutekeleza.
TOST inapaswa ipewe nguvu ya kushinikiza utekelezwaji wa maamuzi yake ili walipakodi waongeze imani zaidi.
Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) itumike zaidi katika upokeaji, uratibu na usikilizwaji wa malalamiko, ili kuwarahisishia walalamikaji wa maeneo mbalimbali.
Kwa kuwa ndiyo kwanza TOST inaanza, bila shaka haitakuwa na ofisi katika kila Mkoa, hivyo mlalamikaji kutoka eneo lolote awe na fursa ya kuwasikisha lalamiko lake kwa njia ya mtandao