Waraka wa Zitto Kabwe kwa Rais Samia kuhusu SGR Kigoma
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuzindua rasmi ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Tabora hadi Kigoma wiki hii. Hatua kubwa, muhimu na ya kupongeza. Ujenzi wa Reli ya Kisasa imekuwa kilio cha watu wa Kigoma kwa muda mrefu. Hakuna namna tumefikiwa sasa, japo kwa kuchelewa. Tunashukuru.
Hata hivyo, watu wa Kigoma hatukulilia reli ya kisasa ilimradi reli, la hasha. Tumekuwa tukipigania kupata reli kwa sababu Kigoma ni kituo muhimu sana cha biashara katika eneo la maziwa makuu. Bandari ya Kigoma imeonyesha uwezo mkubwa wa kustahimili changamoto zote na ndiyo bandari inayokua kwa kasi zaidi kuliko nyingine zote za Tanzania. Kigoma ni mlango wa magharibi wa nchi yetu ikihudumia mashariki ya Congo DR ambapo kuna utajiri mkubwa wa madini.
Usafiri wa reli kwenda Kigoma ni lazima uende sambamba na usafiri wa maji katika Ziwa Tanganyika ili kubeba mzigo kutoka mashariki ya DRC kuelekea Bandari ya Dar es Salaam. Hivyo zinahitajika meli kubwa na nyingi kubeba mzigo huo.
Umbali mfupi tu kutoka eneo ambalo Rais ataweka jiwe la msingi la SGR kuna mradi ambao unapaswa kuwa kiunganishi muhimu na cha mkakati kwa mradi huu. Mradi huo ni chelezo, yaani kiwanda cha meli katika eneo la Katabe, kata ya Bangwe.
Mradi huu wa thamani ya zaidi ya Sh600 bilioni umesimama tangu mwaka 2023. Bila mradi huu SGR inakuwa haina maana, kwani itabaki kuwa treni ya abiria tu na si mizigo. Hakika maendeleo ya mradi wa chelezo cha meli cha Katabe yamesimamishwa kwa kiasi kikubwa na ugonjwa unaojulikana sana: ukosefu wa fedha.
Takwimu zinasimulia hadithi ya kukatisha tamaa sana. Mradi wa chelezo uliozinduliwa Oktoba 2023 kwa mkataba na Kampuni ya kutoka Uturuki iitwayo Dearsan, uliundwa kujenga na kuhudumia meli za tani 3,000–3,500 za mzigo. Uzito huu ulizingatia na kufungamanishwa na uwezo na saizi inayohitajika kuunganishwa na SGR.
Meli hizo zimeundwa kwa ufanisi wa 'roll-on/roll-off' yaani zinaweza kubeba mabehewa 25 ya reli au magari marefu pamoja na magari 65 madogo. Mradi wa chelezo ulipaswa kukamilika baada ya miezi 36 kwa mujibu wa mkataba.
Ikiwa imeshasaini mkataba wa ujenzi wa Chelezo, Serikali kupitia mamlaka ya Bandari Tanzania ikaingia mkataba wa kimkakati na kampuni kubwa sana ya madini ya nchini China iitwayo ZIJIN wa kuendesha bandari ya Kigoma.
Kampuni hii inachimba madini ya lithium katika mji wa Manono, karibu 400km kutoka mji wa Kalemie, ikiwa na lengo la kuzalisha tani milioni 5 kwa mwaka. Mzigo huu wote utapita Kigoma. Hata mradi haujaanza ukuaji wa Bandari ya Kigoma ni mkubwa. Mfano kati ya 2024-2025 mizigo iliyohudumiwa imeongezeka kwa asilimia 300. Kusafirisha mzigo huu kwa magari kunahitaji malori makubwa 3,400 ya kubeba tani 30 kila siku kati ya Kigoma na Dar es Salaam.
