UCHAMBUZI: Kiswahili kinaweza kuwa Lingua Franka ya dunia

Tuesday March 31 2020
PIC KIWAHILI

Amani Njoka

Nchi mbalimbali zimeonyesha nia ya dhati ya kutaka kujifunza Kiswahili ikiwamo kutaka kifundishwe shuleni na vyuoni.

Tuna mfano mzuri wa nchi ya Afrika Kusini, ambayo pamoja na kuwa na lugha zaidi ya 15 zinazofundishwa katika shule zake, haikuridhika hadi ikataka Kiswahili nacho kitumike.

Mjadala wa Afrika Kusini kukikumbatia Kiswahili ulimuibua mwanasiasa machachari wa nchi hiyo, Julius Malema aliyesema kuwa Kiswahili kinaweza kuiunganisha Afrika na kuwa kitu kimoja kwa kuwa kinaenea sana

Dunia ya sasa ni dunia inayohitaji watu kuchangamana na kuingiliana katika nyanja zote za kimaisha. Kama watu hawa wanachangamana na wanatoka katika jamii na mataifa tofauti yanayotumia lugha tofauti, hakuna budi kuwapo kwa lugha moja ya kuwaunganisha kimawasiliano wanapokutana. Katika fani ya lugha, lugha hiyo huitwa ‘Lingua Franka’.

Lingua franka ni lugha inayowawezesha watu kutoka jamii mbili au zaidi zinazotumia lugha tofauti kuwasiliana. Kwa mfano, kwa Tanzania kuna makabila mengi na pale ambapo watu wa makabila tofauti wanapokutana basi watatumia Kiswahili au lugha ya Kiingereza.

Mpaka sasa Kiswahili kinazungumzwa Afrika Mashariki, Kati, Kusini kwa kiasi fulani na sehemu nyingine za bara Asia. Pia kuna watu Marekani na Ulaya ambao wanakitumia kwa masomo na shughuli nyinginezo. Takwimu hizo zinafanya wazungumzaji wa Kiswahili kuwa zaidi ya milioni 120 duniani.

Advertisement

Watu milioni 120 ni wengi sana, hii ina maana kwamba mtu yeyote anapotembelea Afrika Mashariki na Kati hakwepi kukutana na wazungumzaji wa Kiswahili, kila mahali na katika shughuli yoyote.

Afrika Mashariki ina kila kitu kinachoweza kuwavutia wageni ikiwamo utalii, masomo, uwekezaji, biashara na shughuli nyingine za kibinadamu. Maana yake ni kwamba Kiswahili kinapaswa kuwa daraja la kuwaunganisha watu hawa. Kiswahili hakikwepeki katika maeneo yafuatayo.

Biashara, ni shughuli muhimu zaidi ya ubadilishanaji na ununuzi wa bidhaa iliyowaunganisha watu wa jamii tofauti tangu kale.

Licha ya mataifa ya nje ya Afrika kuja Afrika Mashariki kufanya biashara, raia wengi wa Afrika hutembelea Afrika Mashariki kwa ajili ya biashara, mathalani mataifa ya Afrika ya kati kama Congo hutumia bandari za Dar es Salaam na Mombasa. Wageni hao wanapotembelea Afrika Mashariki hulazimika kutumia Kiswahili. Matumizi ya Kiswahili huwaunganisha wafanyabiashara kutoka mataifa yasiyozungumza Kiswahili na kufanikisha biashara zao.

Utalii, wageni wengi hasa nje ya Afrika huwa na utamaduni wa kutalii.

Kuwapo kwa mbuga za wanyama kama Serengeti, Hifadhi ya Ngorongoro na nyinginezo huwafanya wageni kuvutiwa zaidi kutembelea Afrika Mashariki kwa ajili ya utalii.

Kwa kuwa wageni hawa wanakuja katika mazingira mageni, huamua kujifunza Kiswahili au kuokoteza maneno ambayo angalau yataleta maelewano miongoni mwao na wenyeji.

Elimu, zipo taasisi za nyingi za kielimu ndani na nje ya nchi na Afrika Mashariki ambazo hutahini wanafunzi kwa ajili ya mafunzo ya lugha ya Kiswahili.

Taasisi hizi huwaleta pamoja wanafunzi wa lugha hiyo na kuitumia wakati wa kuwasiliana na hata mazoezi yao ya darasani na hivyo kukifahamu zaidi Kiswahili na kule wanapoenda hukieneza na hatimaye kupata wazungumzaji wapya.

Mikutano ya kisiasa na kidiplomasia, hili ni eneo jingine ambalo huwakutanisha wakuu wa mataifa mbalimbali kwa ajili ya masuala yahusuyo nchi zao.

Katika mikutano hiyo zipo lugha ambazo huwa ni rasmi kwa mawasiliano. Kwa sasa Kiswahili ni lugha rasmi katika Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Hatua hii ni muhimu sana na inakiweka Kiswahili katika uwanja wa kutumiwa na watu wengi zaidi kadri siku zinavyokwenda.

Vyombo vya habari, ni njia muhimu sana ya kufikisha habari popote pale. Kwa kuwa vyombo vya habari hukusudia kufikisha ujumbe kwa watu, hutumia lugha inayoeleweka kwa jamii.

Haja ya mashirika makubwa ya habari duniani kama BBC, Sauti ya Amerika, Redio Ufaransa, Idhaa ya Kiswahili ya DW na mengineyo kuwafikia wasikilizaji wanaotumia Kiswahili popote duniani, kumevilazimu vyombo hivi kutumia Kiswahili.

Matumizi ya Kiswahili katika maeneo haya yamekifanya Kiswahili kuendelea kuzungumzwa na kuenea kwa kasi katika sehemu nyingi duniani.

Kwa sababu hiyo, Kiswahili kimekuwa mhimili wa mawasiliano kwa watu wengi na hivyo kuwa Lingua Franka miongoni mwa jamii za watu wanaozungumza lugha nyingi tofauti.

Mwandishi ni mdau na mwalimu wa Kiswahili. 0672395558

Advertisement