Udhibiti uimarishwe kuongeza samaki Ziwa Viktoria

Muktasari:

  • Kiuchumi, wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, hasa Mwanza, Kagera, Mara, Geita na sehemu kidogo ya Mkoa wa Simiyu katika eneo la Ramadi wilayani Busega, wanategemea shughuli ya uvuvi ndani ya ziwa hilo linalopatikana Tanzania, keny ana Uganda.

Asilimi 51 ya Ziwa Victoria ipo Tanzania na kiasi kinachobaki kipo kwenye mataifa mengine ya Afrika Mashariki.

Kiuchumi, wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, hasa Mwanza, Kagera, Mara, Geita na sehemu kidogo ya Mkoa wa Simiyu katika eneo la Ramadi wilayani Busega, wanategemea shughuli ya uvuvi ndani ya ziwa hilo linalopatikana Tanzania, keny ana Uganda.

Hata hivyo, wavuvi katika mikoa hiyo wameanza kuingiwa na hofu kutokana idadi ya samaki wanaovuliwa hasa sato na sangara kuendelea kupungua mwaka hadi mwaka.

Samaki wengine kama vile ningu, njegere au kuyu, hongwe, nembe, gogogo na domodomo au mbete wanatoweka pia.

Takwimu za Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri), Kituo cha Mwanza zinaonyesha uzalishaji wa samaki ndani ya Ziwa Victoria ulishuka kwa asilimia 25 mwaka 2016 ikilinganishwa na mwaka 2015.

Hata hivyo, takwimu hizo zinaonyesha dagaa waliongezeka kwa tani 62, 668 baada ya kuvuliwa tani 433, 845 mwaka 2015 kulinganisha na tani 371, 177 zilizovuliwa mwaka 2014, furu waliongezeka kutoka tani 58, 386 mwaka 2014 hadi kufikia tani 67, 297 mwaka 2015, ikiwa ni ongezeko la tani 8, 911.

Mkuu wa idara ya utafiti wa ubora wa maji na usafi wa mazingira kutoka kituo cha utafiti mkoani Mwanza (Tafiri), Charles Ezekiel anasema katika sensa zinayofanyika kila baada ya miaka miwili zinabainisha ongezeko la wavuvi mara dufu tangu mwaka 2000 walipokuwa 55, 985 ambao sasa wamefika 109, 397.

Licha ya wavuvi, zana ni suala jingine la kupungua kwa samaki ziwani humo. Ezekiel anasema miaka 16 iliyopita kulikuwa na vyombo 15,434 vya uvuvi ambavyo vimeongezeka mpaka 31,773 mwaka jana.

Sababu nyingine ya upungufu wa samaki ni kujaa kwa udongo ndani ya ziwa hilo hali inayosababisha maji kupoteza uangavu na upungufu wa chakula unaosababishwa na uchafuzi wa mazingira.

Kwa kuwa wataalam wa masuala ya nguvu ya uvuvi ndio yametajwa kuwa chanzo cha samaki hao kupungua kutokana na baadhi yao kutumia dhana haramu za uvuvi, ni vema serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo kuhakikisha inadhibiti hali hiyo mara moja.

Halikadhalika serikali kwa kushirikiana na vyombo vya dola inatakiwa kudhibiti uvushaji samaki kwa magendo mipakani tatizo linaloonekana kushamiri siku za karibuni.

Doria ya mara kwa mara kwenye zaidi ya mialo 640 ziongezwe kusaidia kubaini wavuvi wanaotumia zana haramu kuvua kwenye mazalia ya samaki yaliyoko pembeni mwa ziwa hususan sato na furu.

Suala la uchache wa wataalam katika sekta ya uvuvi nalo linatakiwa kuangaliwa upya kwa kuwa licha ya upungufu huo kuanzia halmashauri hadi mkoa, baadhi yao wamekuwa wakituhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa wawapo doria.

Pamoja na mambo mengine, serikali inatakiwa kuimarisha kamati za ulinzi wa rasilimali za Ziwa Victoria (BMU) ambazo nyingi hazina wataalam wa kutosha kukabiliana na uvuvi haramu kwenye mialo.

Kamati hizo ambazo zinatekeleza kazi ya ulinzi na usimamizi wa ziwa, nyingi hazina vitendea kazi vinavyorahisha kufanya doria hususan nyakati za usiku.

Samaki ni chanzo kizuri cha protini na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha Watanzania tunatumia kiasi kidogo cha virutubisho hivyo.

Licha ya vyanzo vingi vya maji vilivyopo nchini, bado wananchi hawapati samati wa kutosha kulingana na viwango vya kimataifa.

Endapo ulinzi utaongezwa fursa nyingine kama vile utalii zinaweza zikazalishwa hivyo kukuza kipato cha wananchi na taifa kwa ujumla.

Ngollo ni mwandishi wa gazeti hili Mwanza. Anapatikana kwa namba 0757 708 277