UCHAMBUZI: Usiyatamani maendeleo, bali jipange kuyapata

Kila mtu anawaza maendeleo, hata Serikali pia huweka mpango wa maendeleo ndani ya miaka kadhaa ijayo. Ili kuyapata ni lazima kuwepo na mikakati inayohitaji kubadili namna ya kufikiri.

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema, Serikali yake imefanya mazuri na mabaya ila kilichomshangaza ni kwa Serikali zilizofuata kuiga mabaya na kuacha mazuri aliyofanya.

Baadhi ya viongozi walioiga mabaya ambayo kimsingi yalikuwa na madhara ya kiuchumi, waliamua kufikiri na kutenda hivyo ama kwa kujua au kutokujua. Matokeo ya kunena au kutenda yanayotokana na mawazo aliyonayo mwanadamu husika.

Maandiko matakatifu yanasema mtu hunena yaliyomjaa. Kunahitajika kubadili namna ya kufikiri kuelewa kuwa ni lazima ufanye kazi ndio ule na si vinginevyo.

Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi aliwahi kusema kila zama na kitabu chake. Kwa tafsiri ya kawaida kila awamu huja na mambo yake, kikubwa ni watu kuacha mazoea ya awamu zilizopita au kufananisha awamu iliyopo na zilizotangulia.

Kubadili namna ya kufikiri ni muhimu kwani inasaidia kuondoa msongo wa mawazo, hasira na mambo mengine yanayoweza kuhatarisha afya.

Leo nataka kuzungumzia miundombinu mbalimbali ya uchumi inayotekelezwa na Serikali ili kuonyesha matumizi endelevu ya kodi za wananchi.

Serikali inafanya kazi kubwa katika ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi. Huenda faida zake zisiwe za kipindi kifupi kijacho ila zina umuhimu kwa muda mrefu ujao.

Awamu ya kwanza ilijenga miundombinu ya uchumi vikiwamo viwanda vya kimkakati, reli, barabara, hoteli, vyuo vya ufundi, shule na hospitali kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanatekeleza majukumu yao vizuri na kwa wepesi.

Badala ya kikundi kidogo cha watu kufaidika na rasilimali za nchi, iliahakikisha kiasi kikubwa cha fedha kinatumika kutekeleza miradi yenye faida kwa kizazi cha sasa na baadaye.

Miundombinu ya uchumi inayoendelea kujengwa sasa ikiwamo reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege, ununuzi wa meli na ndege, ina lengo la kuhakikisha shughuli za maendeleo zinafanyika kwa urahisi pia. Hii ni pamoja na uwekezaji katika sekta ya umeme, afya, maji na elimu.

Kuimarisha miundombinu ya uchumi pamoja na kuzuia bidhaa zinazoingizwa nchini kunakusudia kuendeleza viwanda vya ndani na kukuza sekta zitkazoongeza uzalishaji wa bidhaa zinazosafirishwa kwenda nje.

Nchi yoyote inahitajika kukuza, kuimarisha na kuendeleza miundombinu ya uchumi ili ielekeze fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo kuliko matumizi ya kawaida. Kuelewa falsafa hii inahitaji kubadili namna ya kufikiri.

Tanzania sasa imejielekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya uchumi, uendelezaji na uimarishaji wa miundombinu ya uchumi kwa kuwekeza kwenye miradi mikubwa kama ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) inayokisiwa kugharimu Sh7 trilioni kuikamilisha.

Mradi wa kufufua umeme katika Bonde la Mto Rufiji unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,100 ukigharimu zaidi ya Sh6 trilioni utaifanya Tanzania kuwa miongoni kwa nchi zinazozalisha umeme nafuu Afrika.

Ununuzi wa ndege aina ya Bombardier, Boeing Dremliner na Airbus uliofanywa ili kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) umegharimu zaidi ya Sh739.6 bilioni. Hii yote ni miradi ya kimkakati ambayo inakusudia kutengeneza miundombinu ya uchumi ya muda mrefu.

Serikali pia inaimarisha miundombinu vijijini kwa kuhakikisha kila kimoja kinaunganishiwa umeme ili kuchochea na kukuza maendeleo. Tayari Mradi wa Umeme Vijijini (Rea) kwa kipindi cha mwaka Julai 2016 hadi Machi 2017 ulitengewa na kupewa Sh389.2 bilioni.

Na ili kukuza sekta ya barabara, Serikali imeanzisha Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) kuhakikisha miundombinu ya Serikali za Mitaa inaimarika na kuchangia kukuza uchumi.

Aidha, Serikali ipo mbioni kuanzisha Wakala wa Maji Mjini na Vijijini (Ruwa) kuhakikisha huduma bora na salama inapatikana kwa wananchi wote.

Miundombinu ya uchumi inajumuisha sekta ya elimu, kwa kutambua hilo Serikali imeendelea kutoa elimu bila malipo kwa Watanzania wanyonge na maskini kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne, huduma hii huigharimu Serikali wastani wa Sh28.3 bilioni kila mwezi ambazo ni sawa na Sh339.6 bilioni kwa mwaka.

Mwandishi Anapatikana kwa namba ya simu 0685-214949