Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Upungufu sekta ya afya ushughulikiwe    

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeibua upungufu katika maeneo mbalimbali, yakiwamo utoaji wa huduma za afya, usimamizi wa rasilimali watu na ufanisi wa taasisi za umma.

Miongoni mwa maeneo aliyoyaibua ni utoaji wa huduma ndani ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), hususan uhaba wa madaktari wa mazoezi ya viungo na wauguzi.

Hili si suala la taasisi moja pekee, bali ni kioo cha hali halisi ya mfumo wa afya unaohitaji maboresho ya haraka na ya kimkakati.

Sekta ya afya ni mhimili mkuu wa ustawi wa taifa, na changamoto zinazoikumba zinapaswa kushughulikiwa kwa uzito wa kipekee. Ucheleweshaji wa huduma kwa wagonjwa, unaotokana na mzigo mkubwa wa kazi kwa watumishi wachache, una athari kubwa zaidi ya afya ya mtu mmoja mmoja.

Wagonjwa wanapokaa muda mrefu hospitalini, si tu kwamba wanakosa nafasi ya kurejea kwenye shughuli zao za uzalishaji, bali pia mfumo wa afya unazidi kulemewa. Hali hii inapunguza ufanisi wa huduma na kuongeza gharama kwa Serikali na wananchi kwa ujumla.

Ni wazi kuwa afya bora ya wananchi ndiyo injini ya maendeleo ya kiuchumi, Taifa lenye nguvu kazi dhaifu kiafya haliwezi kufikia malengo yake ya kiuchumi kwa ufanisi. Wafanyakazi wagonjwa au wanaochelewa kupona hushindwa kushiriki kikamilifu katika uzalishaji mali, hali inayodhoofisha kasi ya ukuaji wa uchumi.

Hivyo, uwekezaji katika sekta ya afya si gharama, bali ni mtaji wa maendeleo ya muda mrefu unaopaswa kupewa kipaumbele cha juu katika mipango ya Serikali.

Katika kipindi hiki ambacho Serikali inaelekea kuandaa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, kuna kila sababu ya kuipa sekta ya afya kipaumbele cha juu zaidi. Bajeti hii inapaswa kuangalia si tu ujenzi wa miundombinu ya hospitali, bali pia kuimarisha rasilimali watu, ambao ndio uti wa mgongo wa utoaji wa huduma bora.

Kuongeza idadi ya madaktari wa mazoezi ya viungo na wauguzi ni hatua ya msingi itakayosaidia kupunguza mzigo uliopo na kuboresha ubora wa huduma kwa wagonjwa.

Tunatambua na kupongeza juhudi zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuongeza ajira na kuendeleza wataalamu wa afya. Hata hivyo, kasi ya juhudi hizi inapaswa kuongezwa zaidi ili kuendana na mahitaji halisi yaliyopo sasa, ambayo yanaonekana wazi kupitia ripoti ya CAG.

Ni muhimu pia kuhakikisha kuwa vibali vya ajira vinatolewa kwa wakati na kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya taasisi husika, ili kuondoa pengo lililopo kati ya mahitaji na upatikanaji wa watumishi.

Pia. Serikali inapaswa kuwekeza katika mifumo madhubuti ya usimamizi na upangaji wa kazi ili kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika kwa ufanisi wa hali ya juu, jambo llitakalosaidia kupunguza mianya ya uzembe, kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma kwa wakati unaostahili, bila kucheleweshwa na changamoto zinazoweza kuzuilika.

Kwa ujumla, changamoto zilizoainishwa na CAG zinapaswa kuchukuliwa kama fursa ya kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya afya. Hatua za haraka na za makusudi zikichukuliwa sasa, si tu zitaboresha huduma za afya, bali pia zitaimarisha msingi wa uchumi wa taifa kwa kuhakikisha nguvu kazi yenye afya njema.