Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uraia pacha unavyowakwamisha Watanzania kuwekeza nyumbani

Leo naendelea na somo la katiba kwa dhima ya mtunga katiba. Japo Katiba ya Tanzania imetoa haki mbalimbali, haki kuu kuliko haki zote, ni haki ya uraia, hii haki ya uraia, ni haki ya msingi ambayo haiwezi kuondolewa kwa namna yoyote, lakini sheria yetu ya uraia, inaweza kuiondoa haki hii ya msingi, kiubatili kwa sababu ubatili huo umeingizwa kwenye sheria.

Sheria ya Uraia ya Tanzania ya mwaka 1995, Sura 357 kama ilivyorejewa mwaka 2002, pamoja na kanuni zake za mwaka 1997, imeainisha aina tatu za uraia wa Tanzania ambazo ni; uraia wa Tanzania kwa kuzaliwa ambao haufutiki, uraia wa Tanzania kwa kurithi ambao ni wa damu na uraia wa Tanzania kwa tajnisi au kujiandikisha, huu ndio unaweza kufutika.

Tanzania inafuata kanuni za kimataifa za uraia za duniani kote yanaongozwa na falsafa kuu mbili ambazo ni haki za kidamu (Jus Sanguinis - The rights of blood) ambapo mtu hupata uraia kutokana na uhusiano wa kidamu na wazazi wenye uraia wa nchi husika na haki za kuzaliwa (Jus Soli - The right of Soil), ambayo mtu hupata uraia kutokana na kuzaliwa kwake katika ardhi ya nchi fulani.

Haki hizi mbili za uraia ni haki za asili, haziwezi kuondolewa. Haki za kidamu ni mtu hupata uraia kutokana na uhusiano wa kidamu na wazazi wenye uraia wa Tanzania kwa mtu kuzaliwa na wazazi Watanzania, au mzazi mmoja Mtanzania. Hivyo, ili mtu kuwa Mtanzania kwa kuzaliwa, anatakiwa pia kuwa na mzazi ambaye ni raia wa Tanzania, haki hii ni ya kidamu na haiwezi kuondolewa.

Falsafa ya pili, (Jus Soli - The right of Soil), ambayo mtu hupata uraia kutokana na kuzaliwa kwake katika ardhi ya Tanzania hata kama wazazi wake sio Watanzania. Hivyo, haki hii pia haiwezi kuondolewa.

Kwa vile hatuna uraia pacha, Mtanzania akipata uraia wa nchi nyingine yoyote, anapoteza haki zake za uraia wa Tanzania, kwa kuhesabiwa kuwa ameukana Utanzania, kitu ambacho sio kweli na sio haki, lakini ndivyo sheria inavyosema.

Hii maana yake na sheria yetu ya urais nayo pia ni sheria batili kama ilivyo sheria yetu ya uchaguzi, lakini ubatili wa sheria ya uraia, bado haujabatilishwa kwa sababu hakuna aliyefungua shauri kupinga ubatili wa sheria hii.

Kukosekana kwa uraia pacha ndicho kikwazo kikuu cha Diaspora wa Tanzania kushindwa kuja kuwekeza nyumbani na hata kuchanua na kung’ara huko walipo.

Nikiwa nchini Marekani kwa ziara binafsi, nimejitahidi kujichanganya na baadhi ya wanadiaspora wa Tanzania walioko nchini Marekani na kujiuliza je, wanadiaspora wetu, wanafanya nini cha kueleweka na cha kuonekana?

Nimejitahidi kuwasiliana na kile chama cha DICOTA, sikubahatika kupata ushirikiano mzuri, lakini nitaendelea kuwatafuta Diaspora wetu waliofanikiwa Marekani, wanafanya nini, na hayo mafanikio yao yanaifaidisha vipi nchi yao ya Tanzania?

Kwa kupitia juhudi binafsi, nimefanikiwa kumuona dada mmoja wa Kitanzania, aliyehamia Marekani mwaka 1999 na yuko Marekani mpaka leo.

Huyu dada ni mmiliki wa kampuni inayofanya biashara ya huduma, services industry, ameajiri watu zaidi ya 50, kila mwezi anawalipa mishahara ya zaidi ya milioni 500.

Dada kanikaribisha kwake, anakaa mtaa wa kitajiri, anamiliki nyumba kubwa ya ghorofa tatu na ana magari matano ya kifahari, ikiwemo Benzi ya G Wagon na gari ya Kimarekani ya Tesla inayotumia umeme. Hesabu ya haraka haraka ya thamani ya magari ni zaidi ya Sh1 bilioni za Kitanzania.

Huu ni mfano mmoja tu wa Mtanzania aliyefanikiwa Marekani, ametoa ajira kwa watu na kutengeneza faida kubwa. Nilipomuuliza kwa nini asiwekeze Tanzania, alinijibu anasubiria uraia pacha, ndipo aje kuwekeza Tanzania.

Muda aliokuja Marekani huyu dada, mwaka 1999, ni muda huo Mkenya, Kevin Onyona alihamia Marekani na kuajiriwa na Home Depot, kampuni ya kimataifa ya uboreshaji wa nyumba ya Marekani.

Sasa hivi ni mmiliki ya migahawa ya Swahili Village ambayo ni moja wapo ya migahawa bora zaidi ya vyakula vya Kiafrika nchini Marekani.

Kevin Onyona alianzisha mlolongo huo mwaka wa 2016 na leo anajivunia migahawa mitatu. Miaka sita baadaye, ametumia migahawa yake kujenga uhusiano halisi kati ya utamaduni wa Kiafrika na dunia nzima.

Mgahawa mkuu wa Swahili Village unapatikana Rhode Island Ave, Beltsville. Migahawa mingine miwili iko Washington DC na New Jersey. Mgahawa wa Washington DC ulifunguliwa na Rais mstaafu, Uhuru Kenyatta, kiongozi gani wa Kitanzania aliwahi kufungua mradi wowote wa Diaspora nje ya nchi?

Wito kwa Diaspora wetu, najua kuna uwezekano kuna mambo makubwa mazuri ya kuonekana ambayo Diaspora wa Tanzania wanafanya, natoa wito kwa Diaspora wetu, onekaneni basi.

Wito kwa Serikali yetu kuharakisha mkakati wa uraia pacha ili Diaspora wa Tanzania waliofanikiwa ughaibuni, waje kuwekeza nyumbani Tanzania na kurudisha shukrani nyumbani Tanzania.

Mimi kama Mtanzania Mzalendo, ninaumia sana kila ninapoona diaspora wa wenzetu wanafanya mambo makubwa ya kuonekana na kujiuliza Diaspora wetu wanafanya nini? Mbona hatuwaoni? Hivyo, napenda kuona Tanzania tunafaidika na mchango wa wanadiaspora wetu wenye exposure kubwa huko walipo, kuitumia kulisaidia taifa letu kisiasa, kiuchumi cha kijamii.