Uongozi uko wapi soko kuuzwa kinyemela
Soko la Kurasini, lililopo Mtaa wa Shimo la Udongo, Wilaya ya Temeke, linakabiliwa na mzozo baada ya kutolewa taarifa, limeuzwa na wafanyabiashara kwa mwekezaji kinyume na utaratibu, bila kushirikisha halmashauri.
Mzozo huu unaonyesha wazi umuhimu wa ushirikishwaji wa wahusika wote katika mchakato wa uuzaji au uendelezaji wa mali za umma.
Hakuna shaka kuwa hatua zilizochukuliwa na mwekezaji na viongozi wa soko zimeibua maswali mengi kuhusu uwazi wa mchakato wa uuzaji na haki za wafanyabiashara wa zamani.
Halmashauri ya Wilaya ya Temeke ina jukumu la kuhakikisha mali za umma zinahifadhiwa na kuendelezwa kwa manufaa ya wananchi wote, na kwamba mchakato wa uuzaji unafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu.
Hadi sasa, hali ni ya kutatanisha, na ni lazima wahusika wapewe nafasi ya kutoa maelezo kamili ili kumaliza utata huu wa kisheria na kimaadili.
Huu ni mgogoro mkubwa wa umiliki, kila upande unadai kuwa na haki ya kisheria na kihistoria.
Halmashauri inasisitiza kuwa soko hili ni mali yake na kwamba hawakushirikishwa kwenye mchakato wa uuzaji unaodaiwa kufanywa na mwekezaji.
Kwa upande wa wafanyabiashara, wanasema madai yao ni ya kihistoria, wakieleza kuwa walihamishiwa hapo kati ya miaka ya 1970 na 1980, hivyo wana haki ya kumiliki eneo hilo au kulipwa fidia kwa kuondoka.
Taarifa ya uuzaji wa soko hilo imezua mjadala, huku wakazi na wafanyabiashara wa Kurasini wakilalamika kuhusu hatua za uuzaji wanazodai hazikuwajumuisha.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Jomary Satura, Soko la Kurasini ni mali ya halmashauri na haki ya umiliki wa eneo hilo haiko mikononi mwa wafanyabiashara.
Anaeleza kuwa, ingawa wafanyabiashara wamekuwa wakifanya biashara hapo kwa muda mrefu, hawana haki ya kumiliki ardhi hiyo kwa mujibu wa sheria, hivyo Serikali za mitaa haziwezi kuwa na mamlaka ya kumiliki ardhi inayomilikiwa na halmashauri.
Hata hivyo, kutokana na taarifa ya uuzaji wa soko hilo kwa mwekezaji, halmashauri ilitoa tamko rasmi kupitia kitengo chake cha mawasiliano, ikikanusha kuhusika na mchakato huo wa uuzaji.
Hali ya mambo ilionekana kubadilika baada ya mwekezaji kuanzisha ujenzi wa uzio kuzunguka eneo la soko, jambo lililozua wasiwasi miongoni mwa wafanyabiashara na wakazi wa eneo hilo.
Wakati mwekezaji alipoanza kuweka uzio wa mabati, halmashauri ililazimika kuchukua hatua na kubandika tangazo la zuio, likisema kuwa shughuli zozote za uendelezaji katika eneo hilo hazikubaliki hadi hapo utaratibu wa kisheria utakapowekwa.
Hatua ya halmashauri kuweka tangazo la zuio inadhihirisha kuwa kuna wasiwasi kuhusu utaratibu wa uuzaji wa eneo hili, ingawa tangazo la zuio lilionekana kufutwa baada ya kubandikwa.
Ni wazi kuwa, hatua hii inaonesha kuwa kuna migogoro ya kiutawala na kiutendaji kuhusu uendelezaji wa Soko la Kurasini.
Serikali na halmashauri husika inapaswa kuchukua hatua za dharura kuhakikisha kuwa masuala haya yanapatiwa ufumbuzi wa kisheria na uwazi kamili, ili kuepuka kurudiwa kwa migogoro ya aina hii katika siku zijazo.