Umeme wa gridi uongeze uzalishaji Kigoma

Muktasari:

Kuanzia jana, Kigoma imeungana na mikoa mingine inayotumia umeme wa gridi ya Taifa kupata nishati ya uhakika baada ya miaka mingi ya kusubiri.

Kuanzia jana, Kigoma imeungana na mikoa mingine inayotumia umeme wa gridi ya Taifa kupata nishati ya uhakika baada ya miaka mingi ya kusubiri.

Pamoja na Kigoma, Geita na baadhi ya wilaya za Mkoa wa Kagera ambazo walau zilikuwa zinatumia umeme kutoka Uganda, nazo zimeingia kwenye mfumo huo wa nishati ya uhakika zaidi nchini.

Ingawa ni zaidi ya miaka 60 tangu Tanzania ipate uhuru Kigoma ndio imeingizwa kwenye gridi ya Taifa. Mkoa huu ni muhimu kwa uchumi wa Taifa ukizingatia kwamba unapakana na mataifa kadhaa ambayo Tanzania inaweza kufanya nayo biashara.

Wakazi wa Kigoma ambao wameongezeka kutoka milioni 2.12 mwaka 2012 mpaka millioni 2.89 mwaka 2021 sasa watakuwa na wigo mpana wa kutanua shughuli za uzalishaji na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.

Umeme huu utatoa fursa za kuzalisha mali kwa muda mrefu zaidi na kufanikisha mapambano dhidi ya umasikini, hasa kipindi hiki Serikali inapotekeleza Mpango wa tatu wa maendeleo wa Taifa na Malengo ya Maendeleo Endelevu ili kuinua ubora wa maisha, ustawi wa jamii na kupunguza umaskini.

Takwimu zinaonyesha watu wanaoishi chini ya dola moja kwa siku walikuwa asilimia 26.4 mwaka 2018 lakini malengo yaliyopo ni kuwapunguza mpaka asilimia 22 mwaka 2025/26. Kigoma na mikoa hii mingine iliyofikiwa na umeme wa gridi, sasa inayo nafasi ya kukuza uchumi na kipato cha kila mwananchi.

Ni wakati muafaka kwa Kigoma kuimarisha uchumi wake saa hivi kuanzi amashambani, viwandani mpaka uvuvi unaofanywa Ziwa Tanganyika ili kukabiliana na umaskini unaoelezwa kuwa ule wa mahitaji ya msingi ni asilimia 26.4.

Mathalan, hivi sasa uwekezaji katika shughuli za uvuvi unaweza kufanyika kwa kiwango kikubwa na uhakika zaidi kutokana na uhakika wa umeme, tofauti na ule uliokuwa unazalishwa na majenereta.

Kigoma ni mkoa unaozalisha chakula kwa wingi na hali ya hewa inaruhusu uzalishaji wa kiwango cha kibiashara ikilima zaidi na umeme ukawezesha uongezaji wa thamani wa mazao hao, njaa itaondoshwa nchini.

Mpaka Desemba 2021, Tanzania ilikuwa na zaidi ya watu milioni 6.39 wanaonufaika na Mpango wa kunusuru kaya maskini (Tasaf). Kwa kutumia rasilimali zilizopo, Kigoma na mikoa mingine ikiweka mikakati makini, itakuwa rahisi kuongeza uzalishaji wenye tija hivyo kuliwezesha Taifa kuondokana na umasikini.

Umeme huu ukafungue fursa kwa wananchi wa Kigoma hasa wanawake wanaojihusisha na uzalishaji mafuta ya maweze, sabuni, biashara ya chakula na huduma nyingine zo zinazotegemea umeme kwa kiwango kikubwa.

Serikali ya mkoa nayo ivutie wawekezaji watakaojenga viwanda, kufungua mashamba makubwa ya chikichi na mazao mengine pamoja na kuimarisha huduma za afya, shughuli za uchimbaji madini na biashara kwa ujumla wake.

Umeme wa uhakika umaanishe na kuonyesha uzalishaji wa muda mrefu zaidi. Huduma zipatikane hata usiku tofauti na ilivyokuwa zamani. Watu wasikeshe kutazama runinga au tamthilia pekee bali uzalishaji hata wa juisi na bidhaa nyingine nyepesi ufanyike majumbani na kwingineko.

Pamoja na umeme, Serikali inaendelea kuimarish amiundombinu ya usafirishaji mkoani humo kuanzia reli, barabara mpaka meli. Hizi zote ni fursa zinazopaswa kuchangamkiwa na wana Kigoma kuelekea kuimarisha uchumi wao ili kuondokana na changamoto zinazodumaza maisha yakiwamo magonjwa ya kipindupindu na mengine yanayoepukika kwa usafi tu.