UCHAMBUZI: Ukarabati viwanja ni ukombozi wa soka la Tanzania

Monday March 09 2020

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally alitoa ahadi ya ukarabati wa viwanja vya soka vinavyomilikiwa na chama hicho ambavyo vimekuwa vikitumika katika mashindano mbalimbali ya mpira wa miguu.

Viwanja hivyo ni Sheikh Amri Abeid (Arusha), Nelson Mandela (Rukwa), Lake Tanganyika (Kigoma), Kambarage (Shinyanga), Jamhuri (Dodoma), Nangwanda Sijaona (Mtwara), Liti (Singida), Jamhuri (Dodoma), Ali Hassan Mwinyi (Tabora), Samora (Iringa) na Sokoine (Mbeya).

Dk. Bashiru alitoa ahadi hiyo katika mahojiano yake na wahariri wa kampuni ya Mwananchi Communications yaliyofanyika Tabata Relini jijini yaliko makao makuu ya kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa Dk. Bashiru, wameunda tume ambayo itashughulikia mchakato wa ukarabati wa viwanja hivyo ili viwe katika hadhi ya kimataifa ya kutumika kwa mechi za soka na matukio mengine.

Tume hiyo iliyoundwa na Kamati Kuu ya chama hicho, itakuwa chini ya uongozi wa mjumbe wa kamati hiyo ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Katibu huyo mkuu wa CCM alifafanua zaidi kuwa kipaumbele cha ukarabati huo kitakuwa ni marekebisho ya eneo la kuchezea, miundombinu ya utoaji majitaka, uwekaji wa mifumo ya maji ya mabomba na uchimbaji wa visima ili kupata uhakika wa saa 24 wa maji ya kumwagilia nyasi za viwanja hivyo.

Advertisement

Ahadi iliyotolewa na CCM juu ya viwanja ni nzuri na ni hatua za kupongezwa iwapo itafanyiwa kazi kwani changamoto ya miundombinu isiyoridhisha ya idadi kubwa ya viwanja vya soka nchini hasa vinavyomilikiwa na chama hicho imekuwa kilio sugu katika soka.

Timu na wachezaji wamekuwa wakishindwa kuonyesha viwango bora kutokana na ubovu wa eneo la kuchezea tofauti na inavyokuwa pindi wanapokuwa katika viwanja vizuri.

Badala ya soka la pasi na ufundi mwingi ambalo limekuwa likimfanya mchezaji aonyeshe ubora na ufundi wake na pia kuwavutia mashabiki, timu zimekuwa zikilazimika kucheza mipira mirefu ya juu ambayo inawanyima fursa timu na wachezaji kuonyesha viwango na ubora wao. Na hilo limekuwa likipelekea kuzipa wakati mgumu timu kwani huwa zinashindwa kutengeneza nafasi na kufunga idadi kubwa ya mabao.

Ushahidi wa hilo ni takwimu za ufungaji katika Ligi Kuu msimu huu ambapo wastani wa mabao yanayofungwa katika viwanja vyenye eneo zuri la kuchezea ni mabao mawili na zaidi kwa kila mchezo wakati kumekuwa na wastani wa chini ya mabao mawili kwa mechi zinazochezwa katika viwanja visivyo na eneo zuri la kuchezea.

Lakini ukiondoa suala la viwango vya wachezaji na mbinu za kitimu, athari nyingine ya kuchezea katika viwanja vibovu ni kusababisha majeraha ya muda mrefu na pia kuhatarisha afya zao, mashabiki na maofisa wanaotumia viwanja hivyo.

Athari nyingine ambayo inasababishwa na mechi kuchezwa katika viwanja visivyo na hali ya kuridhisha ni kukimbiza wadhamini ambao fedha zao zinahitajika katika uwekezaji na maendeleo ya mchezo wa soka hapa nchini.

Hivyo basi ni jambo jema kuona wamiliki wa viwanja hivyo wamegundua changamoto inayovikabili na kutangaza mkakati wa kuishughulikia kwa kuvifanyia ukarabati mkubwa.

Hata hivyo ahadi hiyo ya ukarabati wa viwanja inapaswa kutekelezwa kwa vitendo na isiishie katika makaratasi au kutumia muda mrefu kufanyiwa kazi.

Ni vyema ukarabati huo ukaanza sasa kwani kadri siku zinavyozidi kusogea, ndivyo vipaumbele vinavyopozidi kuongezeka na pengine ikapelekea hesabu kuhamishiwa katika mambo mengine badala ya maboresho ya viwanja.

Na ni vyema jambo hili lisiishie kwa wamiliki tu bali hata watumiaji wa viwanja hivyo nao wanapaswa kushirikiana kusaidia ukarabati huo badala ya kuutegea upande mmoja.

Ikumbukwe kwamba wadau wa soka ndio wanufaika wakubwa wa uwepo wa viwanja hivyo nao wanapaswa kulichukulia suala la ukarabati kama lao na sio kuwategea wamiliki ambao mwisho wa siku wanaweza kunufaika na matumizi ya viwanja katika shughuli nyingine tofauti na mpira wa miguu.

Wanaweza kushiriki kwa kutoa mawazo lakini pia hata kwa kuchangia rasilimali fedha ili kusaidia na kuharakisha mchakato wa maboresho hayo ambao umetangazwa na Dk Bashiru. Michezo ni sekta ambayo inaweza kuzalisha ajira za kutosha na kuinua uchumi wa nchi kupitia malipo ya kodi na uwekezaji.

Advertisement