Watanzania wenye uraia wa nchi nyingine kupewa hadhi maalumu 2024

Muktasari:

  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amezungumzia mikakati mbalimbali ya wizara hiyo kwa mwaka ujao 2024 ikiwemo kukamilisha kwa mchakato wa hadhi maalumu kwa Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora)

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema mchakato wa hadhi maalumu kwa Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) utakamilika mwakani.

Amesema hadhi maalumu itaanza kutumika mwakani ambapo kupitia hadhi hiyo Watanzania wataanza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo ya Tanzania.

“Tutatangaza hadhi maalumu na stahili mahususi kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi, wenye asili ya Tanzania ambao wana uraia wa nchi nyingine kuanza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo ya nchi yao.

“Lakini pia na ustawi wao binafsi ambao unawaunganisha wao na nchi yao,” amesema Waziri Makamba wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Desemba 17, 2023 katika ofisi za wizara hiyo kuhusu utekelezaji wa Diplomasia ya Tanzania.

Katika kuhakikisha hilo, Waziri Makamba amesema kitafanyiwa mabadiliko kifungu cha sheria ya uhamiaji kinachohusu suala hilo katika mkutano ujao wa Bunge.

Akizungumzia hilo, alipotafutwa na Mwananchi , Adolph Makaya Mtanzania aishie nchini Sweden amesema ni jambo la furaha kwa kuwa wameanza kupeleka maombi muda mrefu kwa ajili ya kuwekeza nchini.

Makaya ambaye ni Katibu Mkuu Baraza la Diaspora Watanzania Duniani (TDC Global) amesema kukamilika kwa mchakato huo utawawezesha kuchangia uchumi wa nchi kwa kuwa wataanza kuwekeza bila ya wasiwasi.

“Hii itatufanya tuanze kuwekeza kwenye ardhi ikiwemo kujenga nyumba na kufungua biashara bila wasiwasi. Tumepokea hilo kwa mikono miwili kwa kuwa hata sisi tuliongojea kwa hamu,” ameeleza Makaya.

Kadhalika amesema mchakato huo utakuwa ni faida kubwa kwao kwa kuwa unawaunganisha hata Watanzania wenye uraia wa nchi nyingine.

“Historia ya jambo hili imeanza zamani, mimi nadhani kila jambo linakuja kwa wakati wake na katika hili siwezi kusema tumechelewa kwa akuwa limepelekwa kwa haraka katika miaka hii mitatu ya Rais Samia (Suluhu Hassan) hivyo tunashukuru,” ameongeza.

Awali, akiwa kwenye ziara ya siku tatu nchini Uholanzi aliyoifanya Novemba mwaka huu, Waziri Makamba alisema miongoni mwa masuala yatakayopewa kipaumbele kwenye hadhi maalumu ni haki ya kurithi au kurithishwa mali kwa diaspora hao.

Alisema ili kutekeleza hilo kuna maeneo ya sheria lazima yabadilishwe, ili watoto wa diaspora hao waweze kurithi au kumiliki ardhi.

Alisema baadhi ya masuala mengine yatakayowanufaisha watumiaji wa hadhi maalumu ni fursa na motisha mbalimbali za kuwekeza Tanzania kupitia Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC).

Makamba alibainisha mchakato wa hadhi maalumu utachangia hata kuwatambua Watanzania waishio nje ya nchi ili kurahisisha kuwarejesha nchini pindi majanga makubwa yanapotokea maeneo mbalimbali duniani.

Sera mpya ya Mambo ya Nje

Akiendelea kutoa taarifa ya utekelezaji wa diplomasia ya Tanzania, Waziri Makamba amesema Serikali itakamilisha sera mpya ya mambo ya nje ili iendane na mazingira ya sasa yaliyopo duniani.

“Kama mnavyojua kuna mabadiliko makubwa ya mwelekeo na mkao wa nchi mbalimbali duniani, hivyo imebainika kuna haja ya kubadilisha sera yetu ambayo ni ya mwaka 2001 ili iendane na mazingira ya  sasa hivyo mwakani tutakamilisha na kutoa sera mpya ya mambo ya nje,” amesema.

Mbali na hayo, Waziri Makamba amesema diplomasia ya Tanzania imeongezeka na mwakani Serikali itafungua balozi nyingine katika nchi nyingine mbili au tatu ili kupanua uwakilishi Tanzania duniani.

Amesema diplomasia ya Tanzania imeongezeka kutokana na juhudi za Serikali ya awamu ya sita ambapo kwa mwaka huu nchi imeweza kuhudhuria mikutano mbalimbali vilevile kuwa mwenyeji wa mikutano, majukwaa na makongamano mbalimbali ya kidunia.

Vilevile, kutokana na ziara za Rais Samia pia kupokea wageni mbalimbali, kama Rais wa Rwanda, Ujerumani, Hungary, Romania na Makamu wa Rais Marekani, Kamala Harris na Marais wa taasisi na mashirika mbalimbali ambapo Tanzania imepata marafiki wengi.

Vilevile amesema, mwakani Tanzania itakuwa mwenyekiti wa Taasisi ya Amani, Usalama na Ulinzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Amesema katika mwaka unaokuja wataendelea na malengo ya kidiplomasia ambayo ni kuimarisha uhusiano wa uwili kati ya Tanzania na nchi, taasisi, mashirika mbalimbali duniani, kukuza biashara uwekezaji na kuongeza utalii.

“Kutafuta fedha yani mikopo na misaada kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo ya nchi yetu ikiwemo miradi mikubwa ya kimkakati, pia kuongeza ushawishi ushiriki na sauti ya Tanzania katika masuala mtambuka yanayohitaji ushiriki wa kimataifa ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi na usawa wa kijinsia,” amesema.

Waziri Makamba amesema kuimarisha ujirani mwema na kuimarisha ushirikiano wa kikanda ikiwemo usalama na amani katika maeneo ya kikanda.