Tudhibiti vyakula aina hii shuleni
Tembelea shule yoyote ya msingi au sekondari iwe mjini au kijijini. Aghalabu hutokosa kukuta vibanda vimezunguka shule. Humo huuzwa kila aina ya vyakula.
Hata hivyo, vilivyo maarufu zaidi zaidi ni viazi vya kukaanga maarufu kama chips, soda, juisi za viwandani, keki, biskuti, pizza, mihogo ya kukaanga, maembe mabichi, ice cream, ubuyu, koni, bazoka, karanga na vitu vingine vingi ambavyo hujulikana kama vyakula vya haraka au Kiingereza ‘Junk foods’.
Ni vyakula vinavyokosolewa kwa kutokuwa na virutubisho muhimu kwa lishe ya binadamu. Na kibaya zaidi vinatajwa kuchangia katika matatizo ya kiafya kwa binadamu.
Ukiondoa matatizo ya kiafya, ulaji wa vyakula visivyofaa una athari hata katika maendeleo ya taaluma. Utafiti wa lishe shuleni kwa watoto na vijana wa miaka mitano hadi 19, umebaini asilimia 50 hushindwa kuwa makini kufuatilia masomo wakati wa asubuhi kwa sababu ya kukosa ulaji unaofaa.
Utafiti huo uliofanywa mwaka 2022 huko Zanzibar, pia umebaini asilimia 76 ya maduka yanayozunguka mazingira ya shule yanauza vyakula visivyo na ubora kiafya zikiwemo juisi, barafu, sukari na pipi, vyakula vinavyotajwa kuchochea ulaji usiofaa na kutengeneza sumu mwilini.
Wataalamu wa afya, lishe wanaonya kuwa vyakula aina hiyo vimekuwa kichocheo cha magonjwa kama vile kisukari, kiharusi, shinikizo la juu, unene uliopitiliza, vidonda vya tumbo, magojwa ya moyo na mishipa na mengineyo ambayo kwa sasa yanawatesa watu wengi kila kona ya dunia.
Kwa kuwa vyakula vingi ni vile vyenye wingi wa asidi kama chips na mihogo yenye kachumbari, chumvi na pilipili, lazima tuwazuie wanafunzi kwa kuwa wanajiweka katika mazingira ya kupata magonjwa kama tukiyotaja hapo awali.
Februari 2020, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa angalizo la namna watoto katika nchi mbalimbali duniani walivyo kwenye hatari ya kudhurika kutokana na matangazo ya ulaji wa vyakula vya haraka.
Ifike hatua sasa mamlaka husika zione kuwa vyakula hivi ni sawa na janga kwa watoto na Taifa kwa ujumla.
Udhibiti wa nini wanafunzi wanapaswa kula, hauna budi kuzingatiwa, vinginevyo tunaandaa Taifa la wagonjwa ambao watakuja kuathiri nguvu kazi ya ya Taifa.
Hili lituzindue ili sasa ule mpango wa lishe shuleni utiliwe maanani zaidi, kwa shule zote vijijini na mijini kuwa na utaratibu wa kutoa vyakula kwa wanafunzi. Na kisiwe tu chakula bali uwe mlo bora.
Linaposhindikana hilo, basi hawahawa wauzaji wa vyakula binafsi wadhibitiwe. Walimu wakuu na kamati za shule kwa kushirikiana na maofisa afya ngazi ya mitaa, vijiji na kata, wawe na utaratibu wa kuwasimamia wauzaji wa vyakula shuleni kwa kuwa na orodha yao, anuani na namna wanayopika.
Hilo litasaidia hata siku kukitokea tatizo iwe rahisi kujua wanafunzi walikula kwa nani na chakula gani. Tofauti na sasa ambapo uongozi wa shule unachojua ni kugawa mabanda na kuchukua kodi, huku kila muuzaji akijitengenezea chakula pasipo usimamizi.
Kwa baadhi ya shule, tunatambua kuwapo kwa programu za utoaji wa vyakula, hata hivyo bado uuzwaji wa ‘junk foods’ umekuwa ukiendelea shuleni.
Kwa hakika kama jamii tunapaswa kutupia jicho vyakula hivi, ambavyo athari yake inaweza isionekane sasa, lakini ikaja kuwatesa watoto miaka ijayo na hivyo kuathiri nguvu kazi ya Taifa.