Ubambikiaji wa kesi za Jinai ufike mwisho

Ubambikiaji wa kesi za Jinai ufike mwisho

Muktasari:

  • Siku za karibuni, tumeshuhudia malalamiko mengi ya Watanzania kubambikiwa kesi hasa za uhujumu uchumi ambazo hazina dhamana kisheria.

Siku za karibuni, tumeshuhudia malalamiko mengi ya Watanzania kubambikiwa kesi hasa za uhujumu uchumi ambazo hazina dhamana kisheria.

Tunaamini hili linapaswa kufika mwisho kwa kuwa ni kinyume cha haki za binadamu.

Kutokana na uzito wa suala hili, hata Rais Samia Suluhu Hassan aliwahi kulizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam, akitaka mamlaka zinazohusika kufuta kesi ambazo hazina mashiko na za kubambikiana makosa.

Tunaamini, kauli hii ya Rais ni maagizo muhimu kwa vyombo vinavyohusika na haki, ikiwamo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi, hivyo suala hili baya litafika mwisho.

Tunayasema haya kwa sababu katika gazeti letu la Aprili 30, 2021, tumeandika kwa kirefu namna polisi wa Usa River mkoani Arusha wanavyodaiwa kutaka kumbambikia kesi ya uhujumu Profesa Justine Maeda.

Inadaiwa askari hao walifika nyumbani kwake wakidai wanataka kufanya upekuzi kwamba ana nyara za Serikali alizoficha na hawakujihangaisha kupekua nyumba, bali walikwenda moja kwa moja shambani kwake kulipokuwa na mizinga ya nyuki na kutoa vitu vilivyofanana na pembe za mnyama.

Tukio kama hili liliwahi kutokea Januari mwaka jana huko Marangu Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, polisi wakiwa na watu wengine ambao hawajulikani walimkamata mfanyabiashara ua Utalii, Jullius Mlay.

Polisi hao na watu wengine waliojitambulisha kama maofisa usalama wa Taifa, walimtisha mfanyabiashara huyo kuwa wangemfungulia kesi ya uhujumu uchumi na angefia gerezani hivyo wakamtaka awape rushwa ya Sh140 milioni.

Hata hivyo, walipomshurutisha mfanyabiashara huyo atoe fedha kwa wakala, alikosea kwa makusudi namba ya siri na hiyo ndiyo ilikuwa salama yake kwa kuwa fedha hazikutoka na walimwachia kwa ahadi awaletee fedha hizo siku inayofuata.

Baada ya kupata upenyo huo, alitoa taarifa polisi ambao walikamatwa na walifunguliwa mashitaka ya kijeshi na kupatikana na hatia na kufukuzwa kazi na kisha kufunguliwa kesi ya kuunda genge la kihalifu.

Desemba mwaka jana, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga alionya watu kubambikiana kesi wakati alipotembelea Gereza la Karanga mjini Moshi na kuzungumza na wafungwa na mahabusu na suala hili liliibuka.

Tumejaribu kueleza kwa kirefu kuonyesha kuwa tatizo la watu kubambikiwa kesi ama na vyombo vya dola au baina ya mtu na mtu kwa kusaidiwa na maofisa wasio waaminifu wa vyombo vya dola ni kubwa na linahitaji kupatiwa ufumbuzi.

Bahati mbaya sana, makosa wanayoshtakiwa nayo ni uhujumu uchumi ambayo ndani yake kuna utakatishaji wa fedha, hivyo kuwafanya watuhumiwa kukaa mahabusu muda mrefu na mwisho hukubali kukiri makosa ili tu wawe huru.

Mambo ya namna hii yasipodhibitiwa mapema yanaibua chuki na kukandamiza haki, jambo ambalo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya utawala bora, haipaswi kujipaka matope kwa hilo.

Ni wakati sasa wa vyombo vyetu vya kiuchunguzi kutambua dhamana waliyonayo katika kutenda haki na wasitumie vibaya ofisi zao kubambikia watu kesi ili kujenga mazingira ya kupata fedha au kumkomoa mtu kwa sababu zozote zile.