Vita vya viwanda bubu vipiganwe na wote

Ongezeko la viwanda bubu vinavyozalisha bidhaa mbalimbali nchini, limeelezwa kuwa pigo kwa wazalishaji halisi kwa kuwa linasababisha ongezeko la bidhaa bandia sokoni.

Licha ya jitihada kadha ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali, bado viwanda bubu vimeendelea kuwa tishio kwa wazalishaji wa bidhaa halisi na kuikosesha Serikali mapato.

Pia, bidhaa bandia kama za dawa, mbolea na vifaa vingine vya ujenzi zimeathiri ujenzi wa uchumi na usalama wa fedha na maisha ya watu. 

Mfano, majanga kama ya moto hasa kwenye makazi ya watu mengi yanaelezwa chanzo chake ni hitilafu ya umeme, ambayo mara nyingi inatokana na vifaa bandia au visivyo na ubora vilivyotumika kutengeneza mifumo ya umeme kwenye nyumba.

Tunafahamu Serikali imekuwa ikifanya juhudi kadhaa kupambana na viwanda bubu, lakini tunaona juhudi zinapaswa kuendana na adhabu kali kwa wahusika.

Mamlaka husika kama vile Shirika la Viwango Tanzania (TBS ) na Tume ya Ushindani (FCC) zimefanya juhudi kubwa kuelemisha umma na kuchukua hatua za kisheria ya utengenezaji wa bidhaa bandia unaotokana na viwanda bubu, bado juhudi hizo hazijaleta mafanikio makubwa.

Tunafahamu kuna bidhaa bandia zinazotoka nje ya nchi, lakini ndani ya nchi kuna viwanda bubu vingi vinavyotengeneza bidhaa mbalimbali na hasa pombe kali na vinywaji baridi kama juisi, maji na vitafunwa kama biskuti na nyingine zinazotoka kwa wingi.

Kutokana na kuongezeka wimbi la viwanda bubu, tunawaomba wananchi kushirikiana na Serikali kuvifichua viwanda hivi kwa kuwa kuviacha viendelee kuzalisha bidhaa hizo ni kuikosesha Serikali mapato na kuweka haki ya mlaji mtegoni.

Afya za Watanzania wengi ziko shakani na wanaoumwa maradhi kama yale yasiyo ambukiza wanaelezwa yanatokana na mtindo wa maisha na hasa ulaji wa vyakula vya viwandani na pombe kupita kiasi, zikiwemo zisizo na ubora.

Watanzania wanatakiwa kufahamu miongoni mwa mambo yanayowasababishia kudhoofu kiafya ni biadhaa bandia, hivyo kuna umuhimu wa kila mmoja kushiriki kupiga vita uwepo wa viwanda bubu wa kutoa taarifa kwenye mamlaka.

Tunawashauri watendaji serikalini kujenga uaminifu pale wananchi wanapotoa taarifa kuhusu uwapo wa viwanda bubu, haitakuwa na maana taarifa za wananchi zikatumika kwa wasio waaminifu kama njia ya kupata rushwa.

Rai yetu kwa watendaji wa Serikali waongeze ukaguzi na kushirikisha jamii ngazi ya chini hata kwa kuunda vikundi vya kulinda uchumi na uchafuzi wa mazingira, sababu viwanda bubu pia vinachafua mazingira, ikiwezekana kwa kutoa motisha za aina mbalimbali.

Tunaamini uanzishwaji wa vikundi vya kulinda uchumi na mazingira ngazi za Serikali za Mitaa itaweza kusaidia kuwabaini wenye nia ovu, wanaonzisha viwanda bila kufuata taratibu za kisheria.

Wananchi wafahamu kwamba kujishughulisha na bidhaa bandia ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria waingizaji, wanaohifadhi, wanaosambaza na wanaonunua wanakuwa wametenda kosa hilo.

Tunachoona pamoja na adhabu kuwa ya faini kati ya Sh10 milioni na Sh50 milioni au kifungo jela kati ya miaka mitano hadi 10; wanaokamatwa wengi hawapati adhabu hiyo.

Kumekuwa na matamko mengi ya kupinga viwanda bubu na bidhaa bandia, lakini mara nyingi kesi za namna hiyo hufahamika pale tu wanapokamtwa, tubadilike.