Tuhakikishe shule zinakuwa mahala salama
Septemba 30 katika gazeti la Mwananchi ilichapishwa taarifa iliyobebwa na kichwa cha habari ‘Shule zageuzwa gesti bubu’.
Habari hiyo ni matokeo ya uchunguzi uliofanywa katika shule kadhaa ndani ya jiji la Dar es Salaam na kubaini mazingira yake si salama kwa watoto.
Kulingana na habari hiyo shule hizo hazina uzio, madirisha, milango, ulinzi hivyo kufanya mtu yeyote anaweza kuingia wakati wowote na kuathiri usalama wa wanafunzi.
Kwangu naona haliishii hapo, kwa mazingira hayo ni rahisi sana kwa watoto kujifunza mambo ya ovyo au hata kutozingatia kile kinachofundishwa darasani.
Nafahamu katika hili wengi tutainyooshea kidole Serikali kwanini inashindwa kusimamia shule na kuhakikisha zina mazingira mazuri na salama kwa wanafunzi. Hata kama shule sio za Serikali bado ina dhamana ya kuhakikisha usalama wa wanafunzi.
Mwongozo unaelekeza kabisa ili shule ianze kupokea wanafunzi inapaswa kuwa na miundombinu ya aina gani kuhakikisha usalama wa watoto, hapa ndipo Serikali inapaswa kuwajibika kwanini mambo yanakwenda ndivyo sivyo hali.
Baada ya kuinyooshea kidole Serikali hebu turudi kwetu sisi wazazi na wanajamii kwa ujumla tujiulize tumefanya nini kunusuru hali hiyo. Ninachoamini yakitokea madhara tutakaoumia ni sisi na si hiyo Serikali ambayo tunaamini inabeba mzigo mkubwa.
Najiuliza hivi inawezekana vipi kwa shule iliyo katika Jiji la Dar es Salaam inakosa taa kiasi kwamba watu wasio na nia njema wanatumia mwanya huo wa giza kuingia na kufanya vitu vya hovyo kama ambavyo imeelezwa kwenye habari hiyo.
Shule ambayo ipo ndani ya jiji linaloongoza kwa shughuli za kibiashara inakosaje milango, madirisha au hata mlinzi anayelinda usalama wa watoto na vifaa vinavyopatikana hapo shuleni. Huu ni uzembe wa hali ya juu na kwa tafsiri nyingine ni kwamba jamii imeshindwa kuwajibika.
Kwa ninavyofahamu kila shule ya msingi ina kamati na shule za sekondari zina bodi ambazo zinafanya kazi kwa ukaribu na uongozi wa shule, wazazi na Serikali.
Kupitia kamati hizi ni rahisi kuonesha changamoto ilipo na ikafanyiwa kazi kulingana na uzito wake kwa kuwashirikisha wazazi au hata jamii kwa ujumla ya eneo husika ambapo shule ipo.
Sasa najiuliza kamati za shule zinafanya nini kuhakikisha zinatatua changamoto zinazohatarisha usalama wa wanafunzi katika shule wanazozisimamia.
Nikitolea mfano taa, ni ajabu kusikia kwamba shule ina umeme lakini inakuwa giza kwa sababu hakuna taa. Haya ni mambo ya ajabu na ninarudi kule kule jamii imeshindwa kuwajibika.
Hebu jiulize wewe mzazi unaweza kuruhusu nyumbani kwako kukae giza kwa sababu taa imeungua au kwa sababu yoyote ile hakuna taa?
Jibu ni hapana utapambana kwa kadri ya uwezo wako kuhakikisha kunawaka, sasa kama hivyo ndivyo kwanini tunashindwa kuunganisha nguvu kuwezesha taa kupatikana katika shule wanazosoma watoto wetu.
Mtu ukiwambia hivi atasema shule ni ya Serikali sasa hebu jiulize hiyo Serikali inasimamia shule ngapi na inafanya vitu vingapi hadi ikumbuke kwamba shule yenu haina taa.
Unakuta wazazi wanavutana kulipa mshahara wa mlinzi matokeo yake shule inabaki bila ulinzi, hapo sasa ndio utasikia watu wanaingia usiku na kugeuza gesti bubu.
Kuna mambo mengine wanajamii tunapaswa kuwajibika na wala tusiumizwe na uwajibikaji huo kwa sababu ni sisi ndio tutakopata matunda au maumivu yake. Kama hatutaimairisha ulinzi na usalama katika wa shule watakaokuwa shakani ni watoto wetu na sio Serikali.
Kutokana na uhalisia huo hatuna budi kuwa na mipango madhubuti ya kuhakikisha watoto wetu wanasoma katika mazingira yenye usalama. Mazingira ya kujifunzia yanapokuwa mazuri yana mchango mkubwa katika kiwango cha taaluma na kinyume chake ni hatari.
Wito wangu kwa wazazi tusione uchungu kuchangia vitu ambavyo viko ndani ya uwezo wetu, kama unaumia kutoa fedha basi peleka taa shuleni.
Mkiona kulipa mshahara wa mlinzi ni gharama basi jipangieni zamu za kwenda kulinda shuleni ili kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa wakati wote watoto wasome katika mazingira mazuri.
Katika hili viongozi wa mitaa na vijiji nao wanapaswa kuwajibika kuhakikisha shule zilizo kwenye maeneo yao ziko salama.
Kusubiri Serikali kuu ilete taa, illipe mlinzi, ijenge ukuta inaweza kuchukua muda mrefu lakini hayo yote yanaweza kufanywa na wazazi na wanajamii wa eneo husika.
Elizabeth Edward ni mwandishi mwandamizi wa Mwananchi.