UCHAMBUZI: Dodoma ilindwe isipoteze asili yake

Muktasari:

  • Nimeanza na simulizi hiyo ili kueleza umuhimu wa historia muhimu ya eneo fulani kulindwa kwa ajili ya vizazi vijavyo na ndivyo inavyotakiwa kwa kila eneo. Kama ilivyo miji yote nchini kwa kuwa na historia yake, vivyo hivyo Dodoma nayo ina historia na tamaduni zake za wenyeji zinazostahili kulindwa wakati wote.

Mji wa Bukoba ulianza kujengwa miaka ya 1890 na Kamanda wa Jeshi la Kijerumani, Emin Pasha akilikimbia eneo la Mubembe, Wilaya ya Bukoba baada ya machifu kuagiza asipewe chakula yeye na askari wake.

Baada ya hatua hiyo, Pasha alihamia eneo la mwambao wa Ziwa Victoria ambalo ni Bukoba ya leo. Aliwavuta watu kwa mapishi ya vyakula vya bure na ukarimu wake ulivuma hadi mbali na watu kutamani kuwa na makazi karibu na huyo mpelelezi. Hii ndiyo asili ya eneo la Kashura lililopo kwenye vilima vya mji wa Bukoba. Ni eneo ambalo watu waliitana kwa makundi kwenda kujichana. Kwa sababu hiyo linaendelea kuwa eneo muhimu kihistoria.

Nimeanza na simulizi hiyo ili kueleza umuhimu wa historia muhimu ya eneo fulani kulindwa kwa ajili ya vizazi vijavyo na ndivyo inavyotakiwa kwa kila eneo. Kama ilivyo miji yote nchini kwa kuwa na historia yake, vivyo hivyo Dodoma nayo ina historia na tamaduni zake za wenyeji zinazostahili kulindwa wakati wote.

Baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuamua na kuanza kutekeleza uhamishaji wa shughuli zote za kiutawala kutoka Dar es Salaam kwenda katika Jiji la Dodoma, kwa vyovyote vile kuna mabadiliko makubwa kuanzia kwenye mfumo wa maisha hadi taswira ya jiji lenyewe.

Dodoma ni mji uliozoea kupokea wageni wa muda wakati wa matukio maalumu na sasa kuna wimbi la wageni wa kudumu wenye mila na tamaduni tofauti. Ni katika kipindi hiki wananchi watashuhudia wageni wengi wa mataifa mengine kuliko wakati mwingine wowote.

Ukuaji wa Jiji la Dodoma tayari umeanza kwenda sambamba na kasi ya upanuzi wa miundombinu ya barabara, umeme na majengo ya kisasa kwa ajili ya shughuli za kiofisi na biashara ili kuleta taswira hasa ya makao makuu ya nchi.

Wakati haya yakifanyika ni vizuri kukumbuka kuwa Dodoma ina historia yake ambayo haitakiwi kuathiriwa na wingi wa wageni ikiwa ni pamoja na kuhifadhi majengo ya kale ambayo badala ya kubomolewa yanaweza kuboreshwa bila kupoteza muundo wake.

Ni eneo lenye mitaa yenye majina ya asili ambayo wenyeji wanajua kisa na mikasa iliyotokea hadi yakawepo ambapo ukuaji wa mji na mabadiliko yanayoendelea kutokea yasipewe nafasi ya kumeza historia.

Majina ya wanasiasa yasipewe nafasi ya kufuta majina ya kihistoria katika mitaa na barabara zinazojengwa. Maeneo ya Ihumwa, Chadulu, Nara, Nkhuhungu na mengineyo yanatakiwa kukua huku asili yake ikilindwa kama yalivyokutwa. Isiruhusiwe barabara ya asili itakayoongezewa mathalan kilomita moja ya lami, kubadilishwa jina wakati wa uzinduzi na kutunukiwa jina la mwanasiasa ambaye kimsingi anakuwa tayari amepewa heshima hiyo katika maeneo mengine.

Machapisho yanathibitisha kuwa Dodoma asili yake inatokana na neno la wenyeji ambao ni Wagogo la ‘Idodomya’ na chanzo chake ni eneo chepe ambalo tembo alikutwa amedidimia, yaani yadodomela.

Hii ndiyo sababu matukio ya Dodoma kutembelewa na tembo hayakwepeki, ni njia yao tangu zamani na wanyama hao wana uwezo wa kutunza kumbukumbu kwa miaka mingi na kila mtoto huonyeshwa njia aliyopita babu yake. Mwingiliano wa wageni hasa kutoka nje ulisababisha mabadiliko ya matamshi kwa kutoifahamu lugha ya wenyeji na kupaita Dodoma, jina lililorasimishwa kwenye vitabu na ramani na kutumika mpaka sasa.

Jiji la Dodoma linaweza kuwa sehemu ya kuvutia kama uendelezwaji wake utazingatia ulinzi na uhifadhi wa mambo ya kihistoria ambayo ndiyo msingi wa kuwepo kwake na vizazi vijavyo vitapenda kujifunza.

0767489094