Muda wa miezi 36 wa kujenga chelezo na ujenzi wa meli haukuwa bahati mbaya au muda tu wa mkataba. Bali ulionyesha maono ya kimkakati ya uhamishaji kutoka reli hadi ziwa, kupunguza gharama za usafirishaji kutoka takriban dola 6,000 kwa tani hadi dola 4,000 na kufungua Ukanda wa kati wa Tanzania (central corridor) kwa DRC na kaskazini mwa Zambia.
Muda huu uliendana kabisa na muda wa kuanza uzalishaji wa madini ya lithium nchini DRC. Mwezi huu wa Julai uzalishaji umeanza na kwa sasa hakuna meli za kutosha kubeba mzigo kuuleta Kigoma na baadaye Bandari ya Dar es Salaam.
Maono hayo wakati wa kupanga mradi yamefifia kwani chelezo hakijajengwa na meli zilizopo ni chache zinazomilikiwa na kampuni tanzu ya kampuni ya Zijin. Tanzania inacheleweshwa kufaidika na jiografia yake kwa sababu moja: Warasimu wa Serikali wanasema hakuna fedha. Fedha kiduchu kulinganisha na mabilioni ya dola za Marekani ambazo Taifa lingepata.
DRC pekee ina uwezo wa kupitisha zaidi ya tani milioni 20 za mizigo ya usafirishaji wa kila mwaka katika Bandari ya Kigoma na Dar es Salaam, ikijumuisha tani milioni tano kutoka mgodi mmoja tu wa lithiam wa Manono, mkoa wa Tanganyika, DRC kama nilivyofafanua hapo juu.
Mwaka 2025 Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia mizigo tani milioni 27 kwa ujumla wake. Lango moja tu la Kigoma lingeongeza mzigo kwa bandari hiyo kwa takribani sawa na mzigo wote unaopita Bandari ya Dar es Salaam hivi sasa. Ninashindwa kuelewa inakuwaje Serikali iliyojaa wataalamu wa kila namna inashindwa kuliona hili na kuachia mradi muhimu wa Chelezo Katabe usimame. Haingii akilini!
Jiografia ya Tanzania ni moja ya faida kubwa zisizotumika ipasavyo barani Afrika. Kwa miaka mingi nimekuwa nikiandika kwamba eneo la kijiografia ni hatima katika maendeleo. Nchi yetu, inayohudumia moja kwa moja DRC, Burundi, Rwanda, Uganda, Malawi na Zambia, inapaswa kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji kwa Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na eneo lote la Maziwa Makuu. Badala yake, urasimu, ukosefu wa uratibu na majibu mepesi ya "hakuna fedha" vinaendelea kuchelewesha maendeleo ya kasi ya nchi yetu.
Tutaifikiaje Dira ya Maendeleo 2050 ya uchumi wa dola trilioni moja kwa mwendo huu? Je, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) na Waziri wa Fedha wanajua uwepo wa mradi huu? Kama wanaujua, wanawezaje kulala usingizi huku wakiona mradi umesimama?
Kusimama kwa ujenzi wa chelezo cha Katabe, pamoja na kiwanda cha meli Kigoma, kunadhihirisha ugonjwa mkubwa wa kutokuwapo kwa uratibu wa kimkakati kati ya taasisi za Serikali.
Shirika la Meli Tanzania (MSCL) lilitia saini mkataba na Kampuni ya Dearsan, lakini upungufu wa fedha umesimamisha kazi baada ya miaka miwili tu. Wakati huohuo, Shirika la Reli Tanzania (TRC) linaendelea na ujenzi wa sehemu ya kilomita 506 ya reli ya kisasa ya Tabora–Kigoma (SGR Lot 6).
Miradi hii miwili ilichukuliwa kuwa mapacha wanaotegemeana: reli ikileta mizigo hadi vituo maalumu vya Kigoma, ambapo mabehewa yangeingia moja kwa moja kwenye meli zinazojengwa na kutunzwa katika chelezo. Meli zingesafirisha mizigo hadi Kalemie, DRC, kushusha mizigo na kupakia madini kwa ajili ya kuyasafirisha Kigoma na hatimaye Bandari ya Dar es Salaam. Meli hizi zingepunguza muda wa safari ya majini kati ya Kigoma na Kalemie kutoka saa 24 hadi saa sita tu.
Iweje leo Serikali hiyo hiyo, kupitia wizara hiyo hiyo, impeleke Mkuu wa Nchi kuzindua ujenzi wa reli wakati mradi wake pacha umesimama kwa miaka mitatu? TRC na MSCL zote ziko chini ya wizara moja. Wizara hiyo inamweleza nini Rais? Isije ikawa hata reli hii ya SGR itazinduliwa ujenzi wake, halafu baadaye isimame kama ilivyotokea kwa chelezo cha Katabe.
Kiwanda hiki cha meli na chelezo chake, kilichokusudiwa kutoa ajira 1,000 kila siku kwa wananchi wa Kigoma na kubadilisha kabisa uchumi wa mji huo, kilipaswa kuwa mradi wa kuonyesha imani kwa wananchi wa Kigoma kwamba si watu wa kukumbukwa mwisho wa maendeleo. Umeme wa gridi ulifika Kigoma ikiwa miongoni mwa mikoa ya mwisho, barabara za kuunganisha mkoa huo zilichelewa, reli ya kisasa imefika baadaye kuliko maeneo mengine, na sasa kuna dalili za kucheleweshwa kwa makusudi kwa mradi wa chelezo kiasi kwamba reli inaweza kukosa manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi wa Kigoma.
Ujio wa Rais Kigoma wiki hii unapaswa kuwa fursa ya kutafakari, si ya sherehe pekee. Kufanya sherehe za uzinduzi ni jambo jepesi. Kuhakikisha mfumo mzima wa usafiri unafanya kazi kwa ufanisi ndiyo mtihani wa kweli wa uongozi. Maendeleo ya Tanzania hayawezi kupatikana kwa kufanya kazi katika "silos". Miradi lazima ipangwe kwa mpangilio sahihi (sequencing), ifadhiliwe kwa uthabiti na isimamiwe kama mifumo iliyounganishwa. Miradi lazima isomane. Kuchelewa kwa Chelezo cha Katabe ni dalili kwamba miradi hii miwili pacha haisomani na pengine, hakuna mkakati mahususi wa kuitekeleza kwa pamoja.
Wakazi wa Kigoma na maelfu ya vijana wanaotafuta ajira wanastahili huduma bora zaidi kutoka kwa serikali yao. Ajira 1,000 kwa vijana wa Kigoma zingezalisha maelfu ya ajira nyingine kupitia athari chanya za matumizi ya walioajiriwa. Wakulima wangefaidika, sekta ya huduma ingekua kwa kasi, na vijana wengi wangejenga makazi yao, jambo ambalo lingeongeza mahitaji ya vifaa vya ujenzi. Kile kinachoitwa multiplier effect katika nadharia za uchumi kingeonekana wazi kupitia mradi huu.
Ombi muhimu kwa Rais Samia katika ziara yake hii ni kutembelea eneo la Katabe na kutaka majibu kutoka kwa wasaidizi wake kuhusu namna ya kuukwamua mradi huu muhimu wa kimkakati wa kiwanda cha meli. Bila mradi huu wa chelezo cha Katabe, kufika kwa Reli ya Kisasa (SGR) Kigoma kunapoteza sehemu kubwa ya umuhimu wake kulingana na manufaa yaliyokusudiwa.
Zitto Kabwe ni Kiongozi wa zamani wa ACT-Wazalendo na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Kigoma Mjini. Ni mchumi kwa taaluma anayefanya tafiti na kuandika kuhusu uchumi wa jiografia.
Makala haya ni maoni yake binafsi na siyo msimamo wa tovuti ya Mwananchi.