Utalii wa matibabu uwe wa viwango

Utalii wa matibabu uwe wa viwango

Muktasari:

  • Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua mitambo ya kisasa ya matibabu ya moyo kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) mwezi uliopita na kuagiza kuandaliwa kwa mazingira ya kuruhusu utalii wa matibabu, mambo yameiva sasa.

Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua mitambo ya kisasa ya matibabu ya moyo kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) mwezi uliopita na kuagiza kuandaliwa kwa mazingira ya kuruhusu utalii wa matibabu, mambo yameiva sasa.

Juzi, Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi amekabidhiwa jukumu la kuiongoza kamati ya kuhamasisha utalii huo. Wakati suala hili likianza kutekelezwa, tungependa kukumbusha mambo kadhaa muhimu yatakayosaidia kuufanya utalii kuwa wenye tija zaidi.

Afya ya mtu ni kitu muhimu zaidi, hasa yule anayeweza kutenga rasilimali zake kufuata matibabu popote yalipo duniani. Haitapendeza mgonjwa aliyetoka nje ya Tanzania kuja kutibiwa nchini akakutana na huduma mbovu popote atakapopita.

Hii inaanzia uwanja wa ndege atakakotua. Kwa kipindi hiki cha janga la corona, upimaji uwe wa kasi. Foleni zinazowaweka abiria kwa saa kadhaa hazivumiliki kwa wagonjwa. Uandaliwe utaratibu utakaowatoa abiria wa aina hiyo ndani ya muda mfupi haraka iwezekanavyo.

Kutoka uwanja wa ndege mpaka hospitali, pawe na uhakika wa usafiri. Hata kama zitatumika teksi za kawaida, madereva wapewe semina elekezi namna ya kuwahudumia watalii hao. Wafikishwe kwa wakati bila kuzungushwa.

Wakifikishwa hospitalini wajisikie wapo nyumbani. Wapokewe na madaktari na manesi wasio na msongo wa mawazo wanaoweza kuwakaripia au kutoa lugha zisizo za staha na wawepo wenye uwezo wa kuwasiliana kwa lugha mbalimbali. Wabembelezwe na kuhudumiwa kwa viwango vya kimataifa. Katika hili, tukumbuke tunashindana na mataifa makubwa kama India, Marekani na Afrika Kusini. Tukilemaa, tutakosa watalii.

Ofisi zetu za ubalozi popote zilipo, hasa ndani ya Afrika, zinapaswa kutochelewesha kwa namna yoyote visa ya utalii kwa waombaji wao.

Mchakato wa kuthibitisha kama kweli wanastahili kupewa visa hiyo ufanywe kwa haraka zaidi ili kutowakera watalii hawa.

Serikali ilikuwa inatenga mabilioni. Mwaka 2006/07, ilipeleka wagonjwa 85 kutibiwa nje ya nchi. Fedha nyingi za walipa kodi zilikuwa zinatumika kuwatibu wananchi hawa, achilia mbali waliojilipia matibabu.

Bado yapo mataifa mengi Afrika yanayopita tulikotoka, hivyo kuwapo kwa huduma nafuu kwao huenda kukawashawishi wagonjwa wanaojilipia kuja Tanzania kutetea afya zao. Muhimu ni kuhakikisha wanapata huduma walizozitarajia kwa viwango vinavyokubalika.

Tuhakikishe hospitali zitakazotumika kuwapokea na kuwahudumia wagonjwa hao zimejipanga vya kutosha kwa vifaa, wahudumu na mazingira. Wahudumu watakaotoa huduma kwa watalii hawa wajengwe kisaikolojia kutowaathiri wateja wao. Wakalimani wa lugha ya kawaida au ile ya alama waandaliwe ili watumike pindi watakapohitajika.

Wagonjwa hawa huambatana na wauguzi wao. Mahali pa kufikia ndugu au jamaa watakaoongozana nao panatakiwa kuandaliwa. Pawe na gharama zinazowezekana kwa makundi yote ya kiuchumi, isije ikaonekana mtu anashindwa kumhudumia mgonjwa wake kutokana na gharama kubwa.

Taarifa ziwe wazi kuhusu gharama za matibabu na malazi kwa mgonjwa na watu atakaoambatana nao kutoa nafasi ya kujiandaa vyema ili isitokee mtalii akashtukizwa na gharama mpya akishafika nchini.

Utalii huu ukiwa shirikishi kwa mamlaka na vyombo vyote vya umma na binafsi, Tanzania inaweza kuwa kinara kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kuvutia utalii kutokana na ubora wa huduma zake.