Prime
Umesoma vitabu vingapi mwaka huu?
Najua nimeuliza swali ambalo msomaji pengine naye anaweza kutaka kujua mwandishi kasoma vitabu vingapi.
Mhh!sitojibu swali hilo. Idadi ya vitabu nilivyosoma inabaki kuwa siri yangu, kama ambavyo pia inawezekana sikushika kitabu hata kimoja mwaka mzima.
Kwa nini nimeuliza umesoma vitabu vingapi mwaka huu? Nataka ujisaili moyoni mwako kuhusu usomaji. Na hapa nisisitize kuwa usomaji ni zaidi ya vitabu.
Kuna machapisho ya aina mbalimbali ambayo ni muhimu kwa maisha yetu.
Kuanzia machapisho ya nakala ngumu kwa maana ya vitabu, magazeti, majarida, vitini hadi mitandaoni, mwote kuna maarifa ambayo watu wengi tunayakosa kwa kutokuwa na utamaduni wa usomaji.
Nilishawahi kuandika kioja cha Watanzania wanaoweza kusafiri masafa marefu kwenye mabasi, wakaishia kutazama filamu, kuzungumza au kulala.
Basi la watu zaidi ya 40 kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kwa mfano, unaweza usimkute abiria hata mmoja aliye na kitabu au chapisho lolote mkononi kwa safari nzima ya kutwa nzima.
Licha ya maarifa kuwekwa hata mtandaoni, abiria hao wote wana simu tena zile janja. Lakini ni wangapi wanaotumia simu zao kusaka machapisho ya mtandaoni? Sanasana simu hizo zinatumika kutafuta taarifa za umbea na mipasho ya watu maarufu.Waliojiongeza angalau watatafuta habari za michezo.
Watu hawa wanasahau kuwa mtandaoni kuna utajiri mwingi wa maarifa nje ya udaku, burudani na michezo. Ni ukweli kwa wengi wetu, simu zimekuwa kifaa cha mrengo wa burudani zaidi kuliko kifaa cha kutupatia maarifa na hata maendeleo.
Leo hii machapisho mengi yamewekwa mtandaoni. Unaweza kusaka kitabu ukitakacho ukakipata mtandaoni. Lakini wangapi wanaotumia simu zao kusaka maarifa kupitia vitabu?
Wasichojua wengi kusoma vitabu ni moja ya shughuli muhimu katika maisha ya kila siku, kwani hujenga maarifa, ufahamu na mtazamo mpana kuhusu jamii unayoishi na dunia kwa jumla.
Vitabu vinatoa fursa ya kujifunza kutoka kwa wataalamu, wasomi, na waandishi kutoka maeneo tofauti, na hili linakuwa jambo la faida kubwa kwa maendeleo na ustawi wa kiakili wa msomaji.
Mimi nimesoma vitabu kadhaa na nimeona nguvu ya usomaji. Wewe mkurugenzi katika shirika, machinga, mama wa nyumbani au mwanafunzi huna sababu ya kutosoma.
Ukiwa bosi wa kampuni, kuna mambo utakayohitajika kuyajua kutoka kwa wengine. Hayo unaweza kuyapata vitabuni au kwenye machapisho mengine kedekede. Kwa machinga na mjasiriamali mdogo, kuna vitabu tele kuhusu ujasiriamali. Umevitafuta ili kupata maarifa zaidi yanayoweza kukutoa ulipo kwenda kwingine kwenye mafanikio zaidi?
Hata wale wasaka fedha kama msingi wa maisha, kuna mengi yameandikwa kuhusu mbinu za usakaji wa fedha. Tafuta machapisho ujue namna ya kupata fedha ufurahi na moyo wako!
Nikumbushe tu kuwa usomaji una faida chekwa. Kwanza vitabu ni chanzo kikubwa cha maarifa. Unaposoma, unapata habari, mawazo, na mbinu za kukabiliana na maisha katika nyanja mbalimbali.
Vitabu vya kihistoria vinaweza kukusaidia kuelewa tamaduni na hali za watu katika maeneo tofauti duniani.
Usomaji vitabu ni njia nzuri ya kuongeza ufanisi katika kazi na masomo. Watu wanaosoma vitabu mara kwa mara hupata uwezo bora wa kuelewa, kuchanganua, na kutoa maoni kuhusu mambo mbalimbali.
Hii ni kwa sababu vitabu vinatoa mifano na mbinu za kufikiri kwa kina ambazo hujenga ufanisi wa kiakili.
Kwa mfano, vitabu vya fasihi vinasaidia kukuza uwezo wa kufikiri kwa kina na kupanua ufahamu wa jamii.
Kusoma vitabu pia ni njia nzuri ya kupunguza msongo wa mawazo. Kwa wengi, vitabu ni mahali pa kupumzishia akili. Kusoma riwaya au hadithi za kubuni ni kimbilio kutokana na changamoto za kila siku.
Aidha, vitabu vinajenga uwezo wa lugha na uandishi. Kila kitabu kinakuwa na mtindo wake wa utumizi wa lugha na hivyo kukuongezea msamiati na maarifa mengine ya lugha.
Wapo watu wengi wamebadili maisha kutoka hali duni kwenda hali bora zaidi kupitia usomaji vitabu. Wewe unachelewa wapi. Anza sasa kusaka vitabu uone utajiri uliomo kwenye maandishi.
Kwa haya machache yaliyotajwa, ni dhahiri kuwa wasiosoma wanakosa uhondo mwingi. Kama mwaka huu haukuwa wa vitabu kwako, weka azma mwaka 2025 uzidishe kasi ya kubukua.
Abeid Poyo ni mhariri wa elimu wa Mwananchi. 0754990083