Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tuchopeke elimu ya afya ya akili kwenye mtalaa

Muktasari:

  • Kwa muda mrefu, jamii nyingi zimekuwa zikilizingatia suala la afya ya akili kwa mtazamo wa aibu au kutojali, hasa linapohusiana na watoto.

Dar es Salaam. Katika mazingira ya sasa ya kijamii na kiuchumi yenye changamoto nyingi, elimu ya afya ya akili kwa watoto imekuwa suala lisiloweza kupuuzwa tena. 

Kwa muda mrefu, jamii nyingi zimekuwa zikilizingatia suala la afya ya akili kwa mtazamo wa aibu au kutojali, hasa linapohusiana na watoto.

 Hali hii imechangia watoto wengi kukua wakiwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu hisia zao, namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo, au kujenga uwezo wa kuhimili hali ngumu za maisha. .

Ni wazi kwamba bila afya nzuri ya akili, mtoto hawezi kujifunza kwa ufanisi, kujenga uhusiano wenye maana, wala kuwa na mchango bora katika jamii.

Afya ya akili kwa watoto ni zaidi ya kutokuwepo kwa ugonjwa. Ni hali ya ustawi wa kiakili, kihisia na kijamii inayomwezesha mtoto kufikiri vizuri, kujifunza, kushughulikia hisia na kujenga uhusiano wa afya.

Mtoto mwenye afya bora ya akili anaweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za shule, kucheza, na kujifunza bila vikwazo vya kihisia au kisaikolojia. Kinyume chake, mtoto mwenye changamoto za afya ya akili anaweza kuonesha tabia kama kushuka kwa ari ya kusoma, kujitenga, hasira za mara kwa mara, au hata kushindwa kuelewa masomo.


Utafiti mwingi unaonesha kuwa asilimia kubwa ya matatizo ya afya ya akili huanza kabla ya umri wa miaka 14. Lakini kutokana na ukosefu wa elimu sahihi na mwamko wa kijamii, dalili hizo mara nyingi hazitambuliwi mapema.

Watoto wengi hukumbwa na matatizo kama mfadhaiko, wasiwasi  na msongo wa mawazo, lakini hawapati msaada wa kitaalamu. Bila msaada wa mapema, hali hizi huweza kuathiri ukuaji wao wa kiakili, kitaaluma, na kijamii kwa muda mrefu.

Kwa mantiki hiyo, shule zinapaswa kuwa sehemu ya kwanza ya kuweka misingi ya elimu ya afya ya akili.

Afya ya akili shuleni

Kwa kuwa watoto hutumia muda mwingi shuleni, walimu wana nafasi kubwa ya kusaidia kujenga uelewa wa hisia, kujitambua, na kuwasaidia watoto kujifunza stadi za maisha ambazo zitawasaidia kushughulikia changamoto mbalimbali.

Hii inawezekana iwapo elimu ya afya ya akili itaingizwa rasmi kwenye mitalaa ya shule kuanzia ngazi ya awali.

Kuanzishwa kwa elimu ya afya ya akili katika shule hakumaanishi lazima kuwe na somo jipya pekee, bali kunaweza kufanyika kwa njia shirikishi na bunifu.

Shule zinaweza kuanzisha vipindi maalum vya kukuza uelewa wa kihisia, stadi za kuwasiliana, kudhibiti hasira, kujenga kujiamini na huruma kwa wengine. 

Mafunzo haya yanaweza kufanyika kupitia mbinu mbalimbali kama mazungumzo ya darasani, michezo ya kuigiza, sanaa ya uchoraji au uandishi wa hisia binafsi.

Pia, elimu hii inaweza kuingizwa katika masomo yaliyopo tayari kama  dini au maarifa ya jamii. Kwa mfano, wanafunzi wanaweza kufundishwa mbinu za kutatua migogoro bila vurugu, namna ya kushirikiana, au kujua wapi pa kutafuta msaada wanapohisi huzuni au msongo wa mawazo.

 Hili litawezesha watoto kuona kwamba kuzungumzia hisia ni jambo la kawaida na la muhimu, si udhaifu kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.

Lakini mafanikio ya mpango huu hayawezi kupatikana bila kuwajengea uwezo walimu na watendaji wa shule. Walimu wanapaswa kufundishwa kutambua ishara za awali za matatizo ya afya ya akili kwa watoto.

 Mara nyingi mtoto mwenye msongo wa mawazo au huzuni ya muda mrefu, huonekana na walimu kama mvivu au mkaidi, jambo linalosababisha kushindwa kupata msaada unaofaa.

Mafunzo ya kitaalamu yatawasaidia walimu kuwa na uelewa mpana wa saikolojia ya mtoto, na kuwa sehemu ya suluhisho badala ya kuwa chanzo cha shinikizo zaidi.

Zaidi ya shule, wazazi na walezi nao wana jukumu kubwa. Familia ni sehemu ya kwanza ya malezi na ustawi wa mtoto. Kupitia ushirikiano wa karibu kati ya shule na wazazi, elimu ya afya ya akili inaweza kuenea nyumbani. 

Wazazi wafundishwe namna ya kusikiliza watoto, kuwasaidia kueleza hisia zao, na kuwapa msaada wa kihisia. Jamii zetu bado zina changamoto ya kukubali kwamba mtoto anaweza kuwa na matatizo ya kiakili, hali ambayo husababisha watoto kuonewa au kutengwa badala ya kusaidiwa.

Sera muhimu

Ni muhimu pia kuwepo na sera za elimu zinazotambua na kuunga mkono umuhimu wa elimu ya afya ya akili. Wizara ya Elimu, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, zinaweza kuandaa miongozo ya kufundisha stadi za maisha shuleni, kutoa miongozo ya rasilimali za kufundishia, na kuweka mfumo wa upimaji wa hali ya afya ya akili ya watoto kila baada ya kipindi fulani

Aidha, shule ziwekwe katika nafasi ya kuwa na washauri nasaha waliofunzwa ambao watafanya kazi ya kusaidia watoto wanaopitia changamoto za kihisia au kisaikolojia.

Kuweka elimu ya afya ya akili katika mitalaa ya shule ni kuwekeza katika mustakabali wa jamii yenye ustawi. Tunapoandaa watoto kujitambua, kujieleza, na kusaidiana kwa misingi ya kihisia na kijamii, tunawapa silaha muhimu za maisha ambazo zitawasaidia hata baada ya shule. 

Dunia ya sasa inahitaji zaidi ya ujuzi wa kitaaluma; inahitaji watu wenye akili timamu, uthabiti wa kihisia, na uwezo wa kuhimili presha za maisha.

Elimu ya afya ya akili ni msingi wa mafanikio ya watoto  si tu kwa kushinda mitihani, bali kwa kuwa watu wenye furaha, uelewa, na uwezo wa kubadilisha jamii kwa njia chanya. 

Ni wajibu wetu kama wazazi, walimu, watunga sera na wanajamii kuhakikisha elimu hii inaanzia mapema, shuleni na kwa upana unaostahili.