Upotoshaji wa kuchanganya maneno ya Kiingereza unavyofanywa na wanahabari

Muktasari:

Hata wale wanaoajiriwa kwa mkataba hawana ujuzi wa kutosha kwani baadhi yao wamejikita zaidi katika fasihi na wala si katika isimu ya lugha. Suala muhimu ni kuwa na maabara za lugha (Language laboratories) ambazo husaidia hasa watangazaji namna ya kutamka vizuri kwa kuzingatia mkazo katika neno, kiimbo na lafudhi iliyo sahihi.

Katika makala yangu ya mwisho, nilitoa maelezo kuhusu upotoshaji wa Kiswahili unaofanywa na waandishi wa magazeti, watangazaji wa redio na runinga. Upotoshaji huu unatokana na mambo mengi ambayo ni pamoja na kuchanganya maneno au misemo ya Kiswahili na ya Kiingereza katika mawasiliano. Wanashindwa kuelewa kuwa wasomaji na wasikilizaji wao ni wananchi wa kawaida ambao wengi wao ni wana kisomo kinacholingana na elimu ya msingi. Pili, kimaadili hatuchanganyi maneno au vifungu vya maneno kienyeji bila kufuata utaratibu.

Lengo la makala haya ni kushauri hatua za kuchukua ili kurekebisha makosa yanayojitokeza. Kwanza ni wahusika wenyewe kujitambua kuwa wana matatizo ya kisarufi kama ya upatanishi wa kisarufi, mofolojia, fonolojia na semantiki. Kutambua hivyo kutamfanya mhusika kujifunza kwa bidii na kujiendeleza katika taasisi zilizopo hapa nchini kama Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili (Tataki) , Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Taasisi ya Kiswahili ya Lugha za Kigeni ( Takiluki), huko Zanzibar. Hizi ni taasisi zinazotambulika kimataifa na mafunzo yanayotolewa ni ya hali ya juu. Kujiendeleza kwa mtu binafsi ni jambo la heri na wala lisingoje mwajiri kukushughulikia kwa kukusomesha. Wako wafanyakazi wanaojiongezea maarifa kwa kujisomesha na hii ni hatua ya kupigiwa mfano.

Pili, ni kwa waajiri kuona namna ya kuwasaidia wafanyakazi wake kwa kuwaandalia muundo wa ajira (Scheme of Service) unaoonyesha sifa za kitaaluma za mfanyakazi, uzoefu wake na muda wa kufanya kazi katika ngazi fulani.

Muundo huu unamsaidia mfanyakazi kujitambua aliko na wapi anakokwenda kitaaluma na kimasilahi. Huu ni mfumo wa kuwaendeleza wafanyakazi wakiwa kazini na si lazima mtu aende shuleni au chuoni kwa kozi ndefu bali anaweza kupata mafunzo ya muda mfupi kwa siku chache hata wiki wakati bado mwajiriwa yuko kazini.

Eneo la tatu ni mafunzo yanayotolewa katika vyuo vya mafunzo ya uandishi wa habari. Vyuo hivi vinafundisha pamoja na masomo mengine somo la Kiswahili, Kiingereza na mbinu za mawasiliano kwa jumla. Katika mafunzo ya Kiswahili masuala ya fasihi na isimu yanafundishwa. Tatizo ni kuwa hawapo walimu waliobobea katika taaluma ya lugha.

Hata wale wanaoajiriwa kwa mkataba hawana ujuzi wa kutosha kwani baadhi yao wamejikita zaidi katika fasihi na wala si katika isimu ya lugha. Suala muhimu ni kuwa na maabara za lugha (Language laboratories) ambazo husaidia hasa watangazaji namna ya kutamka vizuri kwa kuzingatia mkazo katika neno, kiimbo na lafudhi iliyo sahihi.

Kwa kusikiliza sauti na kutambua ni wapi pa kukazia silabi katika neno na ni wapi pa kushuka na kupanda kwa maana ya lafudhi. Kama mafunzo sahihi yatatolewa, watangazaji wanaweza kuondokana na athari za lugha zao za asili wanapotangaza. Kwa mujibu wa ‘Kitabu cha Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu” kilichotungwa na mabingwa wa Kiswahili wa Taasiis ya Uchunguzi wa Kiswahil (TUKI), sentensi ya Kiswahili inaweza kuleta maana tofauti kulingana na matumizi. Sentensi ni kama:

“Utakwenda mjini” Sentensi hii inaweza kuleta maana tofauti kama ikitumika kama :

Maelezo

Amri

Mshangao

Dharau

Swali

Bila kuwa na maabara ya lugha au vinasa sauti wakati wa kufundisha au kujisomea somo la isimu, ni vigumu kwa wanafunzi kuweza kutofautisha mazingira ya matumizi katika sentensi hizo.

Ni jambo la kutia moyo kuona kuwa Baraza la Habari la Taifa (MCT) limefanikiwa kuandaa mtalaa wa aina moja wa kufundisha katika vyuo vya habari nchini vinavyotoa elimu ya cheti, stashahada na shahada katika uandishi wa habari. Hatua hii ni mwanzo mzuri wa safari ndefu ya kuwaandaa wanahabari weledi katika fani ya uandishi.

Masuala mengine ni upatikanaji wa walimu wenye ujuzi wa fani ya uandishi wa habari, vitabu na vifaa vya ufundishaji. Kama itawezekana pawepo na utaratibu wa kuona kuwa yaliyokubalika yanatekelezwa. Hapa nina maana kuwa pawepo na kitengo MCT cha ukaguzi ambacho kitakuwa kikifuatilia maendeleo ya kitaaluma na kimaadili kwa waandishi pamoja na mazingira za kufanyia kazi.