Tusione soni kufanya haya utekaji raia
Leo hii tungeweza kumleta Mtume Muhammad SAW au Yesu Kristu na kuwauliza wana maoni gani juu ya kutekwa, kupotezwa na kuuawa kwa raia wasio na hatia Tanzania, ninaamini wangesema yanatia hofu, yanaumiza na hayakubaliki.
Ni mtizamo huohuo ndio ambao wamekuwa nao viongozi mbalimbali wa dini hapa nchini, wanaharakati, wanasiasa, wasomi na wananchi wa kawaida, ukiacha wale wachache wanaogeuza matukio hayo kuwa propaganda za kisiasa.
Mimi ningepata nafasi ya kukutana na Rais wangu, Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, ningemuomba afanye mambo matatu makubwa, ili kuiweka kando serikali yake na shutuma kuwa ina mkono katika matukio haya.
Kwa aina ya utekaji wa watu ambao hadi sasa hawajulikani walipo, ama kwa sababu za kisiasa au kihalifu, hakuna mtu ataacha kulinyooshea kidole Jeshi la Polisi kutokana na staili ya utekaji, magari wanayotumia na silaha wanazotumia.
Kama Polisi wanasema Jeshi la Polisi halihusiki na matukio hayo kama Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camilius Wambura alivyopata kusema, basi wangetuambia ni nani wanaofanya matukio kwa sababu wao ndio mabingwa wa intelijensia.
Lakini ili kujisafisha, basi IGP angetupa ufafanuzi walau wa kurasa moja kuhusu nini kinaendelea juu ya uchunguzi wa waliomteka Edgar Mwakalebela au Sativa, madai yake ya kuwekwa Polisi Oysterbay na kumtambua mmoja wa watekaji.
IGP mwenyewe au kupitia kwa msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, angetoa taarifa hata ya kurasa moja juu ya hatua ya uchunguzi wa kutekwa mbele za abiria wenzake, kiongozi wa Chadema, Ally Mohamed Kibao na kisha kuuawa.
Ninasema hivyo kwa sababu matukio hayo mawili ni kama pacha, kwani Sativa anasema waliomteka walikuwa na magari ya ‘ghali’ kama Toyota V8 au Prado, walikuwa na silaha nzito na walikuwa na pingu zilizozoeleka kwa askari Polisi.
Lakini angeeleza walau ukurasa mmoja, nini kinaendelea katika utekwaji na kupotezwa kwa Deusdedit Soka na wenzake wawili na raia wengine zaidi ya 80 waliotajwa na TLS, kukaa kimya maana yake wanakubali kinachosemwa ni kweli.
Ukimya wao, unamfanya Rais Samia na askari wengine wa Jeshi la Polisi kubebeshwa mzigo wa lawama wakati ukimwangalia Rais anavyoongea, unaona kabisa anachukizwa na matendo hayo yanayochafua taswira ya Tanzania.
Bahati mbaya sana na wala simlaumu, Rais katika hotuba yake mbele ya makamanda wa Jeshi la Polisi mjini Moshi, alionyesha ukali kana kwamba kuna kitu alielezwa kabla ya kupanda jukwaani, ambacho sisi raia hatukifahamu.
Katikati ya mtanziko huu, ningetamani Rais aunde Tume ya Kijaji kama alivyofanya Rais Benjamin Mkapa mwaka 1996 alipouawa Mkurugenzi wa zamani wa Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe iliyokuwa chini ya Jaji Damian Lubuva.
Ingawa taarifa ya Tume hiyo imekuwa siri hadi leo, lakini ilituliza joto na hasira za Watanzania, kwani waliona askari sita wa Jeshi la Polisi na raia mmoja wakifikishwa kortini kujibu tuhuma za mauaji hayo na wawili wakahukumiwa adhabu ya kifo.
Mbali na Mkapa, mwaka 2006, Rais Jakaya Kikwete aliunda Tume chini ya Jaji Mussa Kipenka, kuchunguza mauaji ya wafanyabiashara wa madini na dereva taxi na matokeo yake ni kushitakiwa maofisa kadhaa wa Jeshi la Polisi.
Hii ilisaidia kuondoa ile nadharia iliyojengeka kwa wananchi, kama ilivyojengeka sasa, kwamba kesi ya nyani huwezi kumpelekea tumbili, ikimaanisha kesi inayowahusu polisi inapaswa kuchunguzwa na chombo huru cha haki jinai.
Lakini Rais asione soni au haya kuwaalika wachunguzi wa kimataifa na si lazima wawe Scotland Yard ambao wamependekezwa na Chadema, ingawa walishakuja kuchunguza matukio mawili hapa nchini kwetu.
Nasema hivyo kwa sababu mwaka 1984 jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) lilipoungua, Serikali iliwaalika Scotland Yard ambacho ni kitengo mahsusi cha Jeshi la Polisi la Uingereza kilichobobea katika ‘forensic’ kuja kuchunguza tukio hilo
Mwaka 1994 kulipotokea tukio baya la moto shule ya sekondari ya wasichana ya Shauritanga huko wilaya ya Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro na kuua wanafunzi wa kike 43, Rais Ali Hassan Mwinyi (marehemu) aliwaalika Scotland Yard.
Walipoalikwa si kwamba hawakuwa wanaviamini vyombo vyetu vya uchunguzi, walitaka kujenga imani ya wananchi.
Lakini ili kuwaondoa polisi kujichunguza, Rais na serikali yake watunge sheria ya chombo huru cha kuchunguza matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanayofanywa na Polisi, kama ilivyo IPOA ya Kenya au IPID ya Afrika Kusini.