Tuwe makini kuepuka mgawo wa maji

Wananchi katika baadhi ya maeneo kadhaa nchini wanakabiliwa na uhaba wa maji, huku wengine wakilalamika kutofuatwa ratiba kwa yale yenye mgawo wa huduma hiyo.

Upungufu wa maji unaelezwa na baadhi ya mameneja wa mamlaka za maji kwenye baadhi ya maeneo, kwamba unasababishwa na tatizo la kukatika umeme, huku miradi inayoendelea na sehemu zinazotumia mitambo ya umeme jua, ikidaiwa kukosa mwanga wa kutosha wa jua.

Haya yanatokea wakati ambao tayari kuna mgawo wa umeme uliopewa jina la ratiba ya umeme nchini, ambao unawaathiri wananchi majumbani, sehemu za biashara na kazini.

Haikubaliki kuona wananchi wanakosa huduma ya uhakika ya majisafi na salama licha ya Taifa kujaaliwa rasilimali nyingi ya maji, ikiwamo mito inayotiririsha maji kipindi chote cha mwaka, maziwa makubwa kama Victoria, Nyasa na Tanganyika pamoja na mvua zinazonyesha mara mbili kwa mwaka katika maeneo mengi ya nchi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Maji, rasilimali ya maji juu ya ardhi inakadiriwa kuwa na mita za ujazo bilioni 105, wakati iliyopo ardhini ni mita za ujazo bilioni 21 na mahitaji ya maji kwa matumizi mbalimbali nchini kufikia Aprili 2022, yalikadiriwa kuwa ni mita za ujazo bilioni 47 kwa mwaka, sawa na asilimia 37.37 ya maji yaliyopo nchini.

Hivyo kwa hesabu ya kawaida zaidi ya asilimia 62 ya rasilimali maji iliyopo nchini haijatumika.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiwasilisha bungeni hotuba ya bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2023/24 alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira inawafikia zaidi ya asilimia 95 ya wakazi wote wa maeneo ya mijini ifikapo mwaka 2025.

Alisema katika mwaka wa fedha 2022/23, jumla ya miradi 175 ilipangwa kutekelezwa ambayo hadi Aprili 2023; 40 ilikuwa imekamilika na 135 ikiwa kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.

Miradi hii ama imetekelezwa au inatekelezwa katika miji mikuu ya mikoa, miji mikuu ya wilaya, miji midogo, na pia ipo ya kitaifa.

Kwa hali ilivyo ya upatikanaji wa maji hivi sasa, itakuwa vigumu kuufikia mpango huo wa Serikali ndani ya miaka miwili ijayo, iwapo mikakati iliyopo haitapata usimamizi na ufuatiliaji wa kina na zaidi kuwezesha wananchi kupata rasilimali hii muhimu.

Hili haliwezi kutekelezwa na Serikali pekee, kuna haja ya kushirikiana kwa karibu na wadau wa maendeleo katika kujenga, kukarabati na kupanua miundombinu ya majisafi, ikiwa ni pamoja na kuzijengea uwezo Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini.

Kuna haja ya kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na upungufu uliopo kwa kuhakikisha kunakuwa na uhifadhi wa vyanzo vya maji, kuchimba visima virefu na mabwawa, kuvuna maji ya mvua na matumizi ya teknolojia rahisi zilizopo.

Kuendelea kutumia teknolojia zenye gharama kubwa za kupata maji, ukiwamo umeme wa vyanzo aghali, kutaendelea kuathiri upatikanaji wa maji, ikizingatiwa kuwa nishati hiyo bado si ya uhakika.

Ili kuondokana na hali hiyo, ni wakati sasa wa kutumia nishati ya jua na upepo ambayo ni rahisi na rafiki wa mazingira.

Serikali pia inapaswa kuelekeza nguvu na rasilimali fedha katika usimamizi wa sheria, kanuni na sera ya kutunza, kuhifadhi na kulinda vyanzo vya maji vilivyopo.

Tukiacha vyanzo vya maji viharibiwe, athari zake zitakuwa kubwa kwa mazingira na kuzuia upatikanaji wa mvua